Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 6:1-15

2 Samueli 6:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

Kwa mara nyingine, Daudi aliwakusanya wale askari bora wa Israeli, jumla yao 30,000. Daudi aliondoka akaenda pamoja na watu wake wote aliokuwa nao kutoka Baala-yuda, kwenda kulichukua toka huko sanduku la Mungu linaloitwa kwa jina lake Mwenyezi-Mungu wa Majeshi, akaaye kwenye kiti chake cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa. Basi, wakalichukua sanduku la Mungu kutoka katika nyumba ya Abinadabu iliyokuwa mlimani, wakalibeba juu ya gari jipya. Uza na Ahio wana wa Abinadabu wakawa wanaliendesha gari hilo jipya, likiwa na sanduku hilo la Mungu, naye Ahio akiwa anatangulia mbele ya sanduku hilo. Daudi na watu wote wa Israeli, wakawa wanaimba nyimbo na kucheza kwa nguvu zao zote, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Walipiga ala za muziki zilizotengenezwa kwa mvinje: Vinubi, vinanda, matari, kayamba na matoazi. Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Nakoni, Uza aliunyosha mkono wake na kulishika sanduku la Mungu kwa sababu wale ng'ombe walijikwaa. Hapo, hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Uza. Mungu akamuua palepale. Uza akafa papo hapo kando ya sanduku la Mungu. Naye Daudi alikasirika kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alimwadhibu Uza kwa hasira. Hivyo, mahali hapo pakaitwa Peres-uza mpaka hivi leo. Siku hiyo Daudi alimwogopa Mwenyezi-Mungu akasema, “Sasa litanijiaje sanduku la Mwenyezi-Mungu?” Kwa hiyo, Daudi hakuwa tayari kulipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu ndani ya mji wa Daudi, bali Daudi alilipeleka nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku hilo la Mwenyezi-Mungu lilikaa nyumbani kwa Obed-edomu kwa muda wa miezi mitatu; naye Mwenyezi-Mungu akambariki Obed-edomu pamoja na jamaa yake. Mfalme Daudi aliposikia kuwa Mwenyezi-Mungu ameibariki jamaa ya Obed-edomu na vitu vyote alivyokuwa navyo kwa sababu ya sanduku la Mungu, akaenda kulichukua sanduku la agano kutoka nyumbani kwa Obed-edomu na kulipeleka kwenye mji wa Daudi kwa shangwe. Watu wale waliolibeba sanduku la Mwenyezi-Mungu kila walipopiga hatua sita, Daudi alitoa tambiko: Fahali na ndama mmoja mnono. Daudi akiwa amejifunga kizibao cha kuhani kiunoni mwake alicheza kwa nguvu zake zote mbele ya Mwenyezi-Mungu. Hivyo, yeye na Waisraeli wote walilipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu hadi mjini mwa Daudi kwa shangwe na sauti kubwa ya tarumbeta.

2 Samueli 6:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Daudi akakusanya tena wateule wote wa Israeli, watu elfu thelathini. Akaondoka Daudi akaenda pamoja na watu wote waliokuwa naye, mpaka Baala wa Yuda, ili kulipandisha kutoka huko sanduku la Mungu lililoitwa kwa jina, naam, jina la BWANA wa majeshi akaaye juu ya makerubi. Wakaliweka sanduku la Mungu juu ya gari jipya, wakalitoa katika nyumba ya Abinadabu, iliyoko kilimani; nao Uza na Ahio wana wa Abinadabu wakaliendesha lile gari jipya. Wakalitoa katika nyumba ya Abinadabu iliyoko kilimani, pamoja na sanduku la BWANA; na huyo Ahio akatangulia mbele ya sanduku. Daudi na nyumba yote ya Israeli wakacheza mbele za BWANA kwa nguvu zao zote, kwa nyimbo, na kwa vinubi, na kwa vinanda, na kwa matari, na kwa kayamba, na kwa matoazi. Hata walipofika kwenye uga wa Nakoni, Uza akalinyoshea mkono sanduku la Mungu, akalikamata kwa maana wale ng'ombe walijikwaa. Ndipo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Uza; naye Mungu akampiga huko kwa kosa lake; hata akafa pale pale penye sanduku la Mungu. Daudi akaona uchungu kwa kuwa BWANA amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo. Naye Daudi akamwogopa BWANA siku ile; akasema, Litanijiaje sanduku la BWANA? Basi Daudi hakutaka kulileta sanduku la BWANA kwake mjini mwa Daudi; ila Daudi akalihamisha nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku la BWANA akalitia katika nyumba ya Obed-edomu, Mgiti, muda wa miezi mitatu; naye BWANA akambariki Obed-edomu, na nyumba yake yote. Kisha mfalme Daudi akaambiwa ya kwamba, BWANA ameibariki nyumba ya Obed-edomu, na vitu vyote alivyo navyo kwa ajili ya sanduku la Mungu. Daudi akaenda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumba ya Obed-edomu mpaka mji wa Daudi, kwa shangwe. Hata ikawa, watu waliolichukua sanduku la BWANA walipokwisha kwenda hatua sita, akachinja fahali na ndama mnono. Daudi akacheza mbele za BWANA kwa nguvu zake zote; na Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani. Basi Daudi na nyumba yote ya Israeli wakalileta sanduku la BWANA kwa shangwe, na kwa sauti ya tarumbeta.

