2 Timotheo 3:1-17
2 Timotheo 3:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu. Watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu; watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema; watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu. Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo. Baadhi yao huenda katika nyumba za watu na huwateka wanawake dhaifu waliolemewa mizigo ya dhambi na ambao wanaongozwa na tamaa za kila aina; wanawake ambao wanajaribu daima kujifunza lakini hawawezi kuufikia ujuzi wa huo ukweli. Watu hao huupinga ukweli kama vile Yane na Yambre walivyompinga Mose. Hao ni watu wa akili potovu na imani ya uongo. Lakini hawataweza kuendelea zaidi kwa maana upumbavu wao utaonekana wazi kwa wote. Ndivyo ilivyokuwa kwa akina Yane na Yambre. Wewe, lakini, umeyafuata mafundisho yangu, mwenendo wangu, makusudi yangu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu, subira yangu, udhalimu na mateso. Unayajua mambo yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Lustra. Nilivumilia udhalimu mkubwa mno! Lakini Bwana aliniokoa katika mambo hayo yote. Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu lazima adhulumiwe. Watu waovu na wadanganyifu wataendelea kuwa wabaya, wakidanganya wengine, na wao wenyewe wakidanganywa. Lakini wewe dumu katika ukweli ule uliofundishwa ukaukubali kabisa. Wawajua wale waliokuwa waalimu wako, wakumbuka kwamba tangu utoto wako umejua Maandiko Matakatifu ambayo yaweza kukupatia hekima iletayo wokovu kwa njia ya imani kwa Kristo Yesu. Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundishia ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili, ili mtu wa Mungu awe mkamilifu, na tayari kabisa kufanya kila kazi njema.
2 Timotheo 3:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; walio na utaua kwa nje, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao. Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu, na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tamaa za kila namna; wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli. Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani. Lakini hawataendelea sana; maana upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile na upumbavu wa hao wanaume wawili ulivyokuwa dhahiri. Bali wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu, na upendo, na subira; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote. Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa. Lakini watu waovu na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utotoni umeyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.
2 Timotheo 3:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao. Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu, na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi; wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli. Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani. Lakini hawataendelea sana; maana upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile na upumbavu wa hao ulivyokuwa dhahiri. Bali wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu, na upendo, na saburi; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote. Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa. lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.
2 Timotheo 3:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini yakupasa ufahamu jambo hili, kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari. Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu, wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wapendao anasa zaidi kuliko kumpenda Mungu: wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje, lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu wa namna hiyo. Miongoni mwao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu na kuwachukua mateka wanawake wajinga, waliolemewa na dhambi zao na kuyumbishwa na aina zote za tamaa mbaya. Wakijifunza siku zote lakini kamwe wasiweze kufikia ujuzi wa kweli. Kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Mose, vivyo hivyo watu hawa hupingana na ile kweli. Hawa ni watu wenye akili zilizopotoka, ambao wamekataliwa kwa mambo ya imani. Lakini hawataendelea sana, kwa sababu upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama ulivyokuwa dhahiri upumbavu wa hao watu wawili. Lakini wewe umeyajua mafundisho yangu, mwenendo, makusudi, imani, uvumilivu, upendo, ustahimilivu, mateso na taabu, yaani mambo yote yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Listra, mateso yote niliyostahimili, lakini Bwana aliniokoa katika hayo yote. Naam, yeyote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Kristo Yesu atateswa. Lakini watu waovu na wadanganyaji watazidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.