Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 7:1-18

2 Samueli 7:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo BWANA alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana BWANA yu pamoja nawe. Ikawa usiku uo huo, neno la BWANA likamfikia Nathani kusema, Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani. Mahali mwote nilimokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lo lote na mtu ye yote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi? Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, BWANA wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani. Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; naam, kama vilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA atakujengea nyumba. Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu; lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele. Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi. Ndipo Daudi, mfalme, akaingia, akaketi mbele za BWANA, akasema, Mimi ni nani, Bwana MUNGU, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hata hapa?

2 Samueli 7:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya mfalme kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, naye BWANA akiwa amemstarehesha pande zote mbali na adui zake, akamwambia nabii Nathani, “Mimi hapa, ninaishi katika jumba la kifalme la mierezi, wakati Sanduku la Mungu limebaki katika hema.” Nathani akamjibu mfalme, “Lolote ulilo nalo moyoni, endelea ukalifanye, kwa maana BWANA yu pamoja nawe.” Usiku ule neno la BWANA likamjia Nathani, kusema: “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Je, ewe ndiwe wa kunijengea mimi nyumba ili nikae ndani yake? Sijakaa ndani ya nyumba tangu siku niliyowaleta Waisraeli kutoka Misri hadi leo. Nimekuwa nikitembea kutoka mahali pamoja hadi mahali pengine ndani ya hema kama makao yangu. Popote nilipotembea pamoja na Waisraeli wote, je, nimewahi kumwambia kiongozi wao yeyote niliyemwamuru kuwachunga watu wangu Israeli, “Kwa nini hujanijengea nyumba ya mierezi?” ’ “Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: Nilikutoa wewe kutoka machungani na kutoka kuandama kundi la kondoo na mbuzi ili kuwaongoza watu wangu Israeli. Nimekuwa pamoja nawe popote ulipokwenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani. Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali niwapande humo ili kwamba wawe na nyumbani kwao wenyewe wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawaonea tena, kama walivyofanya mwanzoni, na kama walivyofanya tangu mwanzo wakati nilipowaweka viongozi juu ya watu wangu Israeli. Pia nitawapa raha mbele ya adui zenu wote. “ ‘BWANA akuambia kwamba BWANA mwenyewe atakujengea nyumba. Siku zako zitakapokwisha nawe ulale pamoja na baba zako, nitainua mzao wako aingie mahali pako, ambaye atatoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, nami nitaimarisha kiti cha enzi cha ufalme wake milele. Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Atakapokosea nitamwadhibu kwa fimbo ya wanadamu, kwa adhabu ya kupigwa na wanadamu. Lakini upendo wangu kamwe hautaondolewa kwake, kama nilivyouondoa kwa Sauli, niliyemwondoa atoke mbele yako. Nyumba yako na ufalme wako utadumu milele mbele zangu, kiti chako cha enzi kitafanywa imara milele.’ ” Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya. Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za BWANA, akasema: “Ee BWANA Mwenyezi, mimi ni nani, na jamaa yangu ni nini, hata umenileta mpaka hapa nilipo?

2 Samueli 7:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Wakati mfalme Daudi alipokuwa akikaa katika ikulu, naye Mwenyezi-Mungu amemuwezesha kuwa na amani na adui zake kila upande, mfalme Daudi akamwambia nabii Nathani, “Hebu tazama; mimi ninakaa katika nyumba iliyojengwa kwa mierezi, lakini sanduku la Mungu linakaa hemani.” Nathani akamwambia mfalme, “Nenda ufanye chochote unachofikiria moyoni mwako, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu yu pamoja nawe.” Lakini usiku uleule neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Nathani, “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Je, wewe utanijengea nyumba ya kukaa? Tangu siku ile nilipowatoa Waisraeli nchini Misri mpaka hivi leo sijaishi kwenye nyumba. Nimetembea kila mahali nikiwa ninakaa hemani. Je, kila mahali ambako nimekwenda na Waisraeli wote nimemwuliza mtu yeyote wa Israeli ambaye nilimwamuru awachunge watu wa Israeli: Kwa nini hajanijengea nyumba ya mierezi? Kwa hiyo basi, mwambie mtumishi wangu Daudi: Mwenyezi-Mungu wa majeshi anasema hivi: Nilikutoa malishoni ulikokuwa unawachunga kondoo, ili uwe mkuu wa watu wangu Israeli. Tangu wakati huo nimekuwa pamoja nawe kokote ulikokwenda na nimewaangamiza adui zako wote mbele yako. Nitakufanya kuwa maarufu kama wakuu wengine duniani. Nami nitawachagulia watu wangu wa Israeli mahali pa kuishi, niwapandikize, ili waishi mahali pao wenyewe, wasisumbuliwe tena. Nao watu wakatili wanaotumia nguvu hawatawatesa tena kama hapo awali, tangu wakati nilipowateua waamuzi juu ya watu wangu Israeli, nami nitakulinda kutokana na adui zako wote. Zaidi ya yote, mimi Mwenyezi-Mungu nakutangazia kuwa nitakujengea nyumba. Siku zako zitakapotimia na utakapofariki na kujiunga na babu zako, nitamfanya mmoja wa watoto wako wewe mwenyewe awe mfalme, nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya jina langu na kiti chake cha enzi cha ufalme wake nitakiimarisha milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Akifanya maovu, nitamrudi kama wanadamu wanavyowarudi wana wao kwa fimbo. Lakini sitamwondolea fadhili zangu kama vile nilivyoziondoa kwa Shauli, niliyemwondoa mbele yako. Ukoo wako na ufalme wako vitadumu imara daima. Kiti chako cha enzi kitakuwa imara milele.’” Nathani alimweleza Daudi kila kitu ambacho alioneshwa katika maono hayo na Mungu. Kisha mfalme Daudi akaingia ndani na kuketi mbele ya Mwenyezi-Mungu; halafu akaomba, “Mimi ni nani ee Bwana Mungu, na jamaa yangu ni nini hata ukaniinua mpaka hapa nilipo leo!

2 Samueli 7:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo BWANA alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana BWANA yuko pamoja nawe. Ikawa usiku uo huo, neno la BWANA likamfikia Nathani kusema, Nenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani. Mahali kote nilikokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lolote na mtu yeyote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi? Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, BWANA wa majeshi asema hivi, Nilikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani. Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; naam, kama ilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA atakujengea nyumba. Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakiimarisha milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu; lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitaimarishwa milele. Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi. Ndipo Daudi, mfalme, akaingia, akaketi mbele za BWANA, akasema, Mimi ni nani, Bwana MUNGU, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hadi hapa?