Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 17:1-34

Matendo 17:1-34 Biblia Habari Njema (BHN)

Kwa kupitia Amfipoli na Apolonia, walisafiri mpaka Thesalonike ambako kulikuwa na sunagogi la Wayahudi. Paulo alijiunga nao kama ilivyokuwa desturi yake, akajadiliana nao Sabato tatu mfululizo, akitumia Maandiko Matakatifu. Aliyaeleza na kuonesha kwamba ilimbidi Kristo kuteswa na kufufuka kutoka kwa wafu. Akawaambia, “Yesu ambaye mimi namhubiri kwenu ndiye Kristo.” Baadhi yao walikubali wakajiunga na Paulo na Sila. Kadhalika, idadi kubwa ya Wagiriki waliomcha Mungu pamoja na wanawake wengi wa tabaka la juu, walijiunga nao. Lakini Wayahudi wakaona wivu; wakawakodi wafidhuli sokoni, wakafanya kikundi na kuzusha fujo mjini kote. Wakaivamia nyumba ya Yasoni wakitumaini kuwapata humo Paulo na Sila ili wawalete hadharani. Lakini hawakuwapata na hivyo walimburuta Yasoni pamoja na ndugu wengine mpaka kwa wakuu wa mji, wakapiga kelele: “Watu hawa wamekuwa wakivuruga dunia yote na sasa wako hapa mjini. Yasoni amewakaribisha nyumbani kwake. Wote wanafanya kinyume cha amri ya Kaisari wakisema eti: ‘Kuna mfalme mwingine aitwaye Yesu.’” Kwa maneno hayo waliwatia wasiwasi wakuu wa mji na kundi la watu. Wakawafanya Yasoni na wenzake watoe dhamana, kisha wakawaacha waende zao. Usiku, wale ndugu waliwahimiza Paulo na Sila waende Berea. Mara tu walipofika huko, walikwenda katika sunagogi la Wayahudi. Watu wa huko walikuwa wasikivu zaidi kuliko wale wa Thesalonike. Waliupokea ule ujumbe kwa hamu kubwa, wakawa wanayachunguza Maandiko Matakatifu kila siku, ili kuona kama yale waliyosema Paulo na Sila yalikuwa kweli. Wengi wao waliamini na pia wanawake wa Kigiriki wa tabaka la juu na wanaume pia. Lakini, Wayahudi wa Thesalonike walipogundua kwamba Paulo alikuwa anahubiri neno la Mungu huko Berea, walikwenda huko, wakaanza kufanya fujo na kuchochea makundi ya watu. Wale ndugu wakamsindikiza haraka aende pwani lakini Sila na Timotheo walibaki Berea. Wale ndugu waliomsindikiza Paulo walikwenda pamoja naye mpaka Athene. Kisha, wakarudi pamoja na maagizo kutoka kwa Paulo kwamba Sila na Timotheo wamfuate upesi iwezekanavyo. Paulo alipokuwa anawasubiri Sila na Timotheo huko Athene, moyo wake ulighadhibika sana alipoona jinsi mji huo ulivyokuwa umejaa sanamu za miungu. Alijadiliana na Wayahudi na watu wengine waliomcha Mungu katika sunagogi; na kila siku alikuwa na majadiliano mahali pa hadhara pamoja na wote wale waliojitokeza. Wengine waliofuata falsafa ya Epikuro na Stoiki walibishana naye. Wengine walisema, “Anataka kusema nini huyu bwanamaneno?” Kwa kuwa Paulo alikuwa anahubiri juu ya Yesu na juu ya ufufuo, wengine walisema, “Inaonekana kama anahubiri juu ya miungu ya kigeni.” Hivyo walimchukua Paulo, wakampeleka Areopago, wakasema, “Tunataka kujua jambo hili jipya ulilokuwa unazungumzia. Vitu vingine tulivyosikia kwa masikio yetu vinaonekana kuwa viroja kwetu. Tungependa kujua mambo haya yana maana gani.” Wananchi wa Athene na wakazi wengine wa huko walikuwa wanatumia wakati wao wote kuhadithiana na kusikiliza habari mpyampya. Basi, Paulo alisimama mbele ya baraza la Areopago, akasema, “Wananchi wa Athene! Ninaona kwamba nyinyi, kwa vyovyote, ni watu wa dini sana, maana nilipokuwa napita huko na huko nikiangalia sanamu zenu za ibada niliona madhabahu moja ambayo imeandikwa: ‘Kwa Mungu asiyejulikana.’ Basi, huyo mnayemwabudu bila kujua, ndiye ninayemhubiri kwenu. Mungu, aliyeumba ulimwengu na vyote vilivyomo, ni Bwana wa mbingu na dunia; yeye hakai katika hekalu zilizojengwa na watu. Wala hatumikiwi kwa mikono ya watu kana kwamba anahitaji chochote kile, kwa maana yeye mwenyewe ndiye anayewapa watu uhai, anawawezesha kupumua na kuwapa kila kitu. Kutokana na mtu mmoja aliumba mataifa yote na kuyawezesha kuishi duniani kote. Aliamua na kupanga kabla kabisa lini na wapi mataifa hayo yangeishi. Alifanya hivyo, ili mataifa hayo yapate kumfuata, na kama vile kwa kupapasapapasa, yapate kumfikia. Hata hivyo lakini, Mungu hayuko mbali na kila mmoja wetu. Kama alivyosema mtu mmoja: ‘Ndani yake yeye sisi tunaishi, tunajimudu, na tuko!’ Ni kama washairi wenu wengine walivyosema: ‘Sisi ni watoto wake.’ Ikiwa basi, sisi ni watoto wa Mungu, haifai kumfikiria Mungu kuwa kama dhahabu, fedha au hata jiwe lililochongwa na kutiwa nakshi na binadamu. Mungu alifanya kana kwamba haoni nyakati zile watu walipokuwa wajinga. Lakini sasa, anaamuru watu wote kila mahali watubu. Kwa maana amekwisha weka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki kwa njia ya mtu mmoja aliyemteua. Mungu amewathibitishia wote jambo hili kwa kumfufua mtu huyo kutoka kwa wafu!” Walipomsikia Paulo anasema juu ya jambo la kufufuka kwa wafu, wengine wao waliangua kicheko; lakini wengine walisema, “Tunataka kukusikia tena juu ya jambo hili!” Hivyo, Paulo aliwaacha, akatoka barazani. Lakini watu kadhaa waliandamana naye, wakawa waumini. Miongoni mwao walikuwa Dionisio wa Areopago, na mwanamke mmoja aitwaye Damari na wengineo.

