Matendo 18:1-17
Matendo 18:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya hayo, Paulo aliondoka Athene, akaenda Korintho. Huko Korintho, alimkuta Myahudi mmoja aitwaye Akula, mzaliwa wa Ponto. Akula pamoja na mkewe aitwaye Priskila, walikuwa wamerudi kutoka Italia siku hizohizo kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Roma. Paulo alikwenda kuwaona, na kwa vile wao walikuwa mafundi wa kushona mahema kama yeye, Paulo alikaa nao akafanya kazi. Kila Sabato alifanya majadiliano katika sunagogi akijaribu kuwavuta Wayahudi na Wagiriki. Baada ya Sila na Timotheo kuwasili kutoka Makedonia, Paulo alianza kutumia wakati wake wote kwa ajili ya kuhubiri, akawathibitishia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo. Walipompinga na kuanza kumtukana, aliyakunguta mavazi yake mbele yao akisema, “Mkipotea ni shauri lenu wenyewe; mimi sina lawama yoyote juu ya jambo hilo. Na tangu sasa nitawaendea watu na mataifa mengine.” Basi, akatoka hapo akaenda kukaa nyumbani kwa mtu mmoja mcha Mungu aitwaye Tito Yusto, ambaye nyumba yake ilikuwa karibu na lile sunagogi. Krispo, mkuu wa hilo sunagogi, alimwamini Bwana yeye pamoja na jamaa yake yote. Wakorintho wengi waliusikiliza ujumbe huo, wakaamini na kubatizwa. Siku moja usiku, Bwana alimwambia Paulo katika maono: “Usiogope, endelea kuhubiri tu bila kufa moyo, maana mimi niko pamoja nawe. Hakuna mtu atakayejaribu kukudhuru maana hapa mjini pana watu wengi walio upande wangu.” Basi, Paulo alikaa huko akifundisha neno la Mungu kati yao kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. Lakini wakati Galio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Akaya, Wayahudi walimvamia Paulo kwa pamoja na kumpeleka mahakamani. Wakasema, “Tunamshtaki mtu huyu kwa sababu ya kuwashawishi watu wamwabudu Mungu kwa namna inayopingana na sheria.” Kabla tu Paulo hajaanza kusema, Galio aliwaambia Wayahudi, “Sikilizeni enyi Wayahudi! Kama kweli jambo hili lingekuwa juu ya uhalifu au uovu ningekuwa tayari kuwasikilizeni. Lakini kama ni shauri la ubishi kuhusu maneno na majina na sheria yenu, amueni nyinyi wenyewe. Mimi sitaki kuwa hakimu wa mambo hayo!” Basi, akawafukuza kutoka mahakamani. Nao wote wakamkamata Sosthene ambaye alikuwa kiongozi wa sunagogi, wakampiga palepale mbele ya mahakama. Lakini Galio hakujali kitendo hicho hata kidogo.
Matendo 18:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho. Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akila, mzalia wa Ponto; naye amekuja kutoka nchi ya Italia siku za karibu, pamoja na Priskila mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi, naye akafika kwao; na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema. Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wagiriki. Hata Sila na Timotheo walipoteremka kutoka Makedonia, Paulo akasongwa sana na lile neno, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo. Walipopingana naye na kumtukana Mungu, akakung'uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa. Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi. Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa. Bwana akamwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze, kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji huu. Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno la Mungu. Hata Galio alipokuwa mtawala wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, wakisema Mtu huyu huwashawishi watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sheria. Na Paulo alipotaka kufunua kinywa chake, Galio akawaambia Wayahudi, Kama lingekuwa jambo la dhuluma au la hila mbaya, enyi Wayahudi, ingekuwa haki mimi kuchukuliana nanyi; bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo. Akawafukuza waondoke mbele ya kiti cha hukumu. Nao wote wakamshika Sosthene, mkuu wa sinagogi, wakampiga mbele ya kiti cha hukumu. Wala Galio hakuyaona mambo hayo kuwa ni kitu.
Matendo 18:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baada ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho. Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akila, mzalia wa Ponto; naye amekuja kutoka nchi ya Italia siku za karibu, pamoja na Prisila mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi, naye akafikilia kwao; na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema. Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani. Hata Sila na Timotheo walipotelemka kutoka Makedonia, Paulo akasongwa sana na lile neno, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo. Walipopingamana naye na kumtukana Mungu, akakung’uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa. Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi. Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa. Bwana akamwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze, kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji huu. Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno la Mungu. Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, wakisema Mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sheria. Na Paulo alipotaka kufunua kinywa chake, Galio akawaambia Wayahudi, Kama lingekuwa jambo la dhuluma au la hila mbaya, enyi Wayahudi, ingekuwa haki mimi kuchukuliana nanyi; bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo. Akawafukuza waondoke mbele ya kiti cha hukumu. Nao wote wakamshika Sosthene, mkuu wa sinagogi, wakampiga mbele ya kiti cha hukumu. Wala Galio hakuyaona mambo hayo kuwa ni kitu.
Matendo 18:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya haya, Paulo akaondoka Athene akaenda Korintho. Huko akakutana na Myahudi mmoja jina lake Akila, mwenyeji wa Ponto, ambaye alikuwa amewasili karibuni kutoka Italia pamoja na mkewe Prisila, kwa sababu Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo akaenda kuwaona, naye kwa kuwa alikuwa mtengeneza mahema kama wao, akakaa na kufanya kazi pamoja nao. Kila Sabato Paulo alikuwa akihojiana nao katika sinagogi, akijitahidi kuwashawishi Wayahudi na Wayunani. Sila na Timotheo walipowasili kutoka Makedonia, walimkuta Paulo akiwa amejitolea muda wake wote katika kuhubiri, akiwashuhudia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo Wayahudi walipompinga Paulo na kukufuru, yeye aliyakungʼuta mavazi yake, akawaambia, “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu! Mimi sina hatia, nimetimiza wajibu wangu. Kuanzia sasa nitawaendea watu wa Mataifa.” Kisha akaondoka mle kwenye sinagogi, akaenda nyumbani kwa mtu mmoja jina lake Tito Yusto, aliyekuwa mcha Mungu. Nyumba yake ilikuwa karibu na sinagogi. Kiongozi wa hilo sinagogi, aliyeitwa Krispo, akamwamini Bwana, yeye pamoja na watu wote wa nyumbani mwake. Nao Wakorintho wengi waliomsikia Paulo pia wakaamini na kubatizwa. Usiku mmoja Bwana akamwambia Paulo katika maono, “Usiogope, lakini endelea kusema wala usinyamaze, kwa maana mimi niko pamoja nawe, wala hakuna mtu atakayeweza kukushambulia ili kukudhuru, kwa kuwa ninao watu wengi katika mji huu ambao ni watu wangu.” Hivyo Paulo akakaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, akiwafundisha neno la Mungu. Lakini wakati Galio alipokuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala huko Akaya, Wayahudi waliungana kumshambulia Paulo, wakamkamata na kumpeleka mahakamani. Wakamshtaki wakisema, “Mtu huyu anawashawishi watu wamwabudu Mungu kinyume cha sheria.” Paulo alipotaka kujitetea, Galio akawaambia Wayahudi, “Kama ninyi Wayahudi mlikuwa mkilalamika kuhusu makosa makubwa ya uhalifu ingekuwa haki kwangu kuwasikiliza. Lakini kwa kuwa linahusu maneno, majina na sheria yenu, amueni ninyi wenyewe. Mimi sitakuwa mwamuzi wa mambo haya.” Akawafukuza kutoka mahakamani. Ndipo wote wakamkamata Sosthene kiongozi wa sinagogi, wakampiga mbele ya mahakama, lakini Galio hakujali kitendo chao hata kidogo.