Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 26:1-18

Matendo 26:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, Agripa akamwambia Paulo, “Unaruhusiwa kujitetea.” Hapo Paulo alinyosha mkono wake akajitetea hivi: “Mfalme Agripa, ninajiona mwenye bahati leo kujitetea mbele yako kuhusu yale mashtaka yote ambayo Wayahudi walikuwa wamesema juu yangu. Hasa kwa vile wewe mwenyewe ni mtaalamu wa desturi za Wayahudi na migogoro yao, ninakuomba basi unisikilize kwa uvumilivu. “Wayahudi wanajua habari za maisha yangu tangu utoto, jinsi nilivyoishi tangu mwanzo kati ya taifa langu huko Yerusalemu. Wananifahamu kwa muda mrefu, na wanaweza kushuhudia, kama wakipenda, kwamba tangu mwanzo niliishi kama mmoja wa kikundi chenye siasa kali kabisa katika dini yetu, yaani kikundi cha Mafarisayo. Na sasa niko hapa nihukumiwe kwa sababu ninaitumainia ile ahadi ambayo Mungu aliwaahidi babu zetu. Ahadi hiyo ndiyo ileile inayotumainiwa na makabila kumi na mawili ya taifa letu, wakimtumikia Mungu kwa dhati mchana na usiku. Mheshimiwa mfalme, Wayahudi wananishtaki kwa sababu ya tumaini hilo! Kwa nini nyinyi mnaona shida sana kuamini kwamba Mungu huwafufua wafu? Kwa kweli mimi mwenyewe niliamini kwamba ni wajibu wangu kufanya mambo mengi kulipinga jina la Yesu wa Nazareti. Mambo hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Mimi binafsi, nikiwa nimepewa mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu, nilipata kuwatia gerezani wengi wa watu wa Mungu. Nao walipohukumiwa kuuawa, nilipiga kura ya kukubali. Mara nyingi niliwafanya waadhibiwe katika masunagogi yote nikiwashurutisha waikane imani yao. Hasira yangu kwao ilikuwa kubwa hata nikawasaka mpaka miji ya mbali. “Kwa mujibu huohuo, nilikwenda Damasko wakati mmoja, nikiwa na mamlaka na maagizo kutoka kwa makuhani wakuu. Mheshimiwa, wakati nilipokuwa njiani, saa sita mchana, niliona mwanga mkubwa kuliko wa jua ukiangaza kutoka mbinguni, ukanizunguka mimi na wale wasafiri wenzangu. Sisi sote tulianguka chini, nami nikasikia sauti ikiniambia kwa Kiebrania: ‘Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa? Unajiumiza bure kama ng'ombe anayepiga teke fimbo ya bwana wake.’ Mimi nikauliza: ‘Ni nani wewe Bwana?’ Naye Bwana akajibu: ‘Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa. Haidhuru, inuka sasa; simama wima. Nimekutokea ili nikuweke rasmi kuwa mtumishi wangu. Utawathibitishia watu wengine mambo uliyoyaona leo na yale ambayo bado nitakuonesha. Nitakuokoa na watu wa Israeli na watu wa mataifa mengine ambao mimi ninakutuma kwao. Utayafumbua macho yao na kuwawezesha watoke gizani na kuingia katika mwanga; watoke katika utawala wa Shetani, wamgeukie Mungu; ili kwa kuamini, wapate kusamehewa dhambi na kuchukua nafasi yao kati ya wale ambao wamepata kuwa watu wa Mungu.’

Shirikisha
Soma Matendo 26

Matendo 26:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Agripa akamwambia Paulo, Una ruhusa kusema maneno yako. Ndipo Paulo akanyosha mkono wake, akajitetea, Najiona nafsi yangu kuwa na heri, Ee mfalme Agripa, kwa kuwa nitajitetea mbele yako leo, katika mambo yale yote niliyoshitakiwa na Wayahudi. Hasa kwa sababu wewe unajua sana desturi na maswali yote waliyo nayo Wayahudi; kwa sababu hiyo nakuomba unisikilize kwa uvumilivu. Kwa maana Wayahudi wote wanajua maisha yangu tangu ujana, yalivyokuwa tangu mwanzo katika taifa langu huko Yerusalemu, wakinijua sana tangu mwanzo, kama wakipenda kushuhudia, ya kwamba nilikuwa Farisayo kwa kuifuata madhehebu ya dini yetu iliyo sahihi kabisa. Na sasa ninasimama hapa nihukumiwe kwa ajili ya tumaini la ahadi waliyopewa baba zetu na Mungu, ambayo kabila zetu kumi na mbili wanataraji kuifikia, wakimwabudu Mungu kwa bidii mchana na usiku. Nami ninashitakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hilo, Ee Mfalme. Kwa nini limedhaniwa kwenu kuwa ni neno lisiloaminika, kwamba Mungu awafufua wafu? Kweli, mimi mwenyewe niliona ndani ya nafsi yangu kwamba yanipasa kutenda mambo mengi yaliyopingana na jina lake Yesu Mnazareti; nami nikayafanya hayo Yerusalemu; niliwafunga wengi miongoni mwa watakatifu ndani ya magereza, nikiisha kupewa amri na wakuu wa makuhani; na walipouawa nilitoa idhini yangu. Na mara nyingi katika masinagogi yote niliwaadhibu, nikawashurutisha kukufuru; nikawaonea hasira kama mwenye wazimu, nikawaudhi hata katika miji ya ugenini. Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani; Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani niliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote. Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo. Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi. Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako; nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao; uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.

