Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 28:1-31

Matendo 28:1-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Tulipokwisha kuokoka, ndipo tulipojua ya kuwa kisiwa kile chaitwa Melita. Wenyeji wakatufanyia fadhili zisizokuwa za kawaida. Kwa maana waliwasha moto, wakatukaribisha sote, kwa sababu ya mvua iliyonyesha na kwa sababu ya baridi. Paulo alipokuwa amekusanya mzigo wa kuni, na kuuweka motoni, nyoka akatoka kwa ajili ya ule moto akamzonga-zonga mkononi. Wenyeji walipomwona yule nyoka akilewa-lewa mkononi, wakaambiana, Hakosi mtu huyu ni mwuaji; ambaye ijapokuwa ameokoka katika bahari haki haimwachi kuishi. Lakini yeye akamtukusia motoni asipate madhara. Wao wakadhani ya kuwa atavimba au kuanguka chini kwa kufa ghafula; na wakiisha kumwangalia sana, na kuona kwamba halimpati dhara lo lote, wakageuka, wakasema kwamba yeye ni mungu. Karibu na mahali pale palikuwa na mashamba ya mkuu wa kisiwa, jina lake Publio; mtu huyu akatukaribisha kwa moyo wa urafiki, akatufanya wageni wake kwa muda wa siku tatu. Ikawa babaake Publio alikuwa hawezi homa na kuhara damu. Paulo akaingia kwake, akaomba, akaweka mikono yake juu yake, na kumpoza. Yalipokwisha kutendeka hayo wengine waliokuwa na magonjwa katika kisiwa wakaja wakapozwa; nao wakatuheshimu kwa heshima nyingi; basi tulipoabiri wakatupakilia vitu vile tulivyokuwa na haja navyo. Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Iskanderia iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha. Tukafika Sirakusa, tukakaa siku tatu. Kutoka huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na siku ya pili tukawasili Puteoli. Huko tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi tukafika Rumi. Na kutoka huko ndugu, waliposikia habari zetu, wakaja kutulaki mpaka Soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akachangamka. Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda. Ikawa baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane, hata walipokutanika akawaambia, Ndugu zangu, ningawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali nimefungwa, tokea Yerusalemu. Na hao walipokwisha kuniuliza-uliza walitaka kunifungua, kwa maana hapakuwa na sababu yo yote kwangu ya kuuawa. Lakini Wayahudi walipotoa hoja juu ya shauri hili nalishurutishwa kutaka rufani kwa Kaisari. Si kwamba nalikuwa na neno la kuwashitaki watu wa taifa langu. Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli. Wale wakamwambia, Sisi hatukupata nyaraka zenye habari zako kutoka Uyahudi, wala hapana ndugu hata mmoja aliyefika hapa na kutupasha habari, au kunena neno baya juu yako. Lakini tunataka kusikia kwako uonavyo wewe; kwa maana katika habari za madhehebu hiyo imejulikana kwetu kwamba inanenwa vibaya kila mahali. Wakiisha kuagana naye siku, wakamjia katika nyumba aliyokaa, watu wengi sana, akawaeleza kwa taratibu na kuushuhudia ufalme wa Mungu, akiwaonya mambo yake Yesu, kwa maneno ya sheria ya Musa na ya manabii, tangu asubuhi hata jioni. Wengine waliamini yale yaliyonenwa, wengine hawakuyaamini. Na walipokuwa hawapatani wao kwa wao, wakaenda zao, Paulo alipokwisha kusema neno hili moja, ya kwamba, Roho Mtakatifu alinena vema na baba zetu, kwa kinywa cha nabii Isaya, akisema, Enenda kwa watu hawa, ukawaambie, Kusikia, mtasikia wala hamtafahamu; Na kuona, mtaona wala hamtatambua; Kwa maana mioyo ya watu hawa imepumbaa, Na masikio yao ni mazito ya kusikia, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Na kusikia kwa masikio yao, Na kufahamu kwa mioyo yao, Na kubadili nia zao, nikawaponya. Basi ijulikane kwenu ya kwamba wokovu huu wa Mungu umepelekwa kwa Mataifa, nao watasikia! [ Alipokwisha kusema hayo, Wayahudi wakaenda zao, wakiulizana mengi wao kwa wao.] Akakaa muda wa miaka miwili mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.

