Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 4:1-13

Matendo 4:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

Petro na Yohane walipokuwa bado wanawahutubia watu, makuhani na mkuu wa walinzi wa hekalu pamoja na Masadukayo walifika. Walikasirika sana, maana hao mitume walikuwa wanawahubiria watu kwamba Yesu alifufuka, jambo ambalo linaonesha wazi kwamba wafu watafufuka. Basi, waliwatia nguvuni na kwa kuwa usiku ulikuwa umekaribia, wakawaweka chini ya ulinzi mpaka kesho yake. Lakini wengi kati ya wale waliosikia ujumbe wao waliamini, na idadi ya waumini ikawa imefika karibu wanaume 5,000. Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na waalimu wa sheria walikusanyika pamoja huko Yerusalemu. Walikutana pamoja na Anasi kuhani mkuu, Kayafa, Yohane, Aleksanda na wengine waliokuwa wa ukoo wa kuhani mkuu. Walipowasimamisha mitume mbele yao, waliwauliza, “Nyinyi mmefanya jambo hili kwa nguvu gani na kwa jina la nani?” Hapo, Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, “Viongozi na wazee wa watu! Ikiwa mnatuuliza leo juu ya kile kitendo chema alichofanyiwa yule mtu aliyekuwa kiwete na jinsi alivyopata kuwa mzima, basi, nyinyi na watu wote wa Israeli mnapaswa kujua kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu leo, mzima kabisa, kwa nguvu ya jina lake Yesu wa Nazareti ambaye nyinyi mlimsulubisha, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Huyu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema: ‘Jiwe mlilokataa nyinyi waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.’ Wokovu haupatikani kwa mtu mwingine yeyote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye.” Hao wazee wa Baraza, wakiwa wanajua kwamba Petro na Yohane walikuwa watu wasio na kisomo wala elimu yoyote, walishangaa juu ya jinsi walivyosema kwa uhodari. Wakatambua kwamba walikuwa wamejiunga na Yesu.

Shirikisha
Soma Matendo 4

Matendo 4:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Hata walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na walinzi wa hekalu na Masadukayo wakawatokea, wakifadhaika sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri kuwa katika Yesu kuna ufufuo wa wafu. Wakawakamata, wakawaweka gerezani hadi asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni. Lakini wengi katika hao waliosikia lile neno waliamini; na hesabu ya wanaume ikawa kama elfu tano. Kesho yake, wakubwa na wazee na waandishi wakakusanyika Yerusalemu, na Anasi Kuhani Mkuu, na Kayafa pia, na Yohana na Iskanda, na wote wale waliokuwa jamaa zake Kuhani Mkuu. Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya? Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulubisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama akiwa mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.

Shirikisha
Soma Matendo 4

Matendo 4:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na akida wa hekalu na Masadukayo wakawatokea, wakifadhaika sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo wa wafu. Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni. Lakini wengi katika hao waliosikia lile neno waliamini; na hesabu ya watu waume ikawa kama elfu tano. Hata asubuhi wakubwa na wazee na waandishi wakakusanyika Yerusalemu, na Anasi Kuhani Mkuu, na Kayafa pia, na Yohana na Iskanda, na wote wale waliokuwa jamaa zake Kuhani Mkuu. Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya? Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.

Shirikisha
Soma Matendo 4

Matendo 4:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wakati Petro na Yohana walipokuwa wakisema na watu, makuhani, mkuu wa walinzi wa Hekalu na Masadukayo wakawajia, huku wakiwa wamekasirika sana kwa sababu mitume walikuwa wanawafundisha watu na kuhubiri kwamba kuna ufufuo wa wafu ndani ya Yesu. Wakawakamata Petro na Yohana na kuwatia gerezani mpaka kesho yake kwa kuwa ilikuwa jioni. Lakini wengi waliosikia lile neno waliamini, idadi yao ilikuwa yapata wanaume 5,000. Kesho yake, viongozi wa Kiyahudi, wazee na walimu wa sheria wakakusanyika Yerusalemu. Walikuwepo kuhani mkuu Anasi, Kayafa, Yohana, Iskanda, na wengi wa jamaa ya kuhani mkuu. Baada ya kuwasimamisha Petro na Yohana katikati yao, wakawauliza, “Ni kwa uwezo gani au kwa jina la nani mmefanya jambo hili?” Petro, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akajibu, “Enyi watawala na wazee wa watu, kama leo tukihojiwa kwa habari ya mambo mema aliyotendewa yule kiwete na kuulizwa jinsi alivyoponywa, ijulikane kwenu nyote na kwa watu wote wa Israeli kwamba: Ni kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulubisha lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama mbele yenu akiwa mzima kabisa. Huyu ndiye “ ‘jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa, ambalo limekuwa jiwe kuu la pembeni.’ Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” Wale viongozi na wazee walipoona ujasiri wa Petro na Yohana na kujua ya kuwa walikuwa watu wa kawaida, wasio na elimu, walishangaa sana, wakatambua kwamba hawa watu walikuwa na Yesu.

Shirikisha
Soma Matendo 4