Matendo 10:1-8
Matendo 10:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Kulikuwa na mtu mmoja huko Kaisarea aitwaye Kornelio, jemadari wa kikosi kimoja kiitwacho “Kikosi cha Italia.” Alikuwa mtu mwema; naye pamoja na jamaa yake yote walimcha Mungu; alikuwa anafanya mengi kusaidia maskini wa Kiyahudi na alikuwa anasali daima. Yapata saa tisa alasiri, aliona dhahiri katika maono malaika wa Mungu akiingia ndani na kumwambia, “Kornelio!” Kornelio alimkodolea macho huyo malaika kwa hofu, akamwambia, “Kuna nini Mheshimiwa?” Huyo malaika akamwambia, “Mungu amezipokea sala na sadaka zako kwa maskini wala hatazisahau. Sasa, watume watu Yopa wakamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro. Yeye yumo nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko karibu na bahari.” Huyo malaika aliyesema hayo alipokwisha kwenda zake, Kornelio aliwaita watumishi wawili wa nyumbani na mmoja wa askari zake ambaye alikuwa mcha Mungu, akawaeleza yote yaliyotukia, akawatuma Yopa.
Matendo 10:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, jemadari wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamkodolea macho, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, tuma watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda. Na yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa kati ya wale waliomhudumia daima; na alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa.
Matendo 10:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika mji wa Kaisaria palikuwa na mtu jina lake Kornelio, ambaye alikuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia. Yeye alikuwa mcha Mungu pamoja na wote wa nyumbani mwake. Aliwapa watu sadaka nyingi na kumwomba Mungu daima. Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono waziwazi, malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!” Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?” Malaika akamwambia, “Sala zako na sadaka zako kwa maskini zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa tuma watu waende Yafa wakamwite mtu mmoja jina lake Simoni aitwaye Petro. Yeye anaishi na Simoni mtengenezaji ngozi ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.” Yule malaika aliyekuwa akizungumza naye alipoondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili pamoja na askari mmoja mcha Mungu aliyekuwa miongoni mwa wale waliomtumikia. Akawaambia mambo yote yaliyotukia, kisha akawatuma waende Yafa.
Matendo 10:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda. Na yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita wawili katika watumishi wake wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa katika wale waliomhudumia daima; na alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa.