Matendo 20:7-12
Matendo 20:7-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane. Palikuwa na taa nyingi katika orofa ile tulipokuwa tumekusanyika. Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka orofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa. Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema, Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake. Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hata alfajiri, ndipo akaenda zake. Wakamleta yule kijana, yu mzima, wakafarijika faraja kubwa sana.
Matendo 20:7-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Jumamosi jioni tulikutana ili kumega mkate. Kwa vile Paulo alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliwahutubia watu na kuendelea kuongea nao hadi usiku wa manane. Katika chumba tulimokuwa, ghorofani, kulikuwa na taa nyingi zinawaka. Kijana mmoja aitwaye Eutuko alikuwa ameketi dirishani wakati Paulo alipokuwa anaendelea kuhutubu. Eutuko alianza kusinzia kidogokidogo na hatimaye usingizi ukambana, akaanguka chini kutoka ghorofa ya tatu. Wakamwokota amekwisha kufa. Lakini Paulo alishuka chini, akainama, akamkumbatia na kusema, “Msiwe na wasiwasi maana kuna uhai bado ndani yake.” Kisha akapanda tena ghorofani, akamega mkate, akala. Aliendelea kuhubiri kwa muda mrefu hadi alfajiri, halafu akaondoka. Wale watu walimchukua yule kijana hadi nyumbani akiwa mzima kabisa, wakapata kitulizo kikubwa.
Matendo 20:7-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubia, maana aliazimia kusafiri siku iliyofuata, naye akafululiza maneno yake hadi usiku wa manane. Palikuwa na taa nyingi katika ghorofa lile tulipokuwa tumekusanyika. Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka ghorofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa. Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema, Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake. Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hadi alfajiri, ndipo akaenda zake. Wakamleta yule kijana, akiwa mzima, wakafarijika faraja kubwa sana.
Matendo 20:7-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku ya kwanza ya juma tulikutana pamoja kwa ajili ya kumega mkate. Paulo akaongea na watu, naye kwa kuwa alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliendelea kuongea mpaka usiku wa manane. Kwenye chumba cha ghorofani walimokuwa wamekutania kulikuwa na taa nyingi. Kijana mmoja jina lake Eutiko, alikuwa amekaa dirishani, wakati Paulo alipokuwa akihubiri kwa muda mrefu, alipatwa na usingizi mzito, akaanguka kutoka ghorofa ya tatu, wakamwinua akiwa amekufa. Paulo akashuka chini, akajitupa juu yake na kumkumbatia, akasema, “Msishtuke, uzima wake bado umo ndani yake.” Kisha Paulo akapanda tena ghorofani, akamega mkate na kula. Baada ya kuongea mpaka mapambazuko, akaondoka. Watu wakamrudisha yule kijana nyumbani akiwa hai nao wakafarijika sana.