Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 19:21-41

Matendo 19:21-41 Biblia Habari Njema (BHN)

Baada ya mambo hayo, Paulo aliamua kwenda Yerusalemu kwa kupitia Makedonia na Akaya. Alisema, “Baada ya kufika huko, itanilazimu kuona Roma pia.” Hivyo, aliwatuma wawili wa wasaidizi wake, Timotheo na Erasto, wamtangulie kwenda Makedonia, naye akabaki kwa muda huko Asia. Wakati huo ndipo kulipotokea ghasia kubwa huko Efeso kwa sababu ya hiyo njia ya Bwana. Kulikuwa na mfua fedha mmoja aitwaye Demetrio, ambaye alikuwa na kazi ya kutengeneza sanamu za nyumba ya mungu wa kike aitwaye Artemi. Shughuli hiyo iliwapatia mafundi wake faida kubwa. Demetrio aliwakusanya hao wafanyakazi pamoja na wengine waliokuwa na kazi kama hiyo, akawaambia, “Wananchi, mnafahamu kwamba kipato chetu kinatokana na biashara hii. Sasa, mnaweza kusikia na kujionea wenyewe mambo Paulo anayofanya, si hapa Efeso tu, ila pia kote katika Asia. Yeye amewashawishi na kuwageuza watu wakakubali kwamba miungu ile iliyotengenezwa na watu si miungu hata kidogo. Hivyo iko hatari kwamba biashara yetu itakuwa na jina baya. Si hivyo tu, bali pia jambo hilo linaweza kuifanya nyumba ya mungu Artemi kuwa si kitu cha maana. Hatimaye sifa zake huyo ambaye Asia na dunia yote inamwabudu, zitakwisha.” Waliposikia hayo, waliwaka hasira, wakaanza kupiga kelele: “Mkuu ni Artemi wa Efeso!” Mji wote ukajaa ghasia. Wakawavamia Gayo na Aristarko, wenyeji wa Makedonia, ambao walikuwa wasafiri wenzake Paulo, wakakimbia nao mpaka kwenye ukumbi wa michezo. Paulo mwenyewe alitaka kuukabili huo umati wa watu, lakini wale waumini walimzuia. Maofisa wengine wa huo mkoa wa Asia, waliokuwa rafiki zake, walimpelekea Paulo ujumbe wakimsihi asijihatarishe kwa kwenda kwenye ukumbi wa michezo. Wakati huo, kila mtu alikuwa anapayuka; wengine hili na wengine lile, mpaka hata ule mkutano ukavurugika. Wengi hawakujua hata sababu ya kukutana kwao. Kwa vile Wayahudi walimfanya Aleksanda ajitokeze mbele, baadhi ya watu katika ule umati walidhani kuwa ndiye. Basi, Aleksanda aliwaashiria watu kwa mkono akitaka kujitetea mbele ya ule umati wa watu. Lakini walipotambua kuwa yeye ni Myahudi, wote kwa sauti moja walipiga kelele: “Mkuu ni Artemi wa Efeso!” Wakaendelea kupayukapayuka hivyo kwa muda wa saa mbili. Hatimaye karani wa mji alifaulu kuwanyamazisha, akawaambia, “Wananchi wa Efeso, kila mtu anajua kwamba mji huu wa Efeso ni mlinzi wa nyumba ya mungu Artemi na mlinzi wa ile sanamu iliyoanguka kutoka mbinguni. Hakuna anayeweza kukana mambo hayo. Hivyo basi, tulieni; msifanye chochote bila hadhari. Mmewaita watu hawa hapa ingawaje hawakuikufuru nyumba ya mungu wala kumtukana mungu wetu wa kike. Kama, basi Demetrio na wafanyakazi wake wana mashtaka yao kuhusu watu hawa, yapo mahakama na wakuu wa mikoa; wanaweza kushtakiana huko. Kama mna matatizo mengine, yapelekeni katika kikao halali. Kwa maana tungaliweza kushtakiwa kwa kusababisha ghasia kutokana na vituko vya leo. Ghasia hii haina msingi halali na hatungeweza kutoa sababu za kuridhisha za ghasia hiyo.” Baada ya kusema hayo, aliuvunja mkutano.

