2 Samueli 15:13-23
2 Samueli 15:13-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Mjumbe fulani alipomwendea Daudi na kumwambia, “Watu wa Israeli wamevutwa na Absalomu!” Basi, Daudi akawaambia watumishi wake waliokuwa naye mjini Yerusalemu, “Inukeni tukimbie, la sivyo, hatutaweza kumwepa Absalomu. Tufanye haraka kuondoka asije akatuletea maafa na kuuangamiza mji kwa mapanga.” Lakini watumishi wake wakamwambia, “Sisi watumishi wako, bwana wetu mfalme, tuko tayari kufanya lolote unaloamua.” Basi, mfalme akaondoka pamoja na jamaa yake, lakini akawaacha masuria wake kumi wakishughulika na kazi za nyumbani. Mfalme akaondoka pamoja na watu wake wote. Lakini akatua kidogo walipofikia nyumba ya mwisho mjini. Watumishi wote wa mfalme, Wakerethi wote, Wapelethi wote, pamoja na Wagiti 600 waliomfuata mfalme Daudi kutoka mji wa Gathi, waliondoka pamoja naye wakimtangulia. Kisha, mfalme Daudi alipomwona Itai, Mgiti, alimwambia, “Kwa nini hata wewe umeondoka pamoja nasi? Rudi ukakae na huyo mfalme kijana. Maana wewe ni mgeni huku, tena ni mkimbizi kutoka nyumbani kwenu. Wewe ulikuja huku juzijuzi tu. Je, nikufanye mtu wa kutangatanga pamoja nasi, nikijua kuwa sijui hata kule ninakoenda? Rudi nyumbani pamoja na ndugu zako. Naye Mwenyezi-Mungu akuoneshe fadhili zake na uaminifu.” Lakini Itai akamjibu mfalme, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na wewe bwana wangu mfalme uishivyo, popote utakapokuwa, ikiwa ni kwa kufa au ni kwa kuishi, nami mtumishi wako nitakuwapo.” Basi, Daudi akamwambia Itai, “Nenda basi, endelea mbele.” Hivyo, Itai, Mgiti, akapita yeye mwenyewe pamoja na watoto wake. Daudi alipokuwa akipita pamoja na watu wake, watu wote nchini kote walilia kwa sauti. Mfalme Daudi akavuka kijito cha Kidroni pamoja na watu wote, wakapita kuelekea jangwani.
2 Samueli 15:13-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mjumbe akaja na kumwambia Daudi, “Mioyo ya watu wa Israeli inaambatana na Absalomu.” Ndipo Daudi akawaambia maafisa wake wote waliokuwa pamoja naye huko Yerusalemu, “Njooni! Ni lazima tukimbie, la sivyo hakuna hata mmoja wetu atakayeokoka kutoka mkononi mwa Absalomu. Ni lazima tuondoke kwa haraka, la sivyo atakuja mbio na kutupata, atatuangamiza na kuupiga mji kwa upanga.” Maafisa wa mfalme wakamjibu, “Watumishi wako tu tayari kufanya lolote mfalme bwana wetu analochagua.” Mfalme akatoka, pamoja na watu wa nyumbani mwake wakimfuata; lakini akawaacha masuria kumi ili kuangalia jumba la kifalme. Hivyo mfalme akaondoka, pamoja na watu wote wakimfuata, wakatua mahali mbali kiasi. Watu wake wote wakatembea, wakampita wakiwa wamefuatana na Wakerethi na Wapelethi wote; pia Wagiti wote mia sita waliokuwa wamefuatana naye kutoka Gathi wakapita mbele ya mfalme. Mfalme akamwambia Itai, Mgiti, “Kwa nini ufuatane na sisi? Rudi ukakae pamoja na Mfalme Absalomu. Wewe ni mgeni, mkimbizi kutoka nchini mwako. Ulikuja jana tu. Nami leo nikufanye utangetange pamoja nasi, wakati sijui niendako? Rudi, nawe ukawachukue watu wa kwenu. Wema na uaminifu na viwe pamoja nawe.” Lakini Itai akamjibu mfalme, “Hakika kama BWANA aishivyo na kama mfalme bwana wangu aishivyo, popote mfalme bwana wangu atakapokuwa, ikiwa ni kuishi au kufa, hapo ndipo mtumishi wako atakapokuwa.” Daudi akamwambia Itai, “Songa mbele, endelea.” Kwa hiyo Itai, Mgiti, akaendelea pamoja na watu wake wote, pia jamaa zote waliokuwa pamoja naye. Watu wote wa nje ya mji wakalia kwa sauti wakati watu wote walipokuwa wakipita. Mfalme naye akavuka Bonde la Kidroni, nao watu wote wakaelekea jangwani.
2 Samueli 15:13-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mjumbe akamfikia Daudi, akasema, Mioyo ya watu wa Israeli inashikamana na Absalomu. Basi Daudi akawaambia watumishi wake wote waliokuwa pamoja naye Yerusalemu, Ondokeni, tukakimbie kwa kuwa tusipokimbia hapana mtu miongoni mwetu atakayeokoka mikononi mwa Absalomu; haya! Fanyeni haraka, tuondoke, asitupate kwa upesi, na kutuletea maovu, na kuupiga mji huu kwa makali ya upanga. Hao watumishi wa mfalme wakamwambia mfalme, Angalia, sisi watumishi wako tu tayari kutenda lolote atakalolichagua bwana wetu mfalme. Basi mfalme akatoka na watu wa nyumbani mwake wote wakafuatana naye. Mfalme akaacha wanawake kumi, masuria, ili kuitunza nyumba. Mfalme akatoka, na watu wote wakamfuata; wakakaa kidogo katika Beth-merhaki. Watumishi wake wote wakapita karibu naye; na Wakerethi wote, na Wapelethi wote, na Wagiti wote, watu mia sita walioandamana naye kutoka Gathi, wakapita mbele ya mfalme. Ndipo mfalme akamwambia Itai, Mgiti, Mbona wewe unakwenda pamoja nasi? Rudi, ukakae na mfalme; maana wewe u mgeni, tena u mtu uliyefukuzwa mahali pako mwenyewe. Kwa kuwa umekuja jana tu kwa nini nikusumbue leo, na kukuzungusha huku na huko pamoja nasi nami hapa ninaenda niwezapo kwenda? Rudi wewe, ukawarudishe na ndugu zako; rehema na kweli ziwe pamoja nawe. Naye Itai akamjibu mfalme akasema, Kama aishivyo BWANA, na bwana wangu mfalme aishivyo, hakika yake kila mahali atakapokuwapo mfalme, bwana wangu, ikiwa ni kwa kufa au ikiwa ni kwa kuishi, ndipo atakapokuwapo na mtumishi wako. Basi Daudi akamwambia Itai, Haya, nenda ukavuke. Akavuka Itai, Mgiti na watu wake wote, na watoto wadogo wote waliokuwa pamoja naye. Na nchi yote ikalia kwa sauti kuu, nao watu wote wakavuka, mfalme mwenyewe naye akavuka kile kijito Kidroni, na hao watu wote wakavuka, wakielekea njia ya nyika.
2 Samueli 15:13-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mjumbe akamfikilia Daudi, akasema, Mioyo ya watu wa Israeli inashikamana na Absalomu. Basi Daudi akawaambia watumishi wake wote waliokuwa pamoja naye Yerusalemu, Ondokeni, tukakimbie kwa kuwa tusipokimbia hapana mtu miongoni mwetu atakayeokoka mikononi mwa Absalomu; haya! Fanyeni haraka, tuondoke, asitupate kwa upesi, na kutuletea maovu, na kuupiga mji huu kwa makali ya upanga. Hao watumishi wa mfalme wakamwambia mfalme, Angalia, sisi watumishi wako tu tayari kutenda lo lote atakalolichagua bwana wetu mfalme. Basi mfalme akatoka na watu wa nyumbani mwake wote wakafuatana naye. Mfalme akaacha wanawake kumi, masuria, ili kuitunza nyumba. Mfalme akatoka, na watu wote wakamfuata; wakakaa kidogo katika Beth-merhaki. Watumishi wake wote wakapita karibu naye; na Wakerethi wote, na Wapelethi wote, na Wagiti wote, watu mia sita walioandamana naye kutoka Gathi, wakapita mbele ya mfalme. Ndipo mfalme akamwambia Itai, Mgiti, Mbona wewe unakwenda pamoja nasi? Rudi, ukakae na mfalme; maana wewe u mgeni, tena u mtu uliyefukuzwa mahali pako mwenyewe. Kwa kuwa umekuja jana tu kwa nini nikusumbue leo, na kukuzungusha huko na huko pamoja nasi nami hapa naenda niwezapo kwenda? Rudi wewe, ukawarudishe na ndugu zako; rehema na kweli ziwe pamoja nawe. Naye Itai akamjibu mfalme akasema, Kama aishivyo BWANA, na bwana wangu mfalme aishivyo, hakika yake kila mahali atakapokuwapo mfalme, bwana wangu, ikiwa ni kwa kufa au ikiwa ni kwa kuishi, ndipo atakapokuwapo na mtumwa wako. Basi Daudi akamwambia Itai, Haya, enenda ukavuke. Akavuka Itai, Mgiti na watu wake wote, na watoto wadogo wote waliokuwa pamoja naye. Na nchi yote ikalia kwa sauti kuu, nao watu wote wakavuka, mfalme mwenyewe naye akavuka kile kijito Kidroni, na hao watu wote wakavuka, wakielekea njia ya nyika.