Matendo 18:23-28
Matendo 18:23-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya kukaa huko kwa siku kadhaa akaondoka, akapita kati ya nchi ya Galatia na Frigia, mji kwa mji, akiwatia moyo wanafunzi. Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzaliwa wa Aleksandria, msemaji mzuri, akafika Efeso; naye alikuwa na ujuzi wa Maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa bidii habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Priskila na Akila walipomsikia wakampeleka kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi. Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionesha kwa maneno ya Maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.
Matendo 18:23-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata akiisha kukaa huko siku kadha wa kadha akaondoka, akapita kati ya nchi ya Galatia na Frigia, mji kwa mji, akiwathibitisha wanafunzi. Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi. Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.
Matendo 18:23-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya kukaa huko kwa muda, akaondoka na kwenda sehemu moja hadi nyingine huko Galatia na Frigia, akiwaimarisha wanafunzi wote. Basi akaja Efeso Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mwenyeji wa Iskanderia. Yeye alikuwa na elimu kubwa, pia alikuwa hodari katika Maandiko. Alikuwa amefundishwa katika njia ya Bwana, naye alikuwa na bidii katika roho, akafundisha kwa usahihi juu ya Yesu, ingawa alijua tu ubatizo wa Yohana. Apolo alianza kunena kwa ujasiri mkubwa katika sinagogi. Lakini Prisila na Akila walipomsikia, walimchukua kando na kumweleza njia ya Mungu kwa ufasaha zaidi. Naye Apolo alipotaka kwenda Akaya, ndugu wa Efeso walimtia moyo, wakawaandikia wanafunzi huko ili wamkaribishe. Alipofika huko, aliwasaidia sana wale ambao, kwa neema ya Mungu, walikuwa wameamini. Kwa uwezo mkubwa aliwakanusha hadharani Wayahudi waliokuwa wakipinga, akionyesha kwa njia ya Maandiko kwamba Yesu ndiye Kristo.
Matendo 18:23-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Alikaa huko muda mfupi, halafu akaendelea na safari kwa kupitia sehemu za Galatia na Frugia akiwatia moyo wafuasi wote. Myahudi mmoja aitwaye Apolo, mzaliwa wa Aleksandria, alifika Efeso. Alikuwa mtu mwenye ufasaha wa kuongea na mwenye ujuzi mkubwa wa Maandiko Matakatifu. Alikuwa amefundishwa juu ya hiyo njia ya Bwana, na akiwa motomoto, aliongea juu ya habari za Yesu akafundisha kwa usahihi ingawa alikuwa amepata ubatizo wa Yohane tu. Priskila na Akula walipomsikia akiongea kwa uhodari ndani ya sunagogi, walimchukua kwao wakamfundisha hiyo njia ya Mungu kwa usahihi zaidi. Apolo alipoamua kwenda Akaya, wale ndugu walimtia moyo kwa kuwaandikia wafuasi kule Akaya wampokee. Alipofika huko, aliweza kwa msaada wa neema ya Mungu, kuwasaidia sana wale ndugu waliopata kuwa waumini; kwa maana aliendelea kwa uhodari kuwashinda Wayahudi hadharani akithibitisha kwa Maandiko Matakatifu kuwa Yesu ni Kristo.