Shirikisha
Soma Matendo 19

Matendo 19:21-41 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mambo hayo yalipokwisha kumalizika, Paulo akaazimu rohoni mwake, akiisha kupita katika Makedonia na Akaya, aende Yerusalemu, akisema, Baada ya kuwako huko, yanipasa kuuona na Rumi pia. Akatuma watu wawili miongoni mwa wale waliomtumikia kwenda Makedonia, nao ni Timotheo na Erasto, yeye mwenyewe akakaa katika Asia kwa muda. Wakati huo kukatokea ghasia si haba kuhusu Njia ile. Kwa maana mtu mmoja, jina lake Demetrio, mfua fedha, aliyekuwa akifanya vihekalu vya fedha vya Artemi, alikuwa akiwapatia mafundi faida nyingi. Akawakusanya hao, pamoja na wengine wenye kazi ile ile, akasema, Enyi wanaume, mnajua ya kuwa utajiri wetu hutoka katika kazi hii. Tena mnaona na kusikia ya kwamba si katika Efeso tu, bali katika Asia yote pia Paulo huyo ameshawishi watu wengi na kuwageuza nia zao, akisema ya kwamba hiyo inayofanywa kwa mikono siyo miungu. Si kwamba kazi hii yetu ina hatari ya kudharauliwa tu; bali na hekalu la mungu mke aliye mkuu, Artemi, kuhesabiwa si kitu, na kuondolewa utukufu wake, ambaye Asia yote pia na walimwengu wote humwabudu. Waliposikia haya wakajaa ghadhabu, wakapiga kelele, wakisema, Artemi wa Waefeso ni mkuu. Mji wote ukajaa ghasia, wakaenda mbio wakaingia ukumbi wa michezo kwa pamoja, wakiisha kuwakamata Gayo na Aristarko, watu wa Makedonia waliosafiri pamoja na Paulo. Na Paulo alipotaka kuingia kati ya watu, wanafunzi hawakumwacha aingie. Na baadhi ya wakuu wa Asia, walio rafiki zake, wakatuma watu kwake, wakimsihi asiingie ndani katika ukumbi wa michezo. Basi wengine walikuwa wakilia hivi na wengine hivi; kwa maana ule mkutano ulikuwa umechafukachafuka, na wengi wao hawakuijua sababu ya kukusanyika kwao pamoja. Wakamtoa Iskanda katika mkutano, Wayahudi wakimweka mbele ya watu. Iskanda akawapungia mkono, akitaka kujitetea mbele ya wale watu. Lakini walipotambua ya kuwa yeye ni Myahudi, wakapiga kelele wote pia kwa sauti moja kwa muda wa kama saa mbili, wakisema, Artemi wa Waefeso ni mkuu. Na karani wa mji alipokwisha kuwatuliza watu, akasema, Enyi wanaume wa Efeso, ni mtu gani asiyejua ya kuwa mji wa Efeso ni mtunzaji wa hekalu la Artemi, aliye mkuu, na wa kitu kile kilichoanguka kutoka mbinguni? Basi kwa kuwa mambo haya hayawezi kukanushwa, imewapasa kutulia; msifanye neno la haraka haraka. Kwa maana mmewaleta watu hawa, wasioiba vitu vya hekalu wala kumtukana mungu mke wetu. Basi ikiwa Demetrio na mafundi walio pamoja naye wana neno juu ya mtu yeyote, baraza ziko, na watawala wako; na washitakiane. Ikiwa kuna mambo mengine yoyote mnayotaka kujua, ni sharti yasuluhishwe katika kusanyiko lililo halali. Kwa maana tuna hatari ya kushitakiwa kwa ajili ya ghasia hizi za leo, ambazo hazina sababu; maana hakuna sababu tunayoweza kutoa kama chanzo cha ghasia hizi. Alipokwisha kusema haya akauvunja mkutano.

