Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 2:1-18

Matendo 2:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku ya Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika mahali pamoja. Ghafla, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikaijaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa. Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha. Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi duniani. Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Walistaajabu na kushangaa wakisema, “Je, hawa wote tunaowasikia wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya? Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe? Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelamu; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia, Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libia karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni kutoka Roma, Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu.” Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, “Hii ina maana gani?” Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, “Watu hawa wamelewa divai mpya!” Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: “Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu. Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi? Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli: ‘Katika siku zile za mwisho, asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu wa kiume na wa kike watatoa unabii, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. Naam, hata watumishi wangu wa kiume na kike, nitawamiminia Roho wangu siku zile, nao watatoa unabii.

Shirikisha
Soma Matendo 2

Matendo 2:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wakati ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafla toka mbinguni sauti kama mvumo wa upepo mkali ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Yudea na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu. Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya? Wengine walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya. Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Yudea, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu. Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana; lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri.

Shirikisha
Soma Matendo 2

Matendo 2:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu. Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya? Wengine walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya. Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu. Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana; lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri.

Shirikisha
Soma Matendo 2

Matendo 2:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Siku ya Pentekoste ilipowadia, waamini wote walikuwa mahali pamoja. Ghafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo mkali uliotoka mbinguni ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia. Basi walikuwepo Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu. Waliposikia sauti hii, umati wa watu ulikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakiwa wameshangaa na kustaajabu wakauliza, “Je, hawa wote wanaozungumza si Wagalilaya? Imekuwaje basi kila mmoja wetu anawasikia wakinena kwa lugha yake ya kuzaliwa? Wapathi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia, Pamfilia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene na wageni kutoka Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu, sote tunawasikia watu hawa wakisema mambo makuu ya ajabu ya Mungu katika lugha zetu wenyewe.” Wakiwa wameshangaa na kufadhaika wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?” Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa divai!” Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na mmoja, akainua sauti yake na kuhutubia ule umati wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, jueni jambo hili mkanisikilize. Hakika watu hawa hawakulewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi! La, hili ni jambo lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema: “ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu, nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu na binti zenu watatabiri, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho wangu, nao watatabiri.

Shirikisha
Soma Matendo 2