Shirikisha
Soma Matendo 17

Matendo 17:1-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wakiisha kupita kati ya Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambapo palikuwa na sinagogi la Wayahudi. Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimokuwa, akahojiana nao kwa maneno ya Maandiko sabato tatu, akiyafunua na kuwaeleza ya kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu; na ya kwamba, Yesu huyu ninayewaambia ninyi habari zake ndiye Kristo. Wengine miongoni mwao wakaamini, wakafuatana na Paulo na Sila; na Wagiriki waliomcha Mungu, wengi sana, na wanawake wenye cheo si wachache. Na Wayahudi wakaona wivu, wakajitwalia watu kadhaa miongoni mwa watu ovyo wasio na sifa njema, nao wakakutanisha mkutano, wakafanya ghasia mjini, wakawaendea watu wa nyumba ya Yasoni, wakataka kuwapeleka mbele ya watu wa mji; na walipowakosa, wakamkokota Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele, wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako, na Yasoni amewakaribisha; na hawa wote wanatenda mambo yaliyo kinyume cha amri za Kaisari, wakisema na kusema yupo mfalme mwingine, aitwaye Yesu. Wakafadhaisha ule mkutano na wakubwa wa mji walipoyasikia hayo. Nao walipokwisha kumtoza dhamana Yasoni na wenziwe wakawaacha waende zao. Mara hao ndugu wakawatuma Paulo na Sila usiku hadi Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi. Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa hamu kuu, wakayachunguza Maandiko kila siku, ili waone kama mambo hayo ndivyo yalivyo. Basi watu wengi miongoni mwao wakaamini, wakiwemo wanawake wa Kigiriki wenye cheo na wanaume. Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipopata habari ya kwamba neno la Mungu linahubiriwa na Paulo hata katika Beroya, wakaenda huko nako wakawavuruga na kuwafadhaisha makutano. Mara hiyo wale ndugu wakamtuma Paulo aende zake mpaka pwani; bali Sila na Timotheo wakabakia huko. Lakini wale waliomsindikiza Paulo wakampeleka mpaka Athene; nao wakiisha kupokea maagizo kuwapelekea Sila na Timotheo, ya kwamba wasikawie kumfuata, wakaenda zao. Paulo alipokuwa akiwangojea huko Athene na kuona jinsi mji ule ulivyojaa sanamu, roho yake ilichukizwa sana ndani yake. Basi katika sinagogi akahojiana na Wayahudi na waliomcha Mungu, na wale waliokutana naye sokoni kila siku. Na baadhi ya Waepikureo na Wastoiko, wenye ujuzi, wakakutana naye. Wengine wakasema, Mpuzi huyu anataka kusema nini? Wengine walisema, Anaonekana kuwa mtangaza habari za miungu migeni, kwa maana alikuwa akihubiri habari za Yesu na ufufuo. Wakamshika, wakampeleka Areopago, wakisema, Je! Twaweza kujua maana ya elimu hii mpya unayoinena? Kwa maana unaleta mambo mageni masikioni mwetu, tutapenda kujua, basi, maana ya mambo haya. Kwa maana Waathene na wageni waliokaa huko walikuwa hawana nafasi kwa jambo linginelo isipokuwa kuelezea au kusikiliza habari za jambo jipya. Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema, Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini. Kwa sababu nilipokuwa nikipita huku na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, niliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua. Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu chochote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasapapasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazawa wake. Basi, kwa kuwa sisi tu wazawa wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu. Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu. Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu. Basi waliposikia habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine wakasema, Tutakusikiliza tena kuhusu habari hiyo. Basi hivi Paulo akaondoka akawaacha. Baadhi ya watu wakaungana naye, wakaamini; katika hao alikuwamo Dionisio, Mwareopago, na mwanamke mmoja jina lake Damari, na watu wengine pamoja na hao.