Shirikisha
Soma Matendo 26

Matendo 26:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Agripa akamwambia Paulo, Una ruhusa kusema maneno yako. Ndipo Paulo akanyosha mkono wake, akajitetea, Najiona nafsi yangu kuwa na heri, Ee mfalme Agripa, kwa kuwa nitajitetea mbele yako leo, katika mambo yale yote niliyoshitakiwa na Wayahudi. Hasa kwa sababu wewe unajua sana desturi na maswali yote waliyo nayo Wayahudi; kwa sababu hiyo nakuomba unisikilize kwa uvumilivu. Kwa maana Wayahudi wote wanajua maisha yangu tangu ujana, yaliyokuwa tangu mwanzo katika taifa langu huko Yerusalemu, wakinijua sana tangu mwanzo, kama wakipenda kushuhudia, ya kwamba nalikuwa Farisayo kwa kuifuata madhehebu ya dini yetu iliyo sahihi kabisa. Na sasa ninasimama hapa nihukumiwe kwa ajili ya tumaini la ahadi baba zetu waliyopewa na Mungu, ambayo kabila zetu kumi na mbili wanataraji kuifikia, wakimwabudu Mungu kwa bidii mchana na usiku. Nami ninashitakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hilo, Ee Mfalme. Kwa nini limedhaniwa kwenu kuwa ni neno lisilosadikika, kwamba Mungu awafufua wafu? Kweli, mimi mwenyewe naliona ndani ya nafsi yangu kwamba yanipasa kutenda mambo mengi yaliyopingamana na jina lake Yesu Mnazareti; nami nikayafanya hayo Yerusalemu; niliwafunga wengi miongoni mwa watakatifu ndani ya magereza, nikiisha kupewa amri na wakuu wa makuhani; na walipouawa nalitoa idhini yangu. Na mara nyingi katika masinagogi yote naliwaadhibu, nikawashurutisha kukufuru; nikawaonea hasira kama mwenye wazimu, nikawaudhi hata katika miji ya ugenini. Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani; Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote. Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo. Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi. Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako; nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao; uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.

Shirikisha
Soma Matendo 26

Matendo 26:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo Agripa akamwambia Paulo, “Unayo ruhusa kujitetea.” Hivyo Paulo akawaashiria kwa mkono wake, akaanza kujitetea, akasema: “Mfalme Agripa, najiona kuwa na heri kusimama mbele yako leo ninapojitetea kuhusu mashtaka yote ya Wayahudi, hasa kwa sababu unajua vyema desturi zote za Kiyahudi na ya kuwa wewe unajua kwa undani mila na masuala ya mabishano. Kwa hiyo, nakusihi unisikilize kwa uvumilivu. “Wayahudi wote wanajua jinsi nilivyoishi tangu nilipokuwa mtoto, kuanzia mwanzo wa maisha yangu katika nchi yangu na pia huko Yerusalemu. Wao wamefahamu kwa muda mrefu na wanaweza kushuhudia kama wakipenda, ya kwamba kutokana na misimamo mikali sana ya dhehebu letu kwenye dini yetu, niliishi nikiwa Farisayo. Nami sasa ni kwa sababu ya tumaini langu katika kile ambacho Mungu aliwaahidi baba zetu, ninashtakiwa leo. Hii ndiyo ahadi ambayo makabila yetu kumi na mawili yanatarajia kuiona ikitimizwa wanapomtumikia Mungu kwa bidii usiku na mchana. Ee mfalme, ninashtakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hili. Kwa nini yeyote miongoni mwenu afikiri kwamba ni jambo lisilosadikika Mungu kufufua wafu? “Mimi pia nilikuwa nimeshawishika kwamba imenipasa kufanya yote yale yaliyowezekana kupinga Jina la Yesu wa Nazareti. Nami hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Kwa mamlaka ya viongozi wa makuhani, niliwatia wengi wa watakatifu gerezani na walipokuwa wakiuawa, nilipiga kura yangu kuunga mkono. Mara nyingi nilikwenda kutoka sinagogi moja hadi ingine nikiamuru waadhibiwe, nami nilijaribu kuwalazimisha wakufuru. Katika shauku yangu dhidi yao, hata nilikwenda miji ya kigeni ili kuwatesa. “Siku moja nilipokuwa katika mojawapo ya safari hizi nikiwa ninakwenda Dameski, nilikuwa na mamlaka na agizo kutoka kwa kiongozi wa makuhani. Ilikuwa yapata adhuhuri, ee mfalme, nilipokuwa njiani, niliona nuru kutoka mbinguni kali kuliko jua, ikingʼaa kunizunguka pande zote mimi na wale niliokuwa pamoja nao. Wote tulipokuwa tumeanguka chini, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, ‘Sauli, Sauli, mbona unanitesa? Ni vigumu kwako kuupiga teke mchokoo.’ “Nikauliza, ‘Ni nani wewe, Bwana?’ “Naye Bwana akajibu, ‘Ni Mimi Yesu unayemtesa. Sasa inuka usimame kwa miguu yako. Nimekutokea ili nikuteue uwe mtumishi na shahidi wa mambo ambayo umeyaona, na yale nitakayokuonyesha. Nitakuokoa kutoka kwa watu wako na watu wa Mataifa ambao ninakutuma kwao, uyafumbue macho yao ili wageuke kutoka gizani waingie nuruni, na kutoka kwenye nguvu za Shetani wamgeukie Mungu, ili wapate msamaha wa dhambi na sehemu miongoni mwa wale waliotakaswa kwa kuniamini mimi.’

Shirikisha
Soma Matendo 26

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha