Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 11:1-30

Matendo 11:1-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Mitume na ndugu kule Yudea walisikia kwamba watu wa mataifa mengine pia walikuwa wamelipokea neno la Mungu. Basi, Petro aliporudi Yerusalemu, wale Wayahudi waumini waliopendelea watu wa mataifa mengine watahiriwe, walimlaumu wakisema: “Wewe umekwenda kukaa na watu wasiotahiriwa na hata umekula pamoja nao! Hapo Petro akawaeleza kinaganaga juu ya yale yaliyotendeka tangu mwanzo: “Siku moja nikiwa nasali mjini Yopa, niliona maono; niliona kitu kama shuka kubwa ikishushwa chini kutoka mbinguni ikiwa imeshikwa pembe zake nne, ikawekwa kando yangu. Nilichungulia ndani kwa makini nikaona wanyama wenye miguu minne, wanyama wa mwituni, wanyama watambaao na ndege wa angani. Kisha nikasikia sauti ikiniambia: ‘Petro amka, chinja, ule.’ Lakini mimi nikasema: ‘La, Bwana; maana chochote kilicho najisi au kichafu hakijapata kamwe kuingia kinywani mwangu.’ Ile sauti ikasikika tena kutoka mbinguni: ‘Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa.’ Jambo hilo lilifanyika mara tatu, na mwishowe vyote vilirudishwa juu mbinguni. Ghafla, watu watatu waliokuwa wametumwa kwangu kutoka Kaisarea waliwasili kwenye nyumba nilimokuwa nakaa. Roho aliniambia niende pamoja nao bila kusita. Hawa ndugu sita waliandamana nami pia kwenda Kaisarea na huko tuliingia nyumbani mwa Kornelio. Yeye alitueleza jinsi alivyokuwa amemwona malaika amesimama nyumbani mwake na kumwambia: ‘Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro. Yeye atakuambia maneno ambayo kwayo wewe na jamaa yako yote mtaokolewa.’ Na nilipoanza tu kuongea, Roho Mtakatifu aliwashukia kama alivyotushukia sisi pale awali. Hapo nilikumbuka yale maneno Bwana aliyosema: ‘Yohane alibatiza kwa maji, lakini nyinyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.’ Basi, kama Mungu amewapa pia watu wa mataifa mengine kipawa kilekile alichotupa sisi tulipomwamini Bwana Yesu Kristo, je, mimi ni nani hata nijaribu kumpinga Mungu?” Waliposikia hayo, waliacha ubishi, wakamtukuza Mungu wakisema, “Mungu amewapa watu wa mataifa mengine nafasi ya kutubu wapate uhai!” Kutokana na mateso yaliyotokea wakati Stefano alipouawa, waumini walitawanyika. Wengine walikwenda mpaka Foinike, Kupro na Antiokia wakihubiri ule ujumbe kwa Wayahudi tu. Lakini baadhi ya waumini waliotoka Kupro na Kurene, walikwenda Antiokia wakautangaza huo ujumbe kwa watu wa mataifa mengine wakiwahubiria Habari Njema juu ya Bwana Yesu. Bwana aliwasaidia na idadi kubwa ya watu iliamini na kumgeukia Bwana. Habari ya jambo hilo ikasikika kwa lile kanisa la Yerusalemu. Hivyo wakamtuma Barnaba aende Antiokia. Alipofika huko na kuona jinsi Mungu alivyowaneemesha wale watu, alifurahi na kuwahimiza wote wadumu katika uaminifu wao kwa Bwana. Barnaba alikuwa mtu mwema na mwenye kujaa Roho Mtakatifu na imani. Kundi kubwa la watu lilivutwa kwa Bwana. Kisha, Barnaba alikwenda Tarso kumtafuta Saulo. Alipompata, alimleta Antiokia. Nao wote wawili walikaa na ile jumuiya ya kanisa kwa mwaka wote mzima wakifundisha kundi kubwa la watu. Huko Antiokia, ndiko kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo. Wakati huohuo, manabii kadhaa walikuja Antiokia kutoka Yerusalemu. Basi, mmoja wao aitwaye Agabo alisimama, na kwa uwezo wa Roho akabashiri kwamba kutakuwa na njaa kubwa katika nchi yote. (Njaa hiyo ilitokea wakati wa utawala wa Klaudio). Wale wanafunzi waliamua kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake apeleke chochote ili kuwasaidia wale ndugu waliokuwa wanaishi Yudea. Basi, wakafanya hivyo na kuwapa Barnaba na Saulo mchango huo wauwasilishe wao wenyewe kwa wazee wa kanisa.

Shirikisha
Soma Matendo 11

Matendo 11:1-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Yudea wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu. Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye, wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao. Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema, Nilikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inateremshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikia. Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, wale watambaao, na ndege wa angani. Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule. Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijawahi kuingia kinywani mwangu. Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni. Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo, waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria. Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule; akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro, atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote. Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo. Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, Yohana alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu. Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu? Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba liletalo uzima. Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hadi Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao. Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kigiriki, wakihubiri Habari Njema za Bwana Yesu. Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana. Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hadi Antiokia. Naye, alipofika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa moyo wote. Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana. Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia. Siku zizo hizo manabii waliteremka kutoka Yerusalemu hadi Antiokia. Na tulipokusanyika akasimama mmoja wao, jina lake Agabo, akaonesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio. Na wale wanafunzi, kila mtu kwa kadiri ya alivyofanikiwa, wakaazimu kupeleka msaada kwa ndugu zao waliokaa Yudea. Wakafanya hivyo, wakawapelekea wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.

