Matendo 19:1-7
Matendo 19:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati Apolo alipokuwa Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso ambako aliwakuta wanafunzi kadhaa. Akauliza, “Je, mlipopata kuwa waumini mlipokea Roho Mtakatifu?” Nao wakamjibu, “La! Hata hatujasikia kwamba kuna Roho Mtakatifu.” Naye akasema, “Sasa mlipata ubatizo wa namna gani?” Wakamjibu, “Ubatizo wa Yohane.” Naye Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohane ulikuwa wa kuonesha kwamba watu wametubu. Yohane aliwaambia watu wamwamini yule ambaye alikuwa anakuja baada yake, yaani Yesu.” Baada ya kusikia hayo, walibatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Basi, Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akawashukia, wakaanza kusema lugha ngeni na kutangaza ujumbe wa Mungu. Wote jumla walikuwa watu wapatao kumi na wawili.
Matendo 19:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadhaa huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri. Na idadi yao ilikuwa kama wanaume kumi na wawili.
Matendo 19:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri. Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili.
Matendo 19:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Apolo alipokuwa huko Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso. Huko akawakuta wanafunzi kadhaa, akawauliza, “Je, mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?” Wakajibu, “Hapana, hata hatukusikia kuwa kuna Roho Mtakatifu.” Ndipo Paulo akawauliza, “Je, mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakajibu, “Kwa ubatizo wa Yohana.” Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohana ulikuwa wa toba, aliwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja baada yake, yaani Yesu.” Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu. Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akawashukia, nao wakanena kwa lugha mpya na kutabiri. Walikuwa wapatao wanaume kumi na wawili.