Matendo 23:1-35
Matendo 23:1-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Paulo akawakazia macho watu wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hata leo hivi. Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake. Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria? Wale waliosimama karibu wakasema, Je! Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu? Paulo akasema, Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa, Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako. Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu. Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindano baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana. Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; bali Mafarisayo hukiri yote. Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, wakisema, Hatuoni uovu wo wote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema naye, ni nini? Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao, akaamuru askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome. Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako. Kulipopambauka, Wayahudi wakafanya mapatano, wakajifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala hawatakunywa hata wamwue Paulo. Na hao walioapiana hivyo walipata zaidi ya watu arobaini. Nao wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee, wakasema, Tumejifunga kwa kiapo tusionje kitu hata tumwue Paulo. Basi sasa ninyi pamoja na wazee wa baraza mwambieni jemadari amlete chini kwenu, kana kwamba mnataka kujua habari zake vizuri zaidi; na sisi tu tayari kumwua kabla hajakaribia. Mjomba wake Paulo akasikia habari za kuotea kwao, akaenda akaingia ndani ya ngome akampasha Paulo habari. Paulo akamwita akida mmoja, akasema, Mchukue kijana huyu kwa jemadari; maana ana neno la kumwarifu. Basi akamchukua, akampeleka kwa jemadari, akamwambia, Paulo, yule mfungwa, aliniita akataka nikuletee kijana huyu kwa kuwa ana neno la kukuambia. Yule jemadari akamshika mkono akajitenga pamoja naye kando, akamwuliza kwa faragha, Una neno gani utakalo kuniarifu? Akasema Wayahudi wamepatana kukuomba umlete Paulo chini kesho, ukamweke mbele ya baraza, kana kwamba wanataka kupata habari zake kwa usahihi zaidi. Basi wewe usikubali; kwa maana watu zaidi ya arobaini wanamwotea, wamejifunga kwa kiapo wasile wala wasinywe hata watakapomwua; nao sasa wako tayari, wakiitazamia ahadi kwako. Basi yule jemadari akamwacha kijana aende zake, akimwagiza, Usimwambie mtu awaye yote ya kwamba umeniarifu haya. Akawaita maakida wawili, akasema, Wekeni tayari askari mia mbili kwenda Kaisaria, na askari wapanda farasi sabini, na wenye mikuki mia mbili, kwa saa tatu ya usiku. Akawaambia kuweka wanyama tayari wampandishe Paulo, na kumchukua salama kwa Feliki liwali. Akaandika barua, kwa namna hii, Klaudio Lisia kwa liwali mtukufu Feliki, Salamu! Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi, wakawa karibu kumwua, ndipo nikaenda pamoja na kikosi cha askari nikamwokoa, nilipopata habari ya kuwa yeye ni Mrumi. Nami nikitaka kulijua lile neno walilomshitakia, nikamtelemsha nikamweka mbele ya baraza; nikaona kwamba ameshitakiwa kwa ajili ya maswali ya sheria yao, wala hakushitakiwa neno lo lote la kustahili kuuawa wala kufungwa. Hata nilipopewa habari kwamba patakuwa na vitimvi juu ya mtu huyu, mara nikampeleka kwako, nikawaagiza na wale waliomshitaki, wanene habari zake mbele yako. Wasalamu. Basi, wale askari wakamchukua Paulo kama walivyoamriwa, wakampeleka hata Antipatri usiku; hata asubuhi wakawaacha wale wapanda farasi waende pamoja naye, nao wakarudi zao ngomeni. Na wale walipofika Kaisaria, na kumpa liwali ile barua, wakamweka Paulo mbele yake. Naye alipokwisha kuisoma, akawauliza, Mtu huyu ni wa jimbo gani? Alipoarifiwa ya kuwa ni mtu wa Kilikia, akasema, Nitakusikia wewe watakapokuja wale waliokushitaki; akaamuru alindwe katika nyumba ya uliwali ya Herode.
Matendo 23:1-35 Biblia Habari Njema (BHN)
Paulo aliwakodolea macho wale wanabaraza, halafu akaanza kusema, “Ndugu zangu, mpaka hivi leo nimekuwa nikiishi na dhamiri njema mbele ya Mungu.” Hapo kuhani mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wampige kofi mdomoni. Basi, Paulo akamwambia, “Mungu mwenyewe atakupiga kofi wewe uliye kama ukuta uliopakwa chokaa! Unawezaje kukaa hapo ili unihukumu kisheria na huku wewe mwenyewe unaivunja sheria kwa kuamuru nipigwe?” Watu waliokuwa wamesimama pale wakamwambia Paulo, “Unamtukana kuhani mkuu wa Mungu!” Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kama yeye ni kuhani mkuu. Maana Maandiko yasema hivi: ‘Usiseme vibaya juu ya mtawala wa watu wako.’” Wakati huo Paulo alikwisha tambua kwamba sehemu moja ya wanabaraza wale ilikuwa ni Masadukayo na nyingine Mafarisayo. Basi, alipaza sauti yake mbele ya Baraza, “Ndugu zangu, mimi ni Mfarisayo, mwana wa Mfarisayo. Mimi nimeletwa mahakamani kwa kuwa ninatumaini kwamba wafu watafufuka.” Baada ya kusema hivyo, mzozo mkali ulitokea kati ya Mafarisayo na Masadukayo na mkutano ukagawanyika sehemu mbili. Kisa chenyewe kilikuwa hiki, Masadukayo hushikilia kwamba wafu hawafufuki, hakuna malaika, na roho nazo hazipo. Lakini Mafarisayo husadiki hayo yote matatu. Kelele ziliongezeka na baadhi ya waalimu wa sheria wa kikundi cha Mafarisayo walisimama na kutoa malalamiko yao kwa nguvu: “Hatuoni chochote kilicho kiovu katika mtu huyu; huenda ikawa kwamba roho au malaika ameongea naye.” Mzozo ulizidi kuwa mwingi hata mkuu wa jeshi akaogopa kwamba Paulo angeraruliwa vipandevipande. Kwa hiyo, aliwaamuru askari wake kuingia kati ya lile kundi, wamtoe Paulo na kumrudisha ndani ya ngome. Usiku uliofuata, Bwana alisimama karibu na Paulo, akamwambia, “Jipe moyo! Umenishuhudia hapa Yerusalemu, utafanya vivyo hivyo mjini Roma.” Kulipokucha, Wayahudi walifanya kikao cha faragha. Wakala kiapo: “Hatutakula wala kunywa mpaka tutakapokuwa tumekwisha muua Paulo.” Watu zaidi ya arubaini ndio waliokula njama kufanya hivyo. Basi, walikwenda kwa makuhani wakuu na wazee, wakasema, “Sisi tumekula kiapo kwamba hatutaonja chochote kwa vinywa vyetu mpaka hapo tutakapokuwa tumemuua Paulo. Sasa basi, nyinyi pamoja na Baraza tumeni ujumbe kwa mkuu wa jeshi ili amlete Paulo kwenu mkijisingizia kwamba mnataka kupata habari kamili zaidi juu yake. Tuko tayari kumwua hata kabla hajafika karibu.” Lakini mtoto wa ndugu yake Paulo alisikia juu ya mpango huo; hivyo akaenda ndani ya ngome, akamjulisha Paulo juu ya njama hiyo. Hapo Paulo akamwita mmoja wa maaskari, akamwambia, “Mchukue kijana huyu kwa mkuu wa jeshi; ana kitu cha kumwambia.” Askari akamchukua huyo kijana, akamwongoza mpaka kwa mkuu wa jeshi, akasema, “Yule mfungwa Paulo ameniita akaniomba nimlete kijana huyu kwako kwa maana ana jambo la kukuambia.” Mkuu wa jeshi alimshika huyo kijana mkono, akampeleka mahali pa faragha, akamwuliza, “Una nini cha kuniambia?” Yeye akasema, “Wayahudi wamepatana wakuombe umpeleke Paulo Barazani wakijisingizia kwamba Baraza lingependa kupata habari kamili zaidi juu yake. Lakini wewe usikubali kwa maana kuna watu zaidi ya arubaini walio tayari kumvamia. Wameapa kutokula wala kunywa kitu mpaka watakapokuwa wamemuua. Sasa wako tayari, wanangojea tu uamuzi wako.” Mkuu wa jeshi alimwacha aende zake akimwonya asimwambie mtu yeyote kwamba amemletea habari hizo. Basi, mkuu wa jeshi aliwaita askari wawili akawaambia, “Wekeni tayari askari 200, wapandafarasi sabini na askari 200 wa mikuki, waende Kaisarea; muwe tayari kuondoka kabla ya saa tatu leo usiku. Wekeni farasi kadhaa kwa ajili ya Paulo; mfikisheni salama kwa Felisi, mkuu wa mkoa.” Halafu mkuu huyo wa jeshi akaandika barua hivi: “Mimi Klaudio Lusia ninakuandikia wewe Mheshimiwa Felisi, mkuu wa mkoa. Salamu! “Wayahudi walimkamata mtu huyu na karibu wangemuua kama nisingalifahamishwa kwamba yeye ni raia wa Roma na hivyo nikaenda pamoja na askari nikamwokoa. Nilimpeleka mbele ya Baraza lao kuu nikitaka kujua kisa cha mashtaka yao. Niligundua kwamba mashtaka yenyewe yalihusu ubishi juu ya sehemu kadha wa kadha za sheria yao na hivyo sikuona kwamba amefanya chochote kinachostahili auawe au afungwe gerezani. Nilipofahamishwa kwamba Wayahudi walikuwa wamefanya njama za kumwua, niliamua kumleta kwako, nikawaambia washtaki wake walete mashtaka yao mbele yako.” Basi, hao askari walimchukua Paulo kama walivyoamriwa; wakampeleka usiku uleule mpaka Antipatri. Kesho yake askari wa miguu walirudi ngomeni, wakawaacha wale askari wapandafarasi waendelee na safari pamoja na Paulo. Walipofika Kaisarea walimpa mkuu wa mkoa ile barua na kumweka Paulo chini ya mamlaka yake. Felisi alipoisoma hiyo barua aliwauliza Paulo ametoka mkoa gani. Alipofahamishwa kwamba alikuwa ametoka mkoa wa Kilikia, akasema, “Nitasikiliza kesi yako baada ya washtaki wako kufika.” Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi ndani ya ukumbi wa Herode.
Matendo 23:1-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Paulo akawakazia macho watu wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hata leo hivi. Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake. Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu kulingana na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria? Wale waliosimama karibu wakasema, Je! Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu? Paulo akasema, Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa, Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako. Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu. Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindano baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana. Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; bali Mafarisayo hukiri yote. Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, wakisema, Hatuoni uovu wowote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema naye, ni nini? Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akahofia Paulo asije akararuliwa nao, akaamuru askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome. Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako. Kulipopambazuka, Wayahudi wakafanya mapatano, wakajifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala hawatakunywa hadi wamwue Paulo. Na hao walioapiana hivyo walikuwa zaidi ya watu arubaini. Nao wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee, wakasema, Tumejifunga kwa kiapo tusionje kitu hata tumwue Paulo. Basi sasa ninyi pamoja na wazee wa baraza mwambieni jemadari amlete chini kwenu, kana kwamba mnataka kujua habari zake vizuri zaidi; na sisi tuko tayari kumwua kabla hajakaribia. Mjomba wake Paulo akasikia habari za kuotea kwao, akaenda akaingia ndani ya ngome akampasha Paulo habari. Paulo akamwita ofisa mmoja, akasema, Mchukue kijana huyu kwa jemadari; maana ana neno la kumwarifu. Basi akamchukua, akampeleka kwa jemadari, akamwambia, Paulo, yule mfungwa, aliniita akataka nikuletee kijana huyu kwa kuwa ana neno