Shirikisha
Soma Matendo 11

Matendo 11:1-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu. Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye, wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao. Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema, Nalikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inatelemshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikilia. Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, nao watambaao, na ndege wa angani. Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule. Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu. Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni. Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo, waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria. Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule; akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro, atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote. Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo. Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, Yohana alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu. Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu? Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba liletalo uzima. Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao. Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kiyunani, wakihubiri habari njema za Bwana Yesu. Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana. Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia. Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana. Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia. Siku zizo hizo manabii walitelemka kutoka Yerusalemu hata Antiokia. Na tulipokusanyika akasimama mmoja wao, jina lake Agabo, akaonyesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio. Na wale wanafunzi, kila mtu kwa kadiri ya alivyofanikiwa, wakaazimu kupeleka msaada kwa ndugu zao waliokaa Uyahudi. Wakafanya hivyo, wakawapelekea wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.

Shirikisha
Soma Matendo 11

Matendo 11:1-30 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mitume na ndugu walioamini waliokuwa huko Uyahudi wakasikia kuwa watu wa Mataifa nao wamepokea neno la Mungu. Hivyo Petro alipopanda Yerusalemu, wale wa tohara waliokuwa wameamini wakamshutumu, wakisema, “Ulikwenda kwa watu wasiotahiriwa na kula pamoja nao.” Ndipo Petro akaanza kuwaeleza kuhusu mambo yote yalivyotokea hatua kwa hatua akisema, “Nilikuwa katika mji wa Yafa nikiomba, nami nikapitiwa na usingizi wa ghafula, nikaona maono. Kulikuwa na kitu kama nguo kubwa ikishuka kutoka mbinguni, ikishushwa kwa ncha zake nne, nayo ikanikaribia. Nilipoangalia ndani yake kwa karibu niliona wanyama wenye miguu minne wa nchini, wanyama wa mwitu, watambaao na ndege wa angani. Ndipo nikasikia sauti ikiniambia, ‘Petro, ondoka uchinje na ule.’ “Nikajibu, ‘La hasha Bwana! Kitu chochote kilicho najisi hakijaingia kinywani mwangu.’ “Sauti ikasema kutoka mbinguni mara ya pili, ‘Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.’ Jambo hili lilitokea mara tatu, ndipo kile kitu kikavutwa tena mbinguni. “Wakati ule ule watu watatu, waliokuwa wametumwa kutoka Kaisaria waliwasili katika nyumba niliyokuwa nikikaa. Roho Mtakatifu akaniambia niende nao bila kuwa na ubaguzi kati yao na sisi. Hawa ndugu sita pia walifuatana nami, nasi tukaingia nyumbani mwa huyo Kornelio. Akatuambia jinsi alivyoona malaika aliyekuwa amesimama katika nyumba yake na kusema, ‘Tuma watu waende Yafa wakamlete Simoni aitwaye Petro. Yeye atakupa ujumbe ambao kwa huo wewe na wa nyumbani mwako wote mtaokoka.’ “Nami nilipoanza kusema, Roho Mtakatifu akashuka juu yao kama vile alivyotushukia sisi hapo mwanzo. Nami nikakumbuka neno la Bwana alivyosema, ‘Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ Basi ikiwa Mungu aliwapa hawa watu kipawa kile kile alichotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani hata nifikirie kuwa ningeweza kumpinga Mungu?” Waliposikia haya hawakuwa na la kupinga zaidi. Nao wakamwadhimisha Mungu wakisema, “Basi, Mungu amewapa hata watu wa Mataifa toba iletayo uzima wa milele.” Basi wale waliotawanyika kwa ajili ya mateso yaliyotokana na kifo cha Stefano, wakasafiri hadi Foinike na Kipro na Antiokia. Nao hawakuhubiri lile Neno kwa mtu yeyote isipokuwa Wayahudi. Lakini baadhi yao walikuwepo watu wa Kipro na Kirene, ambao walipokuja Antiokia walinena na Wayunani pia wakiwahubiria habari njema za Bwana Yesu. Mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, nayo idadi kubwa ya watu wakaamini na kumgeukia Bwana. Habari hizi zilipofika masikioni mwa kanisa huko Yerusalemu, wakamtuma Barnaba aende Antiokia. Alipofika na kuona madhihirisho ya neema ya Mungu, akafurahi na kuwatia moyo waendelee kuwa waaminifu kwa Bwana kwa mioyo yao yote. Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu, mwenye imani, nayo idadi kubwa ya watu wakaongezeka kwa Bwana. Kisha Barnaba akaenda Tarso kumtafuta Sauli, naye alipompata akamleta Antiokia. Hivyo kwa mwaka mzima Barnaba na Sauli wakakutana na kanisa na kufundisha idadi kubwa ya watu. Ilikuwa ni katika kanisa la Antiokia kwa mara ya kwanza wanafunzi waliitwa Wakristo. Wakati huo manabii walishuka toka Yerusalemu hadi Antiokia. Mmoja wao, jina lake Agabo, akasimama akatabiri kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itaenea ulimwengu mzima. Njaa hiyo ilitokea wakati wa utawala wa Klaudio. Mitume wakaamua kwamba kila mtu, kulingana na uwezo alio nao, atoe msaada kwa ajili ya ndugu wanaoishi Uyahudi. Wakafanya hivyo, misaada yao ikapelekwa kwa wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.

Shirikisha
Soma Matendo 11