Matendo 11:1-10
Matendo 11:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Mitume na ndugu kule Yudea walisikia kwamba watu wa mataifa mengine pia walikuwa wamelipokea neno la Mungu. Basi, Petro aliporudi Yerusalemu, wale Wayahudi waumini waliopendelea watu wa mataifa mengine watahiriwe, walimlaumu wakisema: “Wewe umekwenda kukaa na watu wasiotahiriwa na hata umekula pamoja nao! Hapo Petro akawaeleza kinaganaga juu ya yale yaliyotendeka tangu mwanzo: “Siku moja nikiwa nasali mjini Yopa, niliona maono; niliona kitu kama shuka kubwa ikishushwa chini kutoka mbinguni ikiwa imeshikwa pembe zake nne, ikawekwa kando yangu. Nilichungulia ndani kwa makini nikaona wanyama wenye miguu minne, wanyama wa mwituni, wanyama watambaao na ndege wa angani. Kisha nikasikia sauti ikiniambia: ‘Petro amka, chinja, ule.’ Lakini mimi nikasema: ‘La, Bwana; maana chochote kilicho najisi au kichafu hakijapata kamwe kuingia kinywani mwangu.’ Ile sauti ikasikika tena kutoka mbinguni: ‘Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa.’ Jambo hilo lilifanyika mara tatu, na mwishowe vyote vilirudishwa juu mbinguni.
Matendo 11:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Yudea wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu. Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye, wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao. Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema, Nilikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inateremshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikia. Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, wale watambaao, na ndege wa angani. Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule. Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijawahi kuingia kinywani mwangu. Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni.
Matendo 11:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu. Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye, wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao. Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema, Nalikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inatelemshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikilia. Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, nao watambaao, na ndege wa angani. Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule. Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu. Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni.
Matendo 11:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mitume na ndugu walioamini waliokuwa huko Uyahudi wakasikia kuwa watu wa Mataifa nao wamepokea neno la Mungu. Hivyo Petro alipopanda Yerusalemu, wale wa tohara waliokuwa wameamini wakamshutumu, wakisema, “Ulikwenda kwa watu wasiotahiriwa na kula pamoja nao.” Ndipo Petro akaanza kuwaeleza kuhusu mambo yote yalivyotokea hatua kwa hatua akisema, “Nilikuwa katika mji wa Yafa nikiomba, nami nikapitiwa na usingizi wa ghafula, nikaona maono. Kulikuwa na kitu kama nguo kubwa ikishuka kutoka mbinguni, ikishushwa kwa ncha zake nne, nayo ikanikaribia. Nilipoangalia ndani yake kwa karibu niliona wanyama wenye miguu minne wa nchini, wanyama wa mwitu, watambaao na ndege wa angani. Ndipo nikasikia sauti ikiniambia, ‘Petro, ondoka uchinje na ule.’ “Nikajibu, ‘La hasha Bwana! Kitu chochote kilicho najisi hakijaingia kinywani mwangu.’ “Sauti ikasema kutoka mbinguni mara ya pili, ‘Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.’ Jambo hili lilitokea mara tatu, ndipo kile kitu kikavutwa tena mbinguni.