Shirikisha
Soma Matendo 28

Matendo 28:1-31 Biblia Habari Njema (BHN)

Tulipokwisha fika salama kwenye nchi kavu, tuligundua kwamba kile kisiwa kinaitwa Malta. Wenyeji wa hapo walikuwa wema sana kwetu. Mvua ilikuwa inaanza kunyesha na kulikuwa na baridi, hivyo waliwasha moto, wakatukaribisha. Paulo aliokota mzigo mdogo wa kuni akawa anazitia motoni. Hapo, kwa sababu ya lile joto la moto, nyoka akatoka katika kuni akamnasa Paulo mkononi na kujishikilia hapo. Wenyeji wa pale walipokiona kile kiumbe kinaninginia kwenye mkono wake waliambiana, “Bila shaka mtu huyu amekwisha ua mtu, na ingawa ameokoka kuangamia baharini, ‘Haki’ haitamwacha aendelee kuishi!” Lakini Paulo alikikungutia kile kiumbe motoni na hakuumizwa hata kidogo. Wale watu walikuwa wakitazamia kwamba angevimba au angeanguka chini na kufa ghafla. Baada ya kungojea kwa muda mrefu bila kuona kwamba Paulo amepatwa na jambo lolote lisilo la kawaida, walibadilisha fikira zao juu yake, wakasema kuwa yeye ni mungu. Karibu na mahali pale palikuwa na mashamba ya Publio, mkuu wa kile kisiwa. Publio alitukaribisha kirafiki, tukawa wageni wake kwa siku tatu. Basi, ikawa kwamba baba yake Publio alikuwa amelala kitandani, mgonjwa wa homa na kuhara. Paulo alikwenda kumwona na baada ya kusali, akaweka mikono yake juu ya mgonjwa, akamponya. Kutokana na tukio hilo, wagonjwa wote katika kile kisiwa walikuja wakaponywa. Watu walitupatia zawadi mbalimbali na wakati tulipoanza tena safari, walitia ndani ya meli masurufu tuliyohitaji. Baada ya miezi mitatu tulianza tena safari yetu kwa meli moja ya Aleksandria iitwayo “Miungu Pacha”. Meli hiyo ilikuwa imetia nanga kisiwani wakati wote wa baridi. Tulifika katika mji wa Sirakusa, tukakaa hapo kwa siku tatu. Toka huko tulingoa nanga, tukazunguka na kufika Regio. Baada ya siku moja, upepo ulianza kuvuma kutoka kusini, na baada ya siku mbili tulifika bandari ya Potioli. Huko tuliwakuta ndugu kadhaa ambao walituomba tukae nao kwa juma moja. Hivi ndivyo tulivyopata kufika Roma. Ndugu wa kule Roma walipopata habari zetu, wakaja kutulaki kwenye soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akapata moyo. Tulipofika Roma, Paulo aliruhusiwa kukaa peke yake pamoja na askari mmoja wa kumlinda. Baada ya siku tatu, Paulo aliwaita pamoja viongozi wa Kiyahudi wa mahali hapo. Walipokusanyika, Paulo aliwaambia, “Wananchi wenzangu, mimi, ingawa sikufanya chochote kibaya wala kupinga desturi za wazee wetu, nilitiwa nguvuni kule Yerusalemu na kutiwa mikononi mwa Waroma. Waliponihoji na kuona kwamba sikuwa na hatia yoyote, walitaka kuniachia. Lakini Wayahudi wengine walipinga jambo hilo, nami nikalazimika kukata rufani kwa Kaisari, ingawa sikuwa na chochote cha kuwashtaki wananchi wenzangu. Ni kwa sababu hiyo nimeomba kuonana na kuongea nanyi, maana nimefungwa minyororo hii kwa sababu ya tumaini lile la Israeli.” Wao wakamwambia, “Sisi hatujapokea barua yoyote kutoka Yudea, wala hakuna ndugu yeyote aliyefika hapa na kutoa habari rasmi au kusema chochote kibaya juu yako. Lakini tunafikiri inafaa tusikie kutoka kwako mwenyewe mambo yaliyo kichwani mwako. Kwa maana tujualo sisi kuhusu hicho kikundi ni kwamba kinapingwa kila mahali.” Basi, walipanga naye siku kamili ya kukutana, na wengi wakafika huko alikokuwa anakaa. Tangu asubuhi mpaka jioni Paulo aliwaeleza na kuwafafanulia juu ya ufalme wa Mungu, akijaribu kuwafanya wakubali habari juu ya Yesu kwa kutumia sheria na maandiko ya manabii. Baadhi yao walikubali maneno yake, lakini wengine hawakuamini. Basi, kukawa na mtengano wa fikira kati yao. Walipokuwa wanakwenda zao, Paulo alisema jambo hili: “Kweli ni sawa yale Roho Mtakatifu aliyowaarifu wazee wenu kwa njia ya nabii Isaya akisema: ‘Nenda kwa watu hawa ukawaambie: Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa; kutazama mtatazama, lakini hamtaona. Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameziba masikio yao, wamefumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa masikio yao. Wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya.’” Halafu Paulo akasema, “Jueni basi, kwamba ujumbe wa Mungu juu ya wokovu umepelekwa kwa watu wa mataifa. Wao watasikiliza!” [ Paulo alipokwisha sema hayo, Wayahudi walijiondokea huku wakiwa wanabishana vikali wao kwa wao.] Kwa muda wa miaka miwili mizima Paulo aliishi katika nyumba aliyoipanga yeye mwenyewe; akawa anawakaribisha wote waliofika kumsalimu. Alikuwa akihubiri ufalme wa Mungu na kufundisha juu ya Bwana Yesu Kristo kwa uhodari, bila kizuizi.

Shirikisha
Soma Matendo 28

Matendo 28:1-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Tulipokwisha kuokoka, ndipo tulipojua ya kuwa kisiwa kile chaitwa Melita. Wenyeji wakatufanyia fadhili zisizokuwa za kawaida. Kwa maana waliwasha moto, wakatukaribisha sote, kwa sababu ya mvua iliyonyesha na kwa sababu ya baridi. Paulo alipokuwa amekusanya mzigo wa kuni, na kuuweka motoni, nyoka akatoka kwa ajili ya ule moto akamzongazonga mkononi. Wenyeji walipomwona yule nyoka akilewalewa mkononi, wakaambiana, Hakosi mtu huyu ni mwuaji; ambaye ijapokuwa ameokoka katika bahari haki haimwachi kuishi. Lakini yeye akamtukusia motoni asipate madhara. Wao wakadhani ya kuwa atavimba au kuanguka chini kwa kufa ghafla; na wakiisha kumwangalia sana, na kuona kwamba halimpati dhara lolote, wakageuka, wakasema kwamba yeye ni mungu. Karibu na mahali pale palikuwa na mashamba ya mkuu wa kisiwa, jina lake Publio; mtu huyu akatukaribisha kwa moyo wa urafiki, akatufanya wageni wake kwa muda wa siku tatu. Ikawa babake Publio alikuwa akiugua homa na kuhara damu. Paulo akaingia kwake, akaomba, akaweka mikono yake juu yake, na kumponya. Yalipokwisha kutendeka hayo wengine waliokuwa na magonjwa katika kisiwa wakaja wakaponywa; nao wakatuheshimu kwa heshima nyingi; basi tulipoabiri wakatupakilia vitu vile tulivyokuwa na haja navyo. Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Aleksandria iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha. Tukafika Sirakusa, tukakaa siku tatu. Kutoka huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na siku ya pili tukawasili Puteoli. Huko tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi ndivyo tulifika Rumi. Na kutoka huko ndugu, waliposikia habari zetu, wakaja kutulaki mpaka Soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akachangamka. Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda. Ikawa baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane, na walipokutanika akawaambia, Ndugu zangu, ningawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu, nilitiwa katika mikono ya Warumi, nikiwa nimefungwa, tokea Yerusalemu. Na hao walipokwisha kunihoji walitaka kunifungua, kwa maana hapakuwa na sababu yoyote kwangu ya kuuawa. Lakini Wayahudi walipotoa hoja juu ya shauri hili nilishurutishwa kutaka rufani kwa Kaisari. Si kwamba nilikuwa na neno la kuwashitaki watu wa taifa langu. Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli. Wale wakamwambia, Sisi hatukupata nyaraka zenye habari zako kutoka Yudea, wala hapana ndugu hata mmoja aliyefika hapa na kutupasha habari, au kunena neno baya juu yako. Lakini tunataka kusikia kwako uonavyo wewe; kwa maana kuhusu madhehebu hiyo imejulikana kwetu kwamba inanenwa vibaya kila mahali. Wakiisha kupanga naye siku, wakamjia katika nyumba aliyokaa, watu wengi sana, akawaeleza kwa taratibu na kuushuhudia ufalme wa Mungu, akiwaonya mambo yake Yesu, kwa maneno ya Sheria ya Musa na ya manabii, tangu asubuhi hadi jioni. Wengine waliamini yale yaliyonenwa, wengine hawakuyaamini. Na walipokuwa hawapatani wao kwa wao, wakaenda zao, Paulo alipokwisha kusema neno hili moja, ya kwamba, Roho Mtakatifu alinena vema na baba zetu, kwa kinywa cha nabii Isaya, akisema, Nenda kwa watu hawa, ukawaambie, Kusikia, mtasikia wala hamtafahamu; Na kuona, mtaona wala hamtatambua; Kwa maana mioyo ya watu hawa imepumbaa, Na masikio yao ni mazito ya kusikia, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Na kusikia kwa masikio yao, Na kufahamu kwa mioyo yao, Na kubadili nia zao, nikawaponya. Basi ijulikane kwenu ya kwamba wokovu huu wa Mungu umepelekwa kwa Mataifa, nao watasikia! [ Alipokwisha kusema hayo, Wayahudi wakaenda zao, wakiulizana mengi wao kwa wao.] Akakaa muda wa miaka miwili kamili katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.

Shirikisha
Soma Matendo 28

Matendo 28:1-31 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya kufika nchi kavu salama, ndipo tukafahamu kwamba jina la kile kisiwa ni Malta. Wenyeji wa kile kisiwa wakatufanyia ukarimu usio wa kawaida. Waliwasha moto na kutukaribisha sisi sote kwa sababu mvua ilikuwa inanyesha na kulikuwa na baridi. Paulo alikuwa amekusanya mzigo wa kuni na alipokuwa anaweka kwenye moto kwa ajili ya joto, nyoka mwenye sumu akatoka humo na kujisokotea mkononi mwake. Wale wenyeji wa kile kisiwa walipomwona yule nyoka akiningʼinia mkononi mwa Paulo, wakaambiana, “Huyu mtu lazima awe ni muuaji, ingawa ameokoka kutoka baharini, haki haijamwacha aishi.” Lakini Paulo akamkungʼutia yule nyoka ndani ya moto wala yeye hakupata madhara yoyote. Watu walikuwa wanangoja avimbe au aanguke ghafula na kufa. Lakini baada ya kungoja kwa muda mrefu na kuona kwamba hakuna chochote kisicho cha kawaida kilichomtokea, wakabadili mawazo yao na kuanza kusema kwamba yeye ni mungu. Basi karibu na sehemu ile, palikuwa na shamba kubwa la mtu mmoja kiongozi wa kile kisiwa, aliyeitwa Publio. Alitupokea na akatuhudumia kwa ukarimu mkubwa kwa muda wa siku tatu. Baba yake Publio alikuwa mgonjwa kitandani, akiwa anaumwa homa na kuhara damu. Paulo akaingia ndani ili kumwona na baada ya maombi, akaweka mikono juu yake na kumponya. Jambo hili lilipotukia, watu wote wa kisiwa kile waliokuwa wagonjwa wakaja, nao wakaponywa. Wakatupa heshima nyingi, nasi tulipokuwa tayari kusafiri kwa njia ya bahari, wakapakia melini vitu vyote tulivyokuwa tunavihitaji. Miezi mitatu baadaye tukaanza safari kwa meli iliyokuwa imetia nanga kwenye kisiwa hicho kwa ajili ya majira ya baridi. Hii ilikuwa meli ya Iskanderia yenye alama ya miungu pacha waitwao Kasta na Poluksi. Kituo chetu cha kwanza kilikuwa Sirakusa na tukakaa huko siku tatu. Kisha tukangʼoa nanga, tukafika Regio. Siku iliyofuata, upepo mkali wa kusi ukavuma, na siku ya pili yake tukafika Puteoli. Huko tukawakuta ndugu, nasi tukakaribishwa tukae nao kwa siku saba. Hivyo tukaendelea na safari mpaka Rumi. Ndugu wa huko Rumi waliposikia habari zetu, walikuja mpaka Soko la Apio na mahali paitwapo Mikahawa Mitatu kutulaki. Paulo alipowaona, alimshukuru Mungu akatiwa moyo. Tulipofika Rumi, Paulo aliruhusiwa kuishi peke yake akiwa na askari wa kumlinda. Siku