2 Samueli 14:1-33
2 Samueli 14:1-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Yoabu, mwana wa Seruya, akatambua ya kuwa moyo wa mfalme unamwelekea Absalomu. Yoabu akatuma watu waende Tekoa, akaleta kutoka huko mwanamke mwenye akili, akamwambia, Nakusihi, ujifanye kama unakaa matanga, ukavae nguo za kufiwa, nakusihi, wala usijitie mafuta, ila ukafanane na mwanamke aliyeomboleza siku nyingi kwa ajili yake aliyefariki; kisha uingie kwa mfalme ukamwambie maneno haya. Hivyo Yoabu akamtia maneno kinywani. Naye yule mwanamke wa Tekoa aliponena na mfalme, akaanguka kifulifuli chini, akamsujudia, akasema, Nisaidie, Ee mfalme. Mfalme akamwuliza, Una nini? Naye akajibu, Hakika ni mjane mimi, niliyefiwa na mume wangu. Nami mjakazi wako nalikuwa na wana wawili, na hao wawili wakashindana uwandani, wala hapakuwa na mtu wa kuwaamua, lakini mmoja akampiga mwenzake, akamwua. Na tazama, jamaa yote wameniinukia mimi mjakazi wako, wakasema, Mtoe yule aliyempiga nduguye, ili tupate kumwua yeye kwa maisha ya nduguye aliyemwua, hata na kumfisha mrithi pia; ndivyo watakavyolizima kaa langu lililobaki, wasimwachie mume wangu jina wala masalio usoni pa nchi. Mfalme akamwambia huyo mwanamke, Nenda nyumbani kwako, nami nitakufanyia agizo. Ndipo huyo mwanamke wa Tekoa akamwambia mfalme, Na uwe juu yangu, Ee bwana wangu mfalme, na juu ya nyumba ya baba yangu uovu huu; wala kwa mfalme na kwa kiti chake cha enzi pasiwepo hatia. Mfalme akasema, Ye yote atakaye kuambia neno, mlete kwangu, naye hatakugusa tena. Ndipo akajibu, Nakusihi, mfalme na amkumbuke BWANA, Mungu wako, ili mlipiza kisasi cha damu asizidi kuharibu, wasije kumharibu mwanangu. Naye akasema, Aishivyo BWANA, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa mwanao. Mwanamke akasema, Mwache mjakazi wako, nakusihi, niseme neno moja kwa bwana wangu mfalme. Akasema, Haya nena. Mwanamke akasema, Kwa nini basi wewe umewafikiria mambo kama hayo watu wa Mungu? Kwani kwa kunena neno hili mfalme ni kama mwenye hatia, kwa kuwa mfalme hamleti kwao tena yule mfukuzwa wake. Kwa kuwa hatuna budi kufa, nasi tu kama maji yaliyomwagika chini, yasiyowezekana kuzoleka tena; wala Mungu haondoi maisha ila hufikiri shauri, kwamba yeye aliyefukuzwa asiwe mkimbizi kwake. Hata sasa nilivyokuja mimi kunena neno hili na bwana wangu mfalme, ni kwa sababu watu wamenitisha; nami, mjakazi wako, nikasema, Mimi nitanena sasa kwa mfalme; labda itakuwa mfalme atanifanyia haja yangu mimi mtumwa wake. Kwa kuwa mfalme atasikia, ili amwokoe mtumwa wake mkononi mwa yule mtu atakaye kuniharibu mimi na mwanangu