Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 7:1-11

2 Samueli 7:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

Wakati mfalme Daudi alipokuwa akikaa katika ikulu, naye Mwenyezi-Mungu amemuwezesha kuwa na amani na adui zake kila upande, mfalme Daudi akamwambia nabii Nathani, “Hebu tazama; mimi ninakaa katika nyumba iliyojengwa kwa mierezi, lakini sanduku la Mungu linakaa hemani.” Nathani akamwambia mfalme, “Nenda ufanye chochote unachofikiria moyoni mwako, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu yu pamoja nawe.” Lakini usiku uleule neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Nathani, “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Je, wewe utanijengea nyumba ya kukaa? Tangu siku ile nilipowatoa Waisraeli nchini Misri mpaka hivi leo sijaishi kwenye nyumba. Nimetembea kila mahali nikiwa ninakaa hemani. Je, kila mahali ambako nimekwenda na Waisraeli wote nimemwuliza mtu yeyote wa Israeli ambaye nilimwamuru awachunge watu wa Israeli: Kwa nini hajanijengea nyumba ya mierezi? Kwa hiyo basi, mwambie mtumishi wangu Daudi: Mwenyezi-Mungu wa majeshi anasema hivi: Nilikutoa malishoni ulikokuwa unawachunga kondoo, ili uwe mkuu wa watu wangu Israeli. Tangu wakati huo nimekuwa pamoja nawe kokote ulikokwenda na nimewaangamiza adui zako wote mbele yako. Nitakufanya kuwa maarufu kama wakuu wengine duniani. Nami nitawachagulia watu wangu wa Israeli mahali pa kuishi, niwapandikize, ili waishi mahali pao wenyewe, wasisumbuliwe tena. Nao watu wakatili wanaotumia nguvu hawatawatesa tena kama hapo awali, tangu wakati nilipowateua waamuzi juu ya watu wangu Israeli, nami nitakulinda kutokana na adui zako wote. Zaidi ya yote, mimi Mwenyezi-Mungu nakutangazia kuwa nitakujengea nyumba.

2 Samueli 7:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo BWANA alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana BWANA yuko pamoja nawe. Ikawa usiku uo huo, neno la BWANA likamfikia Nathani kusema, Nenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani. Mahali kote nilikokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lolote na mtu yeyote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi? Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, BWANA wa majeshi asema hivi, Nilikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani. Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; naam, kama ilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA atakujengea nyumba.

2 Samueli 7:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo BWANA alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana BWANA yu pamoja nawe. Ikawa usiku uo huo, neno la BWANA likamfikia Nathani kusema, Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani. Mahali mwote nilimokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lo lote na mtu ye yote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi? Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, BWANA wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani. Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; naam, kama vilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote. Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA atakujengea nyumba.

2 Samueli 7:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Baada ya mfalme kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, naye BWANA akiwa amempa amani pande zote kutoka kwa adui zake, akamwambia nabii Nathani, “Mimi hapa ninaishi katika jumba la kifalme la mwerezi, wakati Sanduku la Mungu limebaki katika hema.” Nathani akamjibu mfalme, “Lolote ulilo nalo moyoni, endelea ukalifanye, kwa maana BWANA yu pamoja nawe.” Usiku ule neno la BWANA likamjia Nathani, kusema: “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Je, ewe ndiwe wa kunijengea mimi nyumba ili nikae ndani yake? Sijakaa ndani ya nyumba tangu siku niliyowaleta Waisraeli kutoka Misri hadi leo. Nimekuwa nikitembea kutoka mahali pamoja hadi mahali pengine na hema kama makao yangu. Popote nilipotembea pamoja na Waisraeli wote, je, nimewahi kumwambia kiongozi wao yeyote niliyemwamuru kuwachunga watu wangu Israeli, “Kwa nini hujanijengea nyumba ya mwerezi?” ’ “Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: Nilikutoa malishoni na kutoka kulisha mifugo, ili uwaongoze watu wangu Israeli. Nimekuwa pamoja nawe popote ulipoenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani. Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali niwapande humo ili wawe na nyumbani kwao wenyewe wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawatesa tena, kama walivyofanya mwanzoni, na kama walivyofanya tangu mwanzo wakati nilipowaweka viongozi juu ya watu wangu Israeli. Pia nitawapa amani mbele ya adui zenu wote. “ ‘BWANA akuambia kwamba BWANA mwenyewe atakujengea nyumba.