la kukuambia. Yule jemadari akamshika mkono akajitenga pamoja naye kando, akamwuliza kwa faragha, Una neno gani utakalo kuniarifu? Akasema Wayahudi wamepatana kukuomba umlete Paulo chini kesho, ukamweke mbele ya baraza, kana kwamba wanataka kupata habari zake kwa usahihi zaidi. Basi wewe usikubali; kwa maana watu zaidi ya arubaini wanamwotea, wamejifunga kwa kiapo wasile wala wasinywe hadi watakapomwua; nao sasa wako tayari, wakisubiri kusikia utasemaje. Basi yule jemadari akamwacha kijana aende zake, akimwagiza, Usimwambie mtu awaye yote ya kwamba umeniambia haya. Akawaita maofisa wawili, akasema, Wekeni tayari askari mia mbili kwenda Kaisaria, na askari wapanda farasi sabini, na wenye mikuki mia mbili, kabla ya saa tatu usiku. Akawaambia kuweka wanyama tayari wampandishe Paulo, na kumchukua salama kwa Feliki mtawala. Akaandika barua, juu ya hili, Klaudio Lisia kwa mtawala mtukufu Feliki, Salamu! Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi, wakawa karibu kumwua, ndipo nikaenda pamoja na kikosi cha askari nikamwokoa, nilipopata habari ya kuwa yeye ni Mrumi. Nami nikitaka kulijua lile neno walilomshitakia, nikamteremsha nikamweka mbele ya baraza; nikaona kwamba ameshitakiwa kwa ajili ya maswali ya sheria yao, wala hakushitakiwa neno lolote la kustahili kuuawa wala kufungwa. Hata nilipopewa habari kwamba patakuwa na ghasia juu ya mtu huyu, mara nikamtuma kwako, nikawaagiza na wale waliomshitaki, wanene habari zake mbele yako. Wasalamu. Basi, wale askari wakamchukua Paulo kama walivyoamriwa, wakampeleka hadi Antipatri usiku; hata asubuhi wakawaacha wale wapanda farasi waende pamoja naye, nao wakarudi zao ngomeni. Na wale walipofika Kaisaria, na kumpa mtawala ile barua, wakamweka Paulo mbele yake. Naye alipokwisha kuisoma, akawauliza, Mtu huyu ni wa mkoa gani? Alipoarifiwa ya kuwa ni mtu wa Kilikia, akasema, Nitakusikia wewe watakapokuja wale waliokushitaki; akaamuru alindwe katika nyumba ya utawala wa Herode.
Matendo 23:1-35 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Paulo akawakazia macho wale wajumbe wa baraza, akasema, “Ndugu zangu, nimetimiza wajibu wangu kwa Mungu kwa dhamiri safi kabisa hadi leo.” Kwa ajili ya jambo hili kuhani mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa karibu na Paulo wampige kofi kinywani. Ndipo Paulo akamwambia, “Mungu atakupiga wewe, ewe ukuta uliopakwa chokaa! Wewe umeketi hapo ili kunihukumu kwa mujibu wa sheria, lakini wewe mwenyewe unakiuka sheria kwa kuamuru kwamba nipigwe kinyume cha sheria!” Wale watu waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wakamwambia, “Je, wewe wathubutu kumtukana kuhani mkuu wa Mungu?” Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kwamba yeye alikuwa kuhani mkuu. Kwa maana imeandikwa, ‘Usimnenee mabaya kiongozi wa watu wako.’ ” Paulo alipotambua ya kuwa baadhi yao walikuwa Masadukayo na wengine ni Mafarisayo, akapaza sauti kwenye baraza, “Ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana Farisayo. Hapa nimeshtakiwa kuhusu tumaini langu katika ufufuo wa wafu.” Aliposema haya, farakano likaanza kati ya Mafarisayo na Masadukayo na baraza lote likagawanyika. (Kwa maana Masadukayo wanasema kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho, lakini Mafarisayo wanaamini haya yote.) Kukawa na ghasia kubwa, nao baadhi ya walimu wa sheria ambao ni Mafarisayo, wakasimama wakapinga kwa nguvu wakisema, “Hatuoni kosa lolote la mtu huyu! Huenda ikawa roho au malaika amezungumza naye” Ugomvi ukawa mkubwa kiasi kwamba yule jemadari akahofu kuwa wangemrarua Paulo vipande vipande, akaamuru vikosi vya askari vishuke na kumwondoa Paulo katikati yao kwa nguvu na kumleta ndani ya ngome ya jeshi. Usiku uliofuata, Bwana akasimama karibu naye akamwambia, “Jipe moyo! Kama vile ulivyonishuhudia hapa Yerusalemu, hivyo imekupasa kunishuhudia huko Rumi pia.” Kulipopambazuka Wayahudi wakafanya shauri pamoja na kujifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wawe wamemuua Paulo. Waliofanya mpango huo walikuwa zaidi ya watu arobaini. Wakawaendea viongozi wa makuhani na wazee na kusema, “Tumejifunga pamoja kwa kiapo kwamba hatutakula wala kunywa mpaka tuwe tumemuua Paulo. Hivyo basi, wewe pamoja na baraza, inawapasa mkamjulishe jemadari ili amteremshe Paulo kwenu, mjifanye kama mnataka kufanya uchunguzi wa kina zaidi wa shauri lake. Nasi tuko tayari kumuua kabla hajafika hapa.” Lakini mtoto wa dada yake Paulo aliposikia juu ya shauri hilo baya, alikwenda kule kwenye ngome ya askari na kumweleza Paulo. Ndipo Paulo akamwita mmoja wa viongozi wa askari, akamwambia, “Mpeleke huyu kijana kwa jemadari, analo jambo la kumweleza.” Hivyo yule kiongozi wa askari akampeleka yule kijana kwa jemadari, akamwambia, “Paulo yule mfungwa aliniita na kuniomba nimlete huyu kijana kwako, kwa sababu ana neno la kukueleza.” Yule jemadari akamshika yule kijana mkono, akampeleka kando na kumuuliza, “Unataka kuniambia nini?” Yule kijana akasema, “Wayahudi wamekubaliana wakuombe umpeleke Paulo kwenye baraza lao kesho kwa kisingizio kwamba wanataka kufanya uchunguzi wa kina wa shauri lake. Lakini usishawishiwe nao kwa maana zaidi ya watu arobaini wanamvizia. Wamejifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wawe wamemuua Paulo. Sasa wako tayari, wanangoja idhini yako kwa ajili ya ombi lao.” Yule jemadari akamruhusu yule kijana aende na akamwonya, akisema, “Usimwambie mtu yeyote kwamba umenieleza habari hizi.” Kisha yule jemadari akawaita viongozi wake wawili wa askari akawaambia, “Jiandaeni kuondoka saa tatu usiku huu kuelekea Kaisaria pamoja na askari 200, wapanda farasi sabini na watu 200 wenye mikuki. Pia tayarisheni na farasi watakaotumiwa na Paulo, mkampeleke salama kwa mtawala Feliksi.” Kisha akaandika barua kwa Feliksi kama ifuatavyo: Klaudio Lisia, Kwa Mtawala, Mtukufu Feliksi: Salamu. Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi wakakaribia kumuua, lakini nikaja na vikosi vyangu vya askari nikamwokoa, kwa kuwa nilipata habari kwamba yeye ni raiya wa Rumi. Nilitaka kujua kwa nini walikuwa wanamshutumu, hivyo nikamleta mbele ya baraza lao. Ndipo nikaona kuwa alikuwa anashutumiwa kwa mambo yanayohusu sheria yao, lakini hakuwa ameshtakiwa kwa jambo lolote linalostahili kifo au kifungo. Nilipoarifiwa kuwa kulikuwa na shauri baya dhidi ya mtu huyu, nilimtuma kwako mara moja. Niliwaagiza washtaki wake pia waeleze mashtaka yao dhidi yake mbele yako. Hivyo askari, kwa kufuata maelekezo waliyopewa, wakamchukua Paulo wakati wa usiku na kumleta mpaka Antipatri. Kesho yake wakawaacha wale wapanda farasi waendelee na safari wakiwa na Paulo, wao wakarudi kwenye ngome ya askari. Askari walipofika Kaisaria, walimpa mtawala ile barua, na kumkabidhi Paulo kwake. Mtawala alipokwisha kuisoma ile barua alimuuliza Paulo alikuwa mtu wa jimbo gani. Alipojua kuwa anatoka Kilikia, alisema, “Nitasikiliza shauri lako washtaki wako watakapofika hapa.” Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi kwenye jumba la kifalme la Herode.