2 Samueli 6:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Daudi akakusanya tena wateule wote wa Israeli, watu thelathini elfu. Akaondoka Daudi akaenda pamoja na watu wote waliokuwa naye, mpaka Baala wa Yuda, ili kulipandisha kutoka huko sanduku la Mungu lililoitwa kwa jina, naam, jina la BWANA wa majeshi akaaye juu ya makerubi. Wakaliweka sanduku la Mungu juu ya gari jipya, wakalitoa katika nyumba ya Abinadabu, iliyoko kilimani; nao Uza na Ahio wana wa Abinadabu wakaliendesha lile gari jipya. Wakalitoa katika nyumba ya Abinadabu iliyoko kilimani, pamoja na sanduku la BWANA; na huyo Ahio akatangulia mbele ya sanduku. Daudi na nyumba yote ya Israeli wakacheza mbele za BWANA kwa nguvu zao zote, kwa nyimbo, na kwa vinubi, na kwa vinanda, na kwa matari, na kwa kayamba, na kwa matoazi. Hata walipofika kwa uga ya Nakoni, Uza akalinyoshea mkono sanduku la Mungu, akalikamata kwa maana wale ng’ombe walikunguwaa. Ndipo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Uza; naye Mungu akampiga huko kwa kosa lake; hata akafa pale pale penye sanduku la Mungu. Daudi akaona uchungu kwa kuwa BWANA amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo. Naye Daudi akamwogopa BWANA siku ile; akasema, Litanijiaje sanduku la BWANA? Basi Daudi hakutaka kulileta sanduku la BWANA kwake mjini mwa Daudi; ila Daudi akalihamisha nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku la BWANA akalitia katika nyumba ya Obed-edomu, Mgiti, muda wa miezi mitatu; naye BWANA akambarikia Obed-edomu, na nyumba yake yote. Kisha mfalme Daudi akaambiwa ya kwamba, BWANA ameibarikia nyumba ya Obed-edomu, na vitu vyote alivyo navyo kwa ajili ya sanduku la Mungu. Daudi akaenda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumba ya Obed-edomu mpaka mji wa Daudi, kwa shangwe. Hata ikawa, watu waliolichukua sanduku la BWANA walipokwisha kwenda hatua sita, akachinja ng’ombe na kinono. Daudi akacheza mbele za BWANA kwa nguvu zake zote; na Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani. Basi Daudi na nyumba yote ya Israeli wakalileta sanduku la BWANA kwa shangwe, na kwa sauti ya tarumbeta.

2 Samueli 6:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Tena Daudi akakusanya watu 30,000 wa Israeli waliochaguliwa. Yeye na watu wake wote wakatoka Baala ya Yuda kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka huko, linaloitwa kwa Jina, naam, jina la BWANA Mwenye Nguvu Zote, ambaye anaketi katika kiti cha enzi kati ya makerubi walioko juu ya hilo Sanduku. Wakaweka hilo Sanduku la Mungu juu ya gari jipya la kukokotwa na kulileta kutoka nyumba ya Abinadabu, iliyokuwa juu ya kilima. Uza na Ahio, wana wa Abinadabu, walikuwa wakiongoza hilo gari jipya la kukokotwa likiwa na Sanduku la Mungu juu yake, naye Ahio alikuwa anatembea akiwa mbele yake. Daudi na nyumba yote ya Israeli walikuwa wanacheza mbele za BWANA kwa nguvu zao zote, kwa nyimbo, vinubi, zeze, matari, kayamba na matoazi. Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Nakoni, Uza akanyoosha mkono na kulishika Sanduku la Mungu kwa sababu maksai walijikwaa. Hasira ya BWANA ikawaka dhidi ya Uza kwa sababu ya kitendo chake cha kukosa heshima, kwa hiyo Mungu akampiga akafia papo hapo kando ya Sanduku la Mungu. Ndipo Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu ya BWANA ilifurika dhidi ya Uza, hivyo hadi leo mahali hapo panaitwa Peres-Uza. Daudi akamwogopa BWANA siku ile, akasema, “Ni jinsi gani Sanduku la BWANA litakavyoweza kunijia?” Hakuwa radhi kulichukua Sanduku la BWANA kwake katika Mji wa Daudi. Badala yake akalipeleka kwenye nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti. Sanduku la BWANA likabaki katika nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti, kwa miezi mitatu, naye BWANA akambariki pamoja na nyumba yake yote. Kisha Mfalme Daudi akaambiwa, “BWANA ameibariki nyumba ya Obed-Edomu pamoja na kila alicho nacho, kwa sababu ya Sanduku la Mungu.” Basi Daudi akateremka na kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka nyumba ya Obed-Edomu hadi Mji wa Daudi kwa shangwe. Wale waliokuwa wamebeba Sanduku la BWANA walipokuwa wametembea hatua sita, Daudi alitoa dhabihu fahali na ndama aliyenoneshwa. Daudi, akiwa amevaa kisibau cha kitani, alicheza mbele za BWANA kwa nguvu zake zote, wakati yeye na nyumba yote ya Israeli walipopandisha Sanduku la BWANA kwa shangwe na sauti za tarumbeta.