Shirikisha
Soma Matendo 19

Matendo 19:21-41 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mambo hayo yalipokwisha kumalizika, Paulo akaazimu rohoni mwake, akiisha kupita katika Makedonia na Akaya, aende Yerusalemu, akisema, Baada ya kuwako huko, yanipasa kuuona na Rumi pia. Akatuma watu wawili miongoni mwa wale waliomtumikia kwenda Makedonia, nao ni Timotheo na Erasto, yeye mwenyewe akakaa katika Asia kitambo. Wakati huo kukatukia ghasia si haba katika habari ya Njia ile. Kwa maana mtu mmoja, jina lake Demetrio, mfua fedha, aliyekuwa akifanya vihekalu vya fedha vya Artemi, alikuwa akiwapatia mafundi faida nyingi. Akawakusanya hao, pamoja na wengine wenye kazi ile ile, akasema, Enyi wanaume, mnajua ya kuwa utajiri wetu hutoka katika kazi hii. Tena mnaona na kusikia ya kwamba si katika Efeso tu, bali katika Asia yote pia Paulo huyo ameshawishi watu wengi na kuwageuza nia zao, akisema ya kwamba hiyo inayofanywa kwa mikono siyo miungu. Si kwamba kazi hii yetu ina hatari ya kudharauliwa tu; bali na hekalu la mungu mke aliye mkuu, Artemi, kuhesabiwa si kitu, na kuondolewa utukufu wake, ambaye Asia yote pia na walimwengu wote humwabudu. Waliposikia haya wakajaa ghadhabu, wakapiga kelele, wakisema, Artemi wa Waefeso ni mkuu. Mji wote ukajaa ghasia, wakaenda mbio wakaingia mahali pa michezo kwa nia moja, wakiisha kuwakamata Gayo na Aristarko, watu wa Makedonia waliosafiri pamoja na Paulo. Na Paulo alipotaka kuingia kati ya watu, wanafunzi hawakumwacha aingie. Na baadhi ya wakuu wa Asia, walio rafiki zake, wakatuma watu kwake, wakimsihi asijihudhurishe nafsi yake ndani ya mahali pa michezo. Basi wengine walikuwa wakilia hivi na wengine hivi; kwa maana ule mkutano ulikuwa umechafuka-chafuka, na wengi wao hawakuijua sababu ya kukusanyika kwao pamoja. Wakamtoa Iskanda katika mkutano, Wayahudi wakimweka mbele ya watu. Iskanda akawapungia mkono, akitaka kujitetea mbele ya wale watu. Lakini walipotambua ya kuwa yeye ni Myahudi, wakapiga kelele wote pia kwa sauti moja kwa muda wa kama saa mbili, wakisema, Artemi wa Waefeso ni mkuu. Na karani wa mji alipokwisha kuwatuliza watu, akasema, Enyi wanaume wa Efeso, ni mtu gani asiyejua ya kuwa mji wa Efeso ni mtunzaji wa hekalu la Artemi, aliye mkuu, na wa kitu kile kilichoanguka kutoka mbinguni? Basi kwa kuwa mambo haya hayawezi kukanushwa, imewapasa kutulia; msifanye neno la haraka haraka. Kwa maana mmewaleta watu hawa, wasioiba vitu vya hekalu wala kumtukana mungu mke wetu. Basi ikiwa Demetrio na mafundi walio pamoja naye wana neno juu ya mtu, baraza ziko, na maliwali wako; na washitakiane. Bali mkitafuta neno lo lote katika mambo mengine, yatatengenezwa katika kusanyiko lililo halali. Kwa maana tuna hatari ya kushitakiwa kwa ajili ya matata haya ya leo, ambayo hayana sababu; na katika neno hilo, hatutaweza kujiudhuru kwa mkutano huu. Alipokwisha kusema haya akauvunja mkutano.

Shirikisha
Soma Matendo 19

Matendo 19:21-41 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya mambo haya kutukia, Paulo akakusudia rohoni kwenda Yerusalemu kupitia Makedonia na Akaya. Akasema, “Baada ya kufika huko, yanipasa pia kwenda Rumi.” Hivyo akatuma wasaidizi wake wawili, Timotheo na Erasto, waende Makedonia, wakati yeye mwenyewe alibaki kwa muda kidogo huko Asia. Wakati huo huo pakatokea dhiki kubwa kwa sababu ya Njia ile ya Bwana. Mtu mmoja jina lake Demetrio mfua fedha aliyekuwa akitengeneza vinyago vya fedha vya Artemi na kuwapatia mafundi wake biashara kubwa, aliwaita pamoja watu wengine waliofanya kazi ya ufundi kama yake na kusema, “Enyi watu, mnajua ya kuwa utajiri wetu unatokana na biashara hii! Pia ninyi mmeona na kusikia jinsi ambavyo si huku Efeso peke yake lakini ni karibu Asia yote, huyu Paulo amewashawishi na kuvuta idadi kubwa ya watu kwa kusema kuwa miungu iliyotengenezwa na watu si miungu. Kwa hiyo kuna hatari si kwa kazi yetu kudharauliwa tu, bali pia hata hekalu la mungu mke Artemi, aliye mkuu, anayeabudiwa Asia yote na ulimwengu wote, litakuwa limepokonywa fahari yake ya kiungu.” Waliposikia maneno haya, wakaghadhibika, wakaanza kupiga kelele, “Artemi wa Waefeso ni mkuu!” Mara mji wote ukajaa ghasia. Wakawakamata Gayo na Aristarko, watu wa Makedonia waliokuwa wakisafiri pamoja na Paulo, na watu wakakimbilia katika ukumbi wa michezo kama mtu mmoja. Paulo akataka kuingia katikati ya umati huo, lakini wanafunzi hawakumruhusu. Hata baadhi ya viongozi wa sehemu ile, waliokuwa rafiki zake Paulo, wakatuma watu wakitamani asiingie katika ule ukumbi. Ule umati ulikuwa na taharuki. Wengine walikuwa wakipiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Idadi kubwa ya watu hawakujua hata ni kwa nini walikuwa wamekusanyika huko. Wayahudi wakamsukumia Aleksanda mbele na baadhi ya watu kwenye ule umati wakampa maelekezo. Akawaashiria kwa mkono ili watulie aweze kujitetea mbele ya watu. Lakini walipotambua kwamba alikuwa Myahudi, wote wakapiga kelele kwa sauti moja kwa karibu muda wa saa mbili, wakisema, “Artemi wa Efeso ni mkuu!” Baadaye karani wa mji akaunyamazisha ule umati wa watu na kusema, “Enyi watu wa Efeso, je, ulimwengu wote haujui ya kuwa mji wa Efeso ndio unaotunza hekalu la Artemi aliye mkuu na ile sanamu yake iliyoanguka kutoka mbinguni? Kwa hiyo, kwa kuwa mambo haya hayakanushiki, inawapasa mnyamaze na wala msifanye lolote kwa haraka. Kwa kuwa mmewaleta hawa watu hapa, ingawa hawajaiba hekaluni wala kumkufuru huyu mungu wetu wa kike. Basi, ikiwa Demetrio na mafundi wenzake wana jambo zito dhidi ya mtu yeyote, mahakama ziko wazi na wasaidizi wa mwakilishi wa mtawala. Wanaweza kufungua mashtaka. Lakini kama kuna jambo jingine lolote zaidi mnalotaka kulileta, itabidi lisuluhishwe katika kusanyiko halali. Kama ilivyo sasa, tuko hatarini kushtakiwa kwa kufanya ghasia kwa sababu ya tukio la leo. Kwa kuwa hakuna sababu tutakayoweza kutoa kuhalalisha msukosuko huu.” Baada ya kusema haya akavunja mkutano.

Shirikisha
Soma Matendo 19

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha