2 Samueli 14:12-17
2 Samueli 14:12-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Yule mwanamke akamwambia, “Nakuomba, mimi mtumishi wako, uniruhusu niseme neno moja kwako mfalme.” Mfalme akamwambia, “Sema”. Yule mwanamke akamwambia, “Kwa nini basi, umepanga uovu huu dhidi ya watu wa Mungu? Kulingana na uamuzi wako juu ya jambo hilo wewe mwenyewe umejihukumu kuwa na hatia kwa sababu humruhusu mwanao arudi nyumbani kutoka alikokimbilia. Sisi sote lazima tutakufa. Sisi ni kama maji yaliyomwagika chini ambayo hayazoleki. Hata Mungu hafanyi tofauti kwa mtu huyu na tofauti kwa mwingine; yeye hutafuta njia ili waliopigwa marufuku, wakakimbia, wapate kurudi. Mimi nimekuja kuzungumza nawe, bwana wangu mfalme, kwani wamenitisha. Basi, mimi mtumishi wako, niliwaza kuwa, ‘Afadhali nikazungumze na mfalme, huenda akanitimizia mahitaji yangu mimi mtumishi wake. Maana mfalme atanisikiliza na kuniokoa mikononi mwa mtu ambaye anataka kuniangamiza mimi pamoja na mwanangu kutoka urithi wa Mungu’. Nami mjakazi wako nilifikiri kuwa, ‘Neno lake bwana wangu mfalme litanipa amani moyoni, kwani wewe bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kupambanua mema na mabaya.’ Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, awe pamoja nawe.”
2 Samueli 14:12-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwanamke akasema, Mwache mjakazi wako, nakusihi, niseme neno moja kwa bwana wangu mfalme. Akasema, Haya nena. Mwanamke akasema, Kwa nini basi wewe umewafikiria mambo kama hayo watu wa Mungu? Maana kwa kunena neno hili mfalme ni kama mwenye hatia, kwa kuwa hamrudishi kwao tena yule mfukuzwa wake. Kwa kuwa hatuna budi kufa, nasi tu kama maji yaliyomwagika chini, yasiyoweza kuzoleka tena; wala Mungu haondoi maisha ila hufikiri shauri, kwamba yeye aliyefukuzwa asiwe mkimbizi kwake. Hata sasa nilivyokuja mimi kunena neno hili na bwana wangu mfalme, ni kwa sababu watu wamenitisha; nami, mjakazi wako, nikasema, Mimi nitanena sasa kwa mfalme; labda itakuwa mfalme atanifanyia haja yangu mimi mtumishi wake. Kwa kuwa mfalme atasikia, ili amwokoe mtumishi wake mkononi mwa yule mtu atakaye kuniharibu mimi na mwanangu pia katika urithi wa Mungu. Ndipo mimi mjakazi wako nikasema, Neno la bwana wangu mfalme na liwe la kustarehesha; kwa kuwa kama malaika wa Mungu ndivyo alivyo bwana wangu mfalme, kuyapambanua yaliyo mema na yaliyo mabaya; naye BWANA, Mungu wako na awe pamoja nawe.
2 Samueli 14:12-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwanamke akasema, Mwache mjakazi wako, nakusihi, niseme neno moja kwa bwana wangu mfalme. Akasema, Haya nena. Mwanamke akasema, Kwa nini basi wewe umewafikiria mambo kama hayo watu wa Mungu? Kwani kwa kunena neno hili mfalme ni kama mwenye hatia, kwa kuwa mfalme hamleti kwao tena yule mfukuzwa wake. Kwa kuwa hatuna budi kufa, nasi tu kama maji yaliyomwagika chini, yasiyowezekana kuzoleka tena; wala Mungu haondoi maisha ila hufikiri shauri, kwamba yeye aliyefukuzwa asiwe mkimbizi kwake. Hata sasa nilivyokuja mimi kunena neno hili na bwana wangu mfalme, ni kwa sababu watu wamenitisha; nami, mjakazi wako, nikasema, Mimi nitanena sasa kwa mfalme; labda itakuwa mfalme atanifanyia haja yangu mimi mtumwa wake. Kwa kuwa mfalme atasikia, ili amwokoe mtumwa wake mkononi mwa yule mtu atakaye kuniharibu mimi na mwanangu pia katika urithi wa Mungu. Ndipo mimi mjakazi wako nikasema, Neno la bwana wangu mfalme na liwe la kustarehesha; kwa kuwa kama malaika wa Mungu ndivyo alivyo bwana wangu mfalme, kuyapambanua yaliyo mema na yaliyo mabaya; naye BWANA, Mungu wako na awe pamoja nawe.
2 Samueli 14:12-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo huyo mwanamke akasema, “Mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa mfalme bwana wangu.” Mfalme akajibu, “Sema.” Huyo mwanamke akasema, “Mbona basi wewe umewaza jambo kama hili dhidi ya watu wa Mungu? Je, mfalme asemapo hili, hajitii hatiani mwenyewe, kwa maana mfalme hajamrudisha mwanawe aliyefukuziwa mbali? Kama vile maji yaliyomwagika ardhini, yasivyoweza kuzoleka tena, hivyo sisi kufa ni lazima. Lakini Mungu haondoi uhai, badala yake, yeye hufanya njia ili kwamba aliyefukuzwa asibaki akiwa amefarikishwa naye. “Nami sasa nimekuja kusema hili kwa bwana wangu mfalme kwa sababu watu wameniogopesha. Mtumishi wako alifikiri, ‘Nitanena na mfalme, labda mfalme atamfanyia mtumishi wake kile anachoomba. Labda mfalme atakubali kumwokoa mtumishi wake kutoka mkononi mwa mtu anayejaribu kunikatilia mbali, mimi na mwanangu, kutoka kwenye urithi Mungu aliotupatia.’ “Basi sasa mtumishi wako anasema, ‘Neno la bwana wangu mfalme na linipatie pumziko, kwa maana bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kutambua jema na baya. BWANA Mungu wako na awe pamoja nawe.’ ”