Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 24:1-21

Matendo 24:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)

Baada ya siku tano, kuhani mkuu Anania aliwasili Kaisarea pamoja na wazee kadhaa na wakili mmoja wa sheria aitwaye Tertulo. Walimwendea yule mkuu wa mkoa wakamweleza mashtaka yao juu ya Paulo. Paulo aliitwa, na Tertulo akafungua mashtaka hivi: “Mheshimiwa Felisi, uongozi wako bora umeleta amani kubwa na marekebisho ya lazima yanafanywa kwa manufaa ya taifa letu. Tunalipokea jambo hili kwa furaha daima na kutoa shukrani nyingi kwako kila mahali. Lakini, bila kupoteza wakati wako zaidi, tunakusihi kwa wema wako, usikilize taarifa yetu fupi. Tumegundua kwamba mtu huyu ni wa hatari mno. Yeye huanzisha ghasia kati ya Wayahudi kila mahali duniani na pia ni kiongozi wa kile chama cha Wanazareti. Tena alijaribu kulikufuru hekalu, nasi tukamtia nguvuni. [Tulitaka kumhukumu kufuatana na sheria yetu. Lakini Lusia, mkuu wa jeshi, aliingilia kati, akamchukua kwa nguvu kutoka mikononi mwetu. Kisha akaamuru washtaki wake waje mbele yako.] Kama ukimhoji wewe mwenyewe, utaweza kubainisha mambo haya yote tunayomshtaki kwayo.” Nao Wayahudi waliunga mkono mashtaka hayo wakisema kwamba hayo yote yalikuwa kweli. Basi, mkuu wa mkoa alimwashiria Paulo aseme. Naye Paulo akasema, “Nafurahi kujitetea mbele yako nikijua kwamba umekuwa hakimu wa taifa hili kwa miaka mingi. Unaweza kujihakikishia kwamba si zaidi ya siku kumi na mbili tu zimepita tangu nilipokwenda kuabudu Yerusalemu. Wayahudi hawakunikuta nikijadiliana na mtu yeyote. Hawakunikuta nikichochea watu hekaluni, wala katika masunagogi yao, wala mahali pengine popote katika mji huo. Wala hawawezi kuthibitisha mashtaka waliyotoa juu yangu. Ninachokubali mbele yako ni hiki: Mimi ninamwabudu Mungu wa wazee wetu nikiishi kufuatana na njia ile ambayo wao wanaiita chama cha uzushi. Ninaamini mambo yote yaliyoandikwa katika vitabu vya sheria na manabii. Mimi namtumainia Mungu, na wao wanalo tumaini hilo, kwamba watu, wema na wabaya, watafufuka. Kwa hiyo ninajitahidi daima kuwa na dhamiri njema mbele ya Mungu na mbele ya watu. “Baada ya kukaa mbali kwa miaka kadhaa, nilirudi Yerusalemu ili kuwapelekea wananchi wenzangu msaada na kutoa tambiko. Wakati nilipokuwa nikifanya hayo ndipo waliponikuta hekaluni, nilipokuwa nimekwisha fanya ile ibada ya kujitakasa. Hakukuwako kundi la watu wala ghasia. Lakini kulikuwa na Wayahudi wengine kutoka mkoa wa Asia; hao ndio wangepaswa kuwa hapa mbele yako na kutoa mashtaka yao kama wana chochote cha kusema dhidi yangu. Au, waache hawa walio hapa waseme kosa waliloliona kwangu wakati niliposimama mbele ya Baraza lao kuu, isipokuwa tu maneno haya niliyosema niliposimama mbele yao: ‘Mnanihukumu leo hii kwa sababu ya kushikilia kwamba wafu watafufuliwa!’”

Shirikisha
Soma Matendo 24

Matendo 24:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Baada ya siku tano, Anania, Kuhani Mkuu, akateremka na baadhi ya wazee pamoja naye, na msemi mmoja, Tertulo, nao wakamweleza mtawala habari za Paulo. Naye alipoitwa, Tertulo akaanza kumshitaki, akisema, Kwa kuwa mnapata amani nyingi chini yako, Feliki mtukufu, na kwa uongozi wako mambo mabaya yanasuluhishwa kwa ajili ya taifa hili, basi tunayapokea kila wakati na kila mahali, kwa shukrani yote. Lakini nisikuudhi zaidi, nakusihi utusikilize maneno machache kwa fadhili zako. Kwa maana tumemwona mtu huyu kuwa mkorofi, mwanzilishi wa fitina katika Wayahudi wote duniani, tena ni kichwa cha madhehebu ya Wanazareti. Na tena alijaribu kulitia hekalu unajisi; tukamkamata; [tukataka kumhukumu kwa sheria yetu. Lakini Lisia jemadari akafika akamwondoa mikononi mwetu kwa nguvu, Akawaamuru wale waliomshitaki waje kwako.] Wewe mwenyewe kwa kumwulizauliza utaweza kupata habari ya mambo yale yote tunayomshitaki sisi. Wayahudi nao wakamshitaki, wakisema ya kuwa ndivyo yalivyo. Na mtawala alipompungia mkono ili anene, Paulo akajibu, Kwa kuwa ninajua ya kwamba wewe umekuwa mwamuzi wa taifa hili kwa muda wa miaka mingi, najitetea mwenyewe kwa moyo wa furaha. Maana waweza kujua ya kuwa hazijapita siku zaidi ya kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu ili kuabudu. Watu hawa hawakuniona ndani ya hekalu, nikihojiana na mtu, au kufanya fujo katika mkutano, wala katika masinagogi wala ndani ya mji. Wala hawawezi kuyahakikisha mambo haya wanayonishitaki sasa. Ila neno hili naungama kwako ya kwamba kwa Njia ile ambayo waiita uzushi, ndivyo ninavyomwabudu Mungu wa baba zetu, nikiyaamini yote yanayopatana na torati na yaliyoandikwa katika vyuo vya manabii. Nina tumaini kwa Mungu, ambalo hata hao nao wanalitazamia, ya kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, wenye haki na wasio haki pia. Nami ninajizoeza katika neno hili niwe na dhamiri isiyo na hatia mbele za Mungu na mbele ya watu siku zote. Baada ya miaka mingi nilifika niwaletee watu wa taifa langu sadaka na matoleo. Wakaniona ndani ya hekalu nikishughulika na mambo haya, nilikuwa nimetakaswa, wala sikuwa na mkutano wala ghasia; lakini walikuwako baadhi ya Wayahudi waliotoka Asia, ambao imewapasa hao kuwapo hapa mbele yako na kunishitaki, kama wana neno lolote juu yangu. Au watu hawa wenyewe na waseme, ni kosa gani waliloliona kwangu niliposimama mbele ya baraza, isipokuwa kwa ajili ya sauti hii moja, nilipolia nikisimama katikati yao, na kusema, Kwa ajili ya ufufuo wa wafu ninahukumiwa mbele yenu hivi leo.

Shirikisha
Soma Matendo 24

Matendo 24:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Baada ya siku tano, Anania, Kuhani Mkuu, akatelemka na baadhi ya wazee pamoja naye, na msemi mmoja, Tertulo, nao wakamweleza liwali habari za Paulo. Naye alipoitwa, Tertulo akaanza kumshitaki, akisema, Kwa kuwa mnapata amani nyingi chini yako, Feliki mtukufu, na kwa maangalizi yako mambo mabaya yanatengenezwa kwa ajili ya taifa hili, basi tunayapokea kila wakati na kila mahali, kwa shukrani yote. Lakini nisikuudhi zaidi, nakusihi utusikilize maneno machache kwa fadhili zako. Kwa maana tumemwona mtu huyu mkorofi, mwanzilishi wa fitina katika Wayahudi wote duniani, tena ni kichwa cha madhehebu ya Wanazorayo. Na tena alijaribu kulitia hekalu unajisi; tukamkamata; [tukataka kumhukumu kwa sheria yetu. Lakini Lisia jemadari akafika akamwondoa mikononi mwetu kwa nguvu, Akawaamuru wale waliomshitaki waje kwako.] Wewe mwenyewe kwa kumwuliza-uliza utaweza kupata habari ya mambo yale yote tunayomshitaki sisi. Wayahudi nao wakamshitaki, wakisema ya kuwa ndivyo yalivyo. Na liwali alipompungia mkono ili anene, Paulo akajibu, Kwa kuwa ninajua ya kwamba wewe umekuwa mwamuzi wa taifa hili kwa muda wa miaka mingi, najitetea mwenyewe kwa moyo wa furaha. Maana waweza kujua ya kuwa hazijapita siku zaidi ya kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu ili kuabudu. Watu hawa hawakuniona ndani ya hekalu, nikihojiana na mtu, au kufanya fujo katika mkutano, wala katika masinagogi wala ndani ya mji. Wala hawawezi kuyahakikisha mambo haya wanayonishitaki sasa. Ila neno hili naungama kwako ya kwamba kwa Njia ile ambayo waiita uzushi, ndivyo ninavyomwabudu Mungu wa baba zetu, nikiyaamini yote yanayopatana na torati na yaliyoandikwa katika vyuo vya manabii. Nina tumaini kwa Mungu, ambalo hata hao nao wanalitazamia, ya kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, wenye haki na wasio haki pia. Nami ninajizoeza katika neno hili niwe na dhamiri isiyo na hatia mbele za Mungu na mbele ya watu siku zote. Baada ya miaka mingi nalifika niwaletee watu wa taifa langu sadaka na matoleo. Wakaniona ndani ya hekalu nikishughulika na mambo haya, hali nimetakaswa, wala sikuwa na mkutano wala ghasia; lakini walikuwako baadhi ya Wayahudi waliotoka Asia, ambao imewapasa hao kuwapo hapa mbele yako na kunishitaki, kama wana neno lo lote juu yangu. Au watu hawa wenyewe na waseme, ni kosa gani waliloliona kwangu niliposimama mbele ya baraza, isipokuwa kwa ajili ya sauti hii moja, nilipolia nikisimama katikati yao, na kusema, Kwa ajili ya ufufuo wa wafu ninahukumiwa mbele yenu hivi leo.

Shirikisha
Soma Matendo 24

Matendo 24:1-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya siku tano, kuhani mkuu Anania akashuka akiwa amefuatana na baadhi ya wazee pamoja na mwanasheria mmoja aitwaye Tertulo, nao wakaleta mashtaka yao dhidi ya Paulo mbele ya mtawala. Paulo alipoitwa aingie ndani, Tertulo akaanza kutoa mashtaka akisema, “Mtukufu Feliksi, kwa muda mrefu tumefurahia amani na matengenezo mengi mazuri yamefanywa kwa ajili ya watu hawa kwa sababu ya upeo wako wa kuona mambo ya mbele. Wakati wote na kila mahali, kwa namna yoyote, mtukufu sana Feliksi, tumeyapokea mambo haya yote kwa shukrani nyingi. Lakini nisije nikakuchosha zaidi, ningekuomba kwa hisani yako utusikilize kwa kifupi. “Tumemwona mtu huyu kuwa ni msumbufu, anayechochea ghasia miongoni mwa Wayahudi duniani pote. Yeye ndiye kiongozi wa dhehebu la Wanazarayo, na hata amejaribu kulinajisi Hekalu, hivyo tukamkamata; [tukataka kumhukumu kufuatana na sheria zetu. Lakini jemadari Lisia alitujia na nguvu nyingi, akamwondoa mikononi mwetu, akiwaamuru washtaki wake waje mbele yako: ili] kwa kumchunguza wewe mwenyewe unaweza kujua kutoka kwake mambo yote tunayomshtaki kwayo.” Pia wale Wayahudi wakaunga mkono wakithibitisha kuwa mashtaka yote haya ni kweli. Mtawala Feliksi alipompungia Paulo mkono ili ajitetee, yeye akajibu, “Najua kwamba wewe umekuwa hakimu katika taifa hili kwa miaka mingi, hivyo natoa utetezi wangu kwa furaha. Unaweza kuhakikisha kwa urahisi kuwa hazijapita zaidi ya siku kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu kuabudu. Hawa wanaonishtaki hawakunikuta nikibishana na mtu yeyote Hekaluni au kuchochea umati wa watu katika sinagogi au mahali pengine popote mjini. Wala hawawezi kabisa kukuthibitishia mashtaka haya wanayonishtaki kwayo. Lakini, ninakubali kwamba mimi namwabudu Mungu wa baba zetu, mfuasi wa Njia, ile ambayo wao wanaiita dhehebu. Ninaamini kila kitu kinachokubaliana na Sheria na kile kilichoandikwa katika Manabii, nami ninalo tumaini kwa Mungu, ambalo hata wao wenyewe wanalikubali kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, kwa wenye haki na wasio na haki. Kwa hiyo ninajitahidi siku zote kuwa na dhamiri safi mbele za Mungu na mbele za wanadamu. “Basi, baada ya kutokuwepo kwa miaka mingi nilikuja Yerusalemu ili kuwaletea watu wangu msaada kwa ajili ya maskini na kutoa dhabihu. Nilikuwa nimeshatakaswa kwa taratibu za kiibada waliponikuta Hekaluni nikifanya mambo haya. Hapakuwa na umati wa watu, pamoja nami wala aliyehusika kwenye fujo yoyote. Lakini kulikuwa na baadhi ya Wayahudi kutoka Asia, ambao wangelazimika wawepo hapa mbele yako ili watoe mashtaka kama wanalo jambo lolote dhidi yangu. Au, watu hawa walioko hapa waseme ni uhalifu gani walioniona nao waliponisimamisha mbele ya baraza, isipokuwa ni kuhusu jambo hili moja nililopiga kelele mbele yao kwamba, ‘Mimi nashtakiwa mbele yenu leo kwa sababu ya ufufuo wa wafu.’ ”

Shirikisha
Soma Matendo 24