Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Timotheo 2:14-26

2 Timotheo 2:14-26 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, wakumbushe watu wako mambo haya na kuwaonya mbele ya Mungu waache ubishi juu ya maneno. Ubishi huo haufai, ila huleta tu uharibifu mkuu kwa wale wanaousikia. Jitahidi kupata kibali kamili mbele ya Mungu kama mfanyakazi ambaye haoni haya juu ya kazi yake na ambaye hufundisha sawa ule ujumbe wa kweli. Jiepushe na majadiliano yasiyofaa na ya kipumbavu; kwani hayo huzidi kuwatenga watu mbali na Mungu. Mafundisho ya aina hiyo ni kama donda linalokula mwili. Miongoni mwa hao waliofundisha hayo ni Humenayo na Fileto. Hawa wamepotoka kabisa mbali na ukweli, na wanatia imani ya watu wengine katika wasiwasi kwa kusema ati ufufuo wetu umekwisha fanyika. Lakini msingi thabiti uliowekwa na Mungu uko imara, na juu yake yameandikwa maneno haya: “Bwana anawafahamu wale walio wake,” na “Kila asemaye yeye ni wa Bwana, ni lazima aachane na uovu.” Katika nyumba kubwa kuna mabakuli na vyombo vya kila namna: Vingine ni vya fedha na dhahabu, vingine vya mbao na udongo, vingine vya matumizi ya heshima na vingine kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Basi, kama mtu atajitakasa kwa kujitenga mbali na mambo hayo yote maovu, atakuwa chombo cha matumizi ya pekee, kwa sababu amewekwa wakfu, anamfaa Bwana wake na yupo tayari kwa kila kazi njema. Jiepushe na tamaa za ujana, fuata uadilifu, imani, upendo, amani, pamoja na watu wote ambao wanamwomba Bwana kwa moyo safi. Epuka ubishi wa kijinga na kipumbavu; wajua kwamba hayo huleta magomvi. Mtumishi wa Bwana asigombane. Anapaswa kuwa mpole kwa watu wote, mwalimu mwema na mvumilivu, ambaye ni mpole anapowaonya wapinzani wake, kwani huenda Mungu akawajalia nafasi ya kutubu, wakapata kuujua ukweli. Hapo fahamu zao zitawarudia tena, wakaponyoka katika mtego wa Ibilisi aliyewanasa na kuwafanya wayatii matakwa yake.

2 Timotheo 2:14-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wanaoyasikia. Jitahidi kujionesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mfanyakazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli. Jiepushe na maneno machafu yasiyo na maana, ambayo si ya dini; kwa kuwa wataendelea zaidi katika maovu, na neno lao litaenea kama donda ndugu. Miongoni mwa hao wamo Himenayo na Fileto, waliopotoka kutoka kwenye kweli, wakisema ya kwamba kiyama imekwisha tokea, hata kuipindua imani ya watu kadhaa. Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye mhuri huu, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila aliitaye jina la Bwana na auache uovu. Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima, vingine havina. Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema. Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi. Lakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi. Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awajalie ili watubu na kuijua kweli; wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambaye amewanasa, hata wakayafanya mapenzi yake.

2 Timotheo 2:14-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao. Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli. Jiepushe na maneno yasiyo na maana, ambayo si ya dini; kwa kuwa wataendelea zaidi katika maovu, na neno lao litaenea kama donda-ndugu. Miongoni mwa hao wamo Himenayo na Fileto, walioikosa ile kweli, wakisema ya kwamba kiyama imekwisha kuwapo, hata kuipindua imani ya watu kadha wa kadha. Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu. Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima, vingine havina. Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema. Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi. Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi. Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli; wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.

2 Timotheo 2:14-26 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Endelea kuwakumbusha mambo haya ukiwaonya mbele za Bwana waache kushindana kwa maneno ambayo hayana faida yoyote bali huwaangamiza tu wale wanaoyasikia. Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli. Jiepushe na maneno mabaya, yasiyo na maana, yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kukosa heshima kwa Mungu. Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kuwako, nao huharibu imani ya baadhi ya watu. Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, ukiwa na muhuri wenye maandishi haya: “Bwana anawajua walio wake”; tena, “Kila alitajaye jina la Bwana, na auache uovu.” Katika nyumba kubwa si kwamba kuna vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali pia vimo vyombo vya miti na vya udongo; vingine kwa matumizi maalum, na vingine kwa matumizi ya kawaida. Basi ikiwa mtu amejitakasa na kujitenga na hayo niliyoyataja, atakuwa chombo maalum, kilichotengwa na ambacho kinamfaa mwenye nyumba, kimeandaliwa tayari kwa kila kazi njema. Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi. Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi. Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.

2 Timotheo 2:14-26

2 Timotheo 2:14-26 BHN2 Timotheo 2:14-26 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha