Matendo 15:36-40
Matendo 15:36-40 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya siku kadhaa, Paulo alimwambia Barnaba, “Turudi tukawatembelee wale ndugu katika kila mji tulikolihubiri neno la Bwana, tukajionee jinsi wanavyoendelea.” Barnaba alitaka wamchukue pia Yohane aitwaye Marko. Lakini Paulo hakupendelea kumchukua Marko, ambaye awali aliwaacha kule Pamfulia na kukataa kushiriki katika kazi yao. Basi, kukatokea ubishi mkali kati yao, wakaachana. Barnaba akamchukua Marko, wakapanda meli kwenda Kupro. Naye Paulo akamchagua Sila, na baada ya ndugu wa mahali hapo kumweka chini ya ulinzi wa neema ya Bwana, akaondoka.
Matendo 15:36-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya siku kadhaa Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Turejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wako hali gani. Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao. Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini. Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akaabiri kwenda Kipro. Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na wale ndugu apewe neema ya Bwana.
Matendo 15:36-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baada ya siku kadha wa kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Mrejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani. Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao. Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini. Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda Kipro. Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na wale ndugu apewe neema ya Bwana.
Matendo 15:36-40 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baada ya muda, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi tukawatembelee ndugu katika miji yote tuliyohubiri neno la Bwana tuone jinsi wanavyoendelea.” Barnaba alitaka wamchukue Yohana aitwaye Marko waende naye. Lakini Paulo aliona si vyema kwa sababu aliwahi kuwaacha walipokuwa huko Pamfilia, hakutaka kuendelea kufanya kazi naye. Pakatokea ubishi mkali kati ya Paulo na Barnaba kuhusu jambo hili, hivyo wakagawanyika. Barnaba akamchukua Yohana Marko wakasafiri baharini kwenda Kipro. Lakini Paulo akamchagua Sila na akaondoka baada ya ndugu kuwatakia neema ya Bwana.