2 Samueli 7:18-29
2 Samueli 7:18-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha mfalme Daudi akaingia ndani na kuketi mbele ya Mwenyezi-Mungu; halafu akaomba, “Mimi ni nani ee Bwana Mungu, na jamaa yangu ni nini hata ukaniinua mpaka hapa nilipo leo! Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Bwana Mungu; zaidi ya hayo umeiahidi jamaa yangu mambo makubwa katika miaka mingi ijayo; na kwamba umenijalia kuona hayo, Ee Bwana Mungu. Nikuambie nini zaidi, mimi Daudi, mtumishi wako? Kwani wewe unanijua mimi mtumishi wako, ee Bwana Mungu! Kutokana na ahadi yako na kulingana na moyo wako, umetenda makuu hayo yote ili unijulishe mimi mtumishi wako. Kutokana na yale tuliyosikia, wewe Mwenyezi-Mungu ni mkuu; hakuna aliye kama wewe, na hakuna Mungu mwingine ila wewe. Tena ni watu gani duniani ambao wanaweza kufananishwa na watu wako wa Israeli, ambao Mungu wake alikwenda kuwakomboa ili wawe watu wake? Wewe ee Mungu ulijifanyia jina na kujitendea mambo makubwa na ya ajabu kwa ajili ya nchi yako mbele ya watu wako ambao kwa ajili yako mwenyewe uliwaokoa kutoka Misri, ukayafukuza mataifa na miungu yake mbele yao? Hata umewaimarisha watu wako wa Israeli kwa ajili yako mwenyewe, ili wawe watu wako milele; nawe ee Mwenyezi-Mungu umekuwa Mungu wao. Basi, sasa, ee Mwenyezi-Mungu, ikamilishe ile ahadi uliyosema kuhusu mimi mtumishi wako na kuhusu jamaa yangu kama ulivyoahidi. Nalo jina lako litatukuzwa milele, nao watu watasema, ‘Mwenyezi-Mungu wa majeshi ni Mungu juu ya Israeli!’ Na jamaa yangu, mimi Daudi mtumishi wako, itaimarika mbele yako. Maana wewe, ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, umenifunulia mimi mtumishi wako, ukisema ‘Nitakujengea nyumba;’ ndio maana nina ujasiri kutoa ombi hili mbele yako. Sasa, ee Bwana Mungu, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ni kweli na umeniahidi mimi mtumishi wako jambo hili jema; kwa hiyo, nakuomba nyumba yangu mimi mtumishi wako ipate kudumu milele mbele yako; kwani wewe umesema hivyo, pia kwa baraka zako nyumba yangu itabarikiwa milele.”
2 Samueli 7:18-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Daudi, mfalme, akaingia, akaketi mbele za BWANA, akasema, Mimi ni nani, Bwana MUNGU, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa? Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Bwana MUNGU; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumishi wako, kwa miaka mingi inayokuja baadaye; na hayo kwa namna ya kibinadamu, Ee Bwana MUNGU. Na mimi, Daudi, nikuambie nini tena zaidi? Iwapo wewe umemjua mtumishi wako, Ee Bwana MUNGU. Kwa ajili ya neno lako, na kwa moyo wako mwenyewe, umetenda makuu hayo yote, ili umjulishe mtumishi wako. Kwa hiyo, wewe ndiwe mkuu, Ee BWANA Mungu, kwa maana hakuna kama wewe, wala hapana Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu. Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako, kama Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake, wawe watu wake mwenyewe, akajifanyie jina, na kutenda mambo makuu kwa ajili yenu, na mambo ya kuogofya kwa ajili ya nchi yako, mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri wawe wako, kutoka katika mataifa na miungu yao. Nawe ulijifanyia imara watu wako wa Israeli, wawe watu wako milele; nawe, BWANA, umekuwa Mungu wao. Basi sasa, Ee BWANA Mungu, neno lile ulilolinena kuhusu mtumishi wako, na kuhusu nyumba yangu, uliimarishe milele, ukatende kama ulivyosema. Jina lako na litukuzwe milele, kwa kusema, BWANA wa majeshi ndiye Mungu juu ya Israeli; na nyumba ya mtumishi wako, Daudi, itaimarika mbele zako. Kwa kuwa wewe, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli umenifunulia mimi, mtumishi wako, ukisema, Nitakujengea nyumba; kwa hiyo mimi, mtumishi wako, nimepata ujasiri nikuombe ombi hili. Na sasa, Ee Bwana MUNGU, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidia mtumishi wako jambo hili jema basi, sasa, uwe radhi, ukaibariki nyumba ya mtumishi wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana MUNGU, umelinena na kwa baraka yako nyumba ya mtumishi wako na ibarikiwe milele.
2 Samueli 7:18-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Daudi, mfalme, akaingia, akaketi mbele za BWANA, akasema, Mimi ni nani, Bwana MUNGU, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hata hapa? Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Bwana MUNGU; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumwa wako, kwa miaka mingi inayokuja baadaye; na hayo kwa namna ya kibinadamu, Ee Bwana MUNGU. Na mimi, Daudi, nikuambie nini tena zaidi? Iwapo wewe umemjua mtumwa wako, Ee Bwana MUNGU. Kwa ajili ya neno lako, na kwa moyo wako mwenyewe, umetenda makuu hayo yote, ili umjulishe mtumwa wako. Kwa hiyo, wewe ndiwe mkuu, Ee BWANA Mungu, kwa maana hakuna kama wewe, wala hapana Mungu mwingine ila wewe, kwa kadiri tulivyosikia kwa masikio yetu. Tena ni taifa lipi duniani lililo kama watu wako, kama Israeli, ambalo Mungu alikwenda kuwakomboa kwa ajili yake, wawe watu wake mwenyewe, akajifanyie jina, na kutenda mambo makuu kwa ajili yenu, na mambo ya kuogofya kwa ajili ya nchi yako, mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri wawe wako, kutoka katika mataifa na miungu yao. Nawe ulijifanyia imara watu wako Israeli, wawe watu wako milele; nawe, BWANA, umekuwa Mungu wao. Basi sasa, Ee BWANA Mungu, neno lile ulilolinena katika habari za mtumwa wako, na katika habari za nyumba yangu, ulifanye imara milele, ukatende kama ulivyosema. Jina lako na litukuzwe milele, kusema, BWANA wa majeshi ndiye Mungu juu ya Israeli; na nyumba ya mtumwa wako, Daudi, itakuwa imara mbele zako. Kwa kuwa wewe, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli umenifunulia mimi, mtumwa wako, ukisema, Nitakujengea nyumba; kwa hiyo mimi, mtumwa wako, nimeona vema moyoni mwangu nikuombe dua hii. Na sasa, Ee Bwana MUNGU, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidia mtumwa wako jambo hili jema basi, sasa, uwe radhi, ukaibarikie nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana MUNGU, umelinena na kwa baraka yako nyumba ya mtumwa wako na ibarikiwe milele.
2 Samueli 7:18-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za BWANA, akasema: “Ee BWANA Mwenyezi, mimi ni nani, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta mpaka hapa nilipo? Naam, kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee BWANA Mwenyezi, wewe umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Je, hii ndiyo njia yako ya kawaida ya kushughulika na mwanadamu, Ee BWANA Mwenyezi? “Je, Daudi aweza kukuambia nini zaidi? Kwa maana unamjua mtumishi wako, Ee BWANA Mwenyezi. Kwa ajili ya neno lako na kwa mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa na kulifanya lijulikane na lifahamike kwa mtumishi wako. “Tazama jinsi ulivyo mkuu, Ee BWANA Mwenyezi! Hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe, Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli, taifa pekee duniani ambalo Mungu alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe, na kujifanyia jina mwenyewe, kwa kufanya maajabu makubwa na ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa na miungu yao mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri? Umeimarisha watu wako Israeli hasa kama watu wako mwenyewe milele, nawe, Ee BWANA, umekuwa Mungu wao. “Basi sasa, BWANA, ukaitimize ahadi uliyosema kuhusu mtumishi wako na nyumba yake milele. Fanya kama ulivyoahidi, ili kwamba jina lako litukuke milele. Ndipo watu watasema, ‘BWANA Mwenye Nguvu Zote ni Mungu juu ya Israeli!’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itakuwa imara mbele zako. “Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, umelifunua hili kwa mtumishi wako, ukisema, ‘Nitakujengea nyumba.’ Hivyo mtumishi wako amepata ujasiri kukuletea dua hii. Ee BWANA Mwenyezi, wewe ndiwe Mungu! Maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri. Sasa naomba uwe radhi kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu mbele zako milele, kwa maana wewe, Ee BWANA Mwenyezi, umesema, na kwa baraka zako nyumba ya mtumishi wako itaendelea kubarikiwa milele.”