2 Timotheo 1:11-18
2 Timotheo 1:11-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi nimechaguliwa niwe mtume na mwalimu kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema, nami nateseka kwa mambo haya kwa sababu hiyo. Lakini niko bado timamu kabisa kwani namjua yule niliyemwamini, tena nina hakika kwamba yeye atakilinda salama kile alichonikabidhi, mpaka siku ile. Shika kwa makini mafundisho yale ya kweli niliyokufundisha na kubaki katika hiyo imani na huo upendo wetu katika kuungana na Kristo Yesu. Jambo lile bora ulilokabidhiwa lilinde kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayeishi ndani yetu. Kama unavyojua, watu wote mkoani Asia wameniacha, miongoni mwao wakiwa Fugelo na Hermogene. Bwana aihurumie jamaa ya Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha rohoni mara nyingi, wala hakuona haya kwa kuwa nilikuwa kifungoni, ila mara tu alipofika Roma, alianza kunitafuta kwa bidii mpaka akanipata. Bwana amjalie kupata huruma ya Mungu katika siku ile! Nawe wajua vizuri mengi aliyonifanyia huko Efeso.
2 Timotheo 1:11-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
kwa ajili ya Injili hiyo niliwekwa niwe mhubiri, mtume na mwalimu. Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, lakini sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile. Shika mfano wa mafundisho ya kweli uliyoyasikia kwangu, katika imani na upendo ulio katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu. Waijua habari hii, ya kuwa wote walio wa Asia waliniepuka, ambao miongoni mwao wamo Figelo na Hermogene. Bwana awape rehema wale walio wa jamaa wa Onesiforo; maana mara nyingi aliniburudisha, wala hakuuonea haya mnyororo wangu; bali, alipokuwapo hapa Rumi, alinitafuta kwa bidii na kunipata. Bwana na amjalie ili kwamba apate rehema machoni pa Bwana siku ile. Na jinsi alivyonihudumia kwa mengi huko Efeso, wewe unajua sana.
2 Timotheo 1:11-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
ambayo kwa ajili ya hiyo naliwekwa niwe mhubiri na mtume na mwalimu. Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile. Shika kielelezo cha maneno yenye uzima uliyoyasikia kwangu, katika imani na upendo ulio katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu. Waijua habari hii, ya kuwa wote walio wa Asia waliniepuka, ambao miongoni mwao wamo Figelo na Hermogene. Bwana awape rehema wale walio wa mlango wake Onesiforo; maana mara nyingi aliniburudisha, wala hakuuonea haya mnyororo wangu; bali, alipokuwapo hapa Rumi, alinitafuta kwa bidii akanipata. Bwana na ampe kuona rehema machoni pa Bwana siku ile. Na jinsi alivyonihudumia kwa mengi huko Efeso, wewe unajua sana.
2 Timotheo 1:11-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii. Hii ndiyo sababu ninateseka namna hii, lakini sioni haya kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kuwa anaweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hadi siku ile. Shika kwa uthabiti kielelezo cha mafundisho yenye uzima yale uliyoyasikia kwangu, pamoja na imani na upendo katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana uliyokabidhiwa kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu. Unajua ya kuwa watu wote katika Asia wameniacha, miongoni mwao wamo Filego na Hermogene. Bwana akawahurumie watu wa nyumbani mwa Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha mara kwa mara wala hakuionea aibu minyororo yangu. Badala yake, alipokuwa Rumi, alinitafuta kwa bidii mpaka akanipata. Bwana na amjalie kupata rehema zake siku ile! Nawe unajua vyema jinsi alivyonisaidia huko Efeso.