tatu baadaye Paulo akawaita pamoja viongozi wa Kiyahudi. Walipokwisha kukusanyika akawaambia, “Ndugu zangu, ingawa sikufanya jambo lolote dhidi ya watu wetu au dhidi ya desturi za baba zetu, lakini nilikamatwa huko Yerusalemu nikakabidhiwa kwa Warumi. Wao walipokwisha kunihoji, wakataka kuniachia huru kwa sababu hawakuona kosa lolote nililolifanya linalostahili adhabu ya kifo. Lakini Wayahudi walipopinga uamuzi huo, nililazimika kukata rufaa kwa Kaisari, ingawa sikuwa na lalamiko lolote juu ya taifa langu. Basi hii ndiyo sababu nimewatumania, ili niseme nanyi. Kwa kuwa ni kwa ajili ya tumaini la Israeli nimefungwa kwa minyororo.” Wakamjibu, “Hatujapokea barua zozote kutoka Uyahudi zinazokuhusu, wala hapana ndugu yeyote aliyekuja hapa ambaye ametoa taarifa au kuzungumza jambo lolote baya juu yako. Lakini tungependa kusikia kutoka kwako unalofikiri kwa sababu tunajua kwamba kila mahali watu wanazungumza mabaya kuhusu jamii hii.” Baada ya kupanga siku ya kuonana naye, watu wengi wakaja kuanzia asubuhi hadi jioni akawaeleza na kutangaza kuhusu Ufalme wa Mungu akijaribu kuwahadithia juu ya Yesu kutoka Sheria ya Mose na kutoka Manabii. Baadhi wakasadiki yale aliyosema, lakini wengine hawakuamini. Hivyo hawakukubaliana, nao walipokuwa wanaondoka, Paulo akatoa kauli moja zaidi: “Roho Mtakatifu alinena kweli na baba zenu aliposema mambo yale yaliyomhusu Bwana Yesu kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba: “ ‘Nenda kwa watu hawa na useme, “Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa; na pia mtatazama, lakini hamtaona.” Kwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu; hawasikii kwa masikio yao, na wamefumba macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na wakasikiliza kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, na kugeuka nami nikawaponya.’ “Basi na ijulikane kwenu kwamba, huu wokovu wa Mungu umepelekwa kwa watu wa Mataifa, nao watasikiliza.” [ Naye akiisha kusema maneno haya, Wayahudi wakaondoka wakiwa na hoja nyingi miongoni mwao.] Kwa miaka miwili mizima Paulo alikaa huko kwa nyumba aliyokuwa amepanga. Akawakaribisha wote waliokwenda kumwona. Akahubiri Ufalme wa Mungu na kufundisha mambo yale yaliyomhusu Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri wote na bila kizuizi chochote.

Shirikisha
Soma Matendo 28