Shirikisha
Soma Matendo 17

Matendo 17:1-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Wakiisha kupita kati ya Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambapo palikuwa na sinagogi la Wayahudi. Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu, akiyafunua na kuwaeleza ya kwamba ilimpasa Kristo kuteswa, na kufufuka katika wafu; na ya kwamba, Yesu huyu ninayewapasha ninyi habari zake ndiye Kristo. Wengine miongoni mwao wakaamini, wakashikamana na Paulo na Sila; na Wayunani waliomcha Mungu, wengi sana, na wanawake wenye cheo si wachache. Na Wayahudi wakaona wivu, wakajitwalia watu kadha wa kadha katika watu ovyo wasio na sifa njema, nao wakakutanisha mkutano, wakafanya ghasia mjini, wakawaendea watu wa nyumba ya Yasoni, wakataka kuwapeleka mbele ya watu wa mji; na walipowakosa, wakamkokota Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele, wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako, na Yasoni amewakaribisha; na hawa wote wanatenda mambo yaliyo kinyume cha amri za Kaisari, wakisema na kwamba yupo mfalme mwingine, aitwaye Yesu. Wakafadhaisha ule mkutano na wakubwa wa mji walipoyasikia hayo. Nao walipokwisha kumtoza dhamana Yasoni na wenziwe wakawaacha waende zao. Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi. Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo. Basi watu wengi miongoni mwao wakaamini, na wanawake wa Kiyunani wenye cheo, na wanaume si wachache. Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipopata habari ya kwamba neno la Mungu linahubiriwa na Paulo hata katika Beroya, wakaenda huko nako wakawachafua na kuwafadhaisha makutano. Mara hiyo wale ndugu wakampeleka Paulo aende zake mpaka pwani; bali Sila na Timotheo wakasalia huko. Lakini wale waliomsindikiza Paulo wakampeleka mpaka Athene; nao wakiisha kupokea maagizo kuwapelekea Sila na Timotheo, ya kwamba wasikawie kumfuata, wakaenda zao. Paulo alipokuwa akiwangojea huko Athene na kuona jinsi mji ule ulivyojaa sanamu, roho yake ilichukizwa sana ndani yake. Basi katika sinagogi akahojiana na Wayahudi na waliomcha Mungu, na wale waliokutana naye sokoni kila siku. Na baadhi ya Waepikureo na Wastoiko, wenye ujuzi, wakakutana naye. Wengine wakasema, Mpuzi huyu anataka kusema nini? Wengine walisema, Anaonekana kuwa mtangaza habari za miungu migeni, kwa maana alikuwa akihubiri habari za Yesu na ufufuo. Wakamshika, wakamchukua Areopago, wakisema, Je! Twaweza kujua maana ya elimu hii mpya unayoinena? Kwa maana unaleta mambo mageni masikioni mwetu, tutapenda kujua, basi, maana ya mambo haya. Kwa maana Waathene na wageni waliokaa huko walikuwa hawana nafasi kwa neno lo lote ila kutoa habari na kusikiliza habari za jambo jipya. Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema, Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini. Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua. Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wenu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake. Basi, kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu. Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu. Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu. Basi waliposikia habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine wakasema, Tutakusikiliza tena katika habari hiyo. Basi hivi Paulo akaondoka akawaacha. Baadhi ya watu wakashikamana naye, wakaamini; katika hao alikuwamo Dionisio, Mwareopago, na mwanamke mmoja jina lake Damari, na watu wengine pamoja na hao.

Shirikisha
Soma Matendo 17

Matendo 17:1-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wakasafiri kupitia Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambako kulikuwa na sinagogi la Wayahudi. Kama desturi yake, Paulo aliingia ndani ya sinagogi, na kwa muda wa Sabato tatu akawa anahojiana nao kutoka kwenye Maandiko, akidhihirisha wazi na kuthibitisha kwamba ilikuwa lazima Kristo ateswe na afufuke kutoka kwa wafu. Akasema, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake, ndiye Kristo.” Baadhi ya Wayahudi wakasadiki, wakaungana na Paulo na Sila, wakiwepo idadi kubwa ya Wayunani waliomcha Mungu na wanawake wengi mashuhuri. Lakini Wayahudi ambao hawakuwa wameamini wakawa na wivu, wakawakodi watu waovu kutoka sokoni, wakakutanisha umati wa watu, wakaanzisha ghasia mjini. Wakaenda mbio nyumbani kwa Yasoni wakiwatafuta Paulo na Sila ili kuwaleta nje penye ule umati wa watu. Lakini walipowakosa wakamburuta Yasoni na ndugu wengine mbele ya maafisa wa mji, wakipiga kelele: “Watu hawa ni wale walioupindua ulimwengu wamekuja huku, naye Yasoni amewakaribisha nyumbani mwake. Hawa wote wanaasi amri za Kaisari wakisema yuko mfalme mwingine aitwaye Yesu.” Waliposikia haya, ule umati wa watu na maafisa wa mji wakaongeza ghasia. Nao baada ya kuchukua dhamana kwa ajili ya Yasoni na wenzake wakawaacha waende zao. Usiku ule ule, wale ndugu walioamini wakawapeleka Paulo na Sila waende zao Beroya. Walipowasili huko wakaenda kwenye sinagogi la Wayahudi. Hawa Waberoya walikuwa waungwana zaidi kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa waliupokea ule ujumbe kwa shauku kubwa na kuyachunguza Maandiko kila siku ili kuona kama yale Paulo aliyosema yalikuwa kweli. Wayahudi wengi wakaamini pamoja na wanawake na wanaume wa Kiyunani wa tabaka la juu. Lakini wale Wayahudi wa Thesalonike waliposikia kuwa Paulo anahubiri neno la Mungu huko Beroya, wakaenda huko ili kuwashawishi watu na kuwachochea. Mara hiyo, wale ndugu wakamsafirisha Paulo hadi pwani, lakini Sila na Timotheo wakabaki Beroya. Wale waliomsindikiza Paulo wakaenda naye mpaka Athene, kisha wakarudi Beroya wakiwa na maagizo kutoka kwa Paulo kuhusu Sila na Timotheo kwamba wamfuate upesi iwezekanavyo. Paulo alipokuwa akiwasubiri huko Athene, alisumbuka sana moyoni mwake kuona vile mji huo ulivyojaa sanamu. Hivyo akahojiana kwenye sinagogi na Wayahudi pamoja na Wayunani waliomcha Mungu, na pia sokoni kila siku na watu aliopatana nao huko. Kisha baadhi ya Waepikureo na Wastoiko wenye falsafa wakakutana naye. Baadhi yao wakasema, “Je, huyu mpayukaji anajaribu kusema nini?” Wengine wakasema, “Inaonekana anasema habari za miungu ya kigeni.” Walisema haya kwa sababu Paulo alikuwa anahubiri habari njema kuhusu Yesu na ufufuo wa wafu. Hivyo wakamchukua na kumleta kwenye mkutano wa Areopago, walikomwambia, “Je, tunaweza kujua mafundisho haya mapya unayofundisha ni nini? Wewe unaleta mambo mapya masikioni mwetu, hivyo tungetaka kujua maana yake ni nini.” (Waathene na wageni wote walioishi humo hawakutumia muda wao kufanya chochote kingine isipokuwa kueleza au kusikia mambo mapya). Ndipo Paulo akasimama katikati ya Areopago akasema, “Enyi watu wa Athene! Ninaona kwamba katika kila jambo ninyi ni watu wa dini sana. Kwa kuwa nilipokuwa nikitembea mjini na kuangalia kwa bidii vitu vyenu vya kuabudiwa, niliona huko madhabahu moja iliyoandikwa: KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi sasa kile ambacho mmekuwa mkikiabudu kama kisichojulikana, ndicho ninachowahubiria. “Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu. Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote. Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu. ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’ “Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu. Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.” Waliposikia habari za ufufuo wa wafu, baadhi yao wakadhihaki, lakini wengine wakasema, “Tunataka kukusikia tena ukizungumza juu ya jambo hili.” Kwa hiyo Paulo akaondoka katikati yao. Lakini baadhi yao wakaungana naye wakaamini. Kati yao alikuwepo Dionisio, Mwareopago na mwanamke mmoja aliyeitwa Damari na wengine wengi.

Shirikisha
Soma Matendo 17