2 Samueli 14:5-11
2 Samueli 14:5-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mfalme akamwambia, “Una shida gani?” Yule mwanamke akajibu, “Nasikitika, mimi ni mjane, mume wangu amekufa. Nilikuwa na watoto wa kiume wawili. Siku moja, walipokuwa mbugani, walianza kugombana. Kwa vile hapakuwa na mtu yeyote wa kuwaamua, mmoja akampiga mwenzake, akamuua. Sasa ndugu zangu wote wamenigeuka mimi mtumishi wako; wanataka nimtoe kwao mtoto aliyemuua mwenzake ili wamuue kwa kuyaangamiza maisha ya ndugu yake. Hivyo, watamuua huyu ambaye sasa ndiye mrithi. Wakifanya hivyo, watazima kabisa tumaini langu lililobakia, na mume wangu hataachiwa jina wala mzawa duniani.” Mfalme akamwambia yule mwanamke, “Rudi nyumbani nitaamuru jambo lako liangaliwe.” Yule mwanamke kutoka Tekoa akasema, “Bwana wangu mfalme, hatia yote na iwe juu yangu na juu ya jamaa ya baba yangu. Hivyo, wewe na ufalme wako msiwe na hatia.” Mfalme akamwambia, “Mtu yeyote akikutishia mlete kwangu na hatakuja kukugusa tena.” Yule mwanamke akamwambia, “Tafadhali, mfalme, niombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ili yule ndugu yangu ambaye angelipiza kisasi cha mauaji ya mwanangu asifanye hatia nyingine kubwa ya kumwua yule mtoto wangu mwingine.” Mfalme Daudi akamwambia, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, hakuna hata unywele mmoja wa mwanao utakaoanguka chini.”
2 Samueli 14:5-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mfalme akamwuliza, Una nini? Naye akajibu, Hakika ni mjane mimi, niliyefiwa na mume wangu. Nami mjakazi wako nilikuwa na wana wawili, na hao wawili wakashindana uwandani, wala hapakuwa na mtu wa kuwaamua, lakini mmoja akampiga mwenzake, akamwua. Na tazama, jamaa yote wameniinukia mimi mjakazi wako, wakasema, Mtoe yule aliyempiga nduguye, ili tupate kumwua yeye kwa maisha ya nduguye aliyemwua, hata na kumwua mrithi pia; ndivyo watakavyolizima kaa langu lililobaki, wasimwachie mume wangu jina wala mabaki usoni pa nchi. Mfalme akamwambia huyo mwanamke, Nenda nyumbani kwako, nami nitakufanyia agizo. Ndipo huyo mwanamke wa Tekoa akamwambia mfalme, Na uwe juu yangu, Ee bwana wangu mfalme, na juu ya nyumba ya baba yangu uovu huu; wala kwa mfalme na kwa kiti chake cha enzi pasiwepo hatia. Mfalme akasema, Yeyote atakaye kuambia neno, mlete kwangu, naye hatakugusa tena. Ndipo akajibu, Nakusihi, mfalme na amkumbuke BWANA, Mungu wako, ili mlipiza kisasi cha damu asizidi kuharibu, wasije kumharibu mwanangu. Naye akasema, Aishivyo BWANA, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa mwanao.
2 Samueli 14:5-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mfalme akamwuliza, Una nini? Naye akajibu, Hakika ni mjane mimi, niliyefiwa na mume wangu. Nami mjakazi wako nalikuwa na wana wawili, na hao wawili wakashindana uwandani, wala hapakuwa na mtu wa kuwaamua, lakini mmoja akampiga mwenzake, akamwua. Na tazama, jamaa yote wameniinukia mimi mjakazi wako, wakasema, Mtoe yule aliyempiga nduguye, ili tupate kumwua yeye kwa maisha ya nduguye aliyemwua, hata na kumfisha mrithi pia; ndivyo watakavyolizima kaa langu lililobaki, wasimwachie mume wangu jina wala masalio usoni pa nchi. Mfalme akamwambia huyo mwanamke, Nenda nyumbani kwako, nami nitakufanyia agizo. Ndipo huyo mwanamke wa Tekoa akamwambia mfalme, Na uwe juu yangu, Ee bwana wangu mfalme, na juu ya nyumba ya baba yangu uovu huu; wala kwa mfalme na kwa kiti chake cha enzi pasiwepo hatia. Mfalme akasema, Ye yote atakaye kuambia neno, mlete kwangu, naye hatakugusa tena. Ndipo akajibu, Nakusihi, mfalme na amkumbuke BWANA, Mungu wako, ili mlipiza kisasi cha damu asizidi kuharibu, wasije kumharibu mwanangu. Naye akasema, Aishivyo BWANA, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa mwanao.
2 Samueli 14:5-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mfalme akamuuliza, “Una shida gani?” Akamwambia, “Mimi ni mjane hasa, mume wangu amekufa. Mimi mtumishi wako nilikuwa na wana wawili. Wakapigana wao kwa wao huko shambani wala huko hapakuwa na mtu hata mmoja wa kuwaamua. Mmoja akampiga mwenzake na kumuua. Sasa ukoo wote umeinuka dhidi ya mtumishi wako, wakisema, ‘Utukabidhi huyo aliyemuua ndugu yake, ili tumuue kwa ajili ya uhai wa ndugu yake ambaye alimuua, nasi hapo tutakuwa tumekatilia mbali na mrithi pia.’ Wakifanya hivyo, watakuwa wamezima tumaini langu lililobaki, mume wangu hataachiwa jina wala mzao katika uso wa dunia.” Mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Nenda nyumbani, nami nitatoa agizo kwa ajili yako.” Lakini huyo mwanamke kutoka Tekoa akamwambia, “Mfalme bwana wangu, lawama na iwe juu yangu na juu ya nyumba ya baba yangu, naye mfalme na kiti chake cha enzi na asiwe na hatia.” Mfalme akajibu, “Ikiwa mtu yeyote atakusemesha lolote, mlete kwangu, naye hatakusumbua tena.” Huyo mwanamke akasema, “Basi mfalme na amwombe BWANA Mungu wake ili kuzuia mlipiza kisasi cha damu kuongeza juu ya uharibifu, ili kwamba mwanangu asije akaangamizwa.” Mfalme akasema, “Hakika kama aishivyo BWANA, hakuna unywele mmoja wa kichwa cha mwanao utakaoanguka chini.”