Matendo 14:14-20
Matendo 14:14-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini mitume Paulo na Barnaba waliposikia haya, wakararua nguo zao, wakawaendea wale watu kwa haraka, wakawapigia kelele, wakisema, “Enyi watu, kwa nini mnafanya mambo haya? Sisi ni wanadamu tu kama ninyi! Tunawaletea habari njema, tukiwaambia kwamba mgeuke mtoke katika mambo haya yasiyofaa, mmwelekee Mungu aliye hai, aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo. Zamani aliwaachia mataifa waishi walivyotaka. Lakini hakuacha kuwaonyesha watu uwepo wake: Ameonyesha wema kwa kuwanyeshea mvua toka mbinguni na kuwapa mazao kwa majira yake, naye amewapa chakula tele na kuijaza mioyo yenu na furaha.” Hata kwa maneno haya yote, ilikuwa vigumu kuuzuia ule umati wa watu kuwatolea dhabihu. Ndipo wakaja baadhi ya Wayahudi kutoka Antiokia na Ikonio wakawashawishi wale watu, wakampiga Paulo kwa mawe, wakamburuta hadi nje ya mji, wakidhani amekufa. Lakini baada ya wanafunzi kukusanyika akainuka na kurudi mjini. Kesho yake yeye na Barnaba wakaondoka kwenda Derbe.
Matendo 14:14-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Barnaba na Paulo walipopata habari hizo waliyararua mavazi yao na kukimbilia katika lile kundi la watu wakisema kwa sauti kubwa: “Ndugu, kwa nini mnafanya mambo hayo? Sisi pia ni binadamu kama nyinyi. Na, tuko hapa kuwahubirieni Habari Njema, mpate kuziacha hizi sanamu tupu, mkamgeukie Mungu aliye hai, Mungu aliyeumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo. Zamani Mungu aliruhusu kila taifa lifanye lilivyopenda. Hata hivyo, Mungu hakuacha kujidhihirisha kwa mambo mema anayowatendea: Huwanyeshea mvua toka angani, huwapa mavuno kwa wakati wake, huwapa chakula na kuijaza mioyo yenu furaha.” Ingawa walisema hivyo haikuwa rahisi kuwazuia wale watu wasiwatambikie. Lakini Wayahudi kadhaa walikuja kutoka Antiokia na Ikonio, wakawafanya watu wajiunge nao, wakampiga mawe Paulo na kumburuta hadi nje ya mji wakidhani amekwisha kufa. Lakini waumini walipokusanyika na kumzunguka, aliamka, akarudi mjini. Kesho yake, yeye pamoja na Barnaba walikwenda Derbe.
Matendo 14:14-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika umati wa watu, wakipiga kelele, wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; tunawahubiria Habari Njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; ambaye zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao wenyewe. Lakini hakujiacha pasipo ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema, akiwapeni mvua kutoka mbinguni, na nyakati za mavuno, akiwashibisha mioyo yenu chakula na furaha. Na kwa maneno hayo wakawazuia watu kwa shida, wasiwatolee dhabihu. Lakini Wayahudi wakafika toka Antiokia na Ikonio, wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji, wakidhania ya kuwa amekwisha kufa. Lakini wanafunzi walipokuwa wakimzunguka pande zote, akasimama, akaingia ndani ya mji; na kesho yake akatoka, akaenda zake pamoja na Barnaba mpaka Derbe.
Matendo 14:14-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele, wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; ambaye zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao wenyewe. Lakini hakujiacha pasipo ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema, akiwapeni mvua kutoka mbinguni, na nyakati za mavuno, akiwashibisha mioyo yenu chakula na furaha. Na kwa maneno hayo wakawazuia makutano kwa shida, wasiwatolee dhabihu. Lakini Wayahudi wakafika toka Antiokia na Ikonio, wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji, wakidhania ya kuwa amekwisha kufa. Lakini wanafunzi walipokuwa wakimzunguka pande zote, akasimama, akaingia ndani ya mji; na siku ya pili yake akatoka, akaenda zake pamoja na Barnaba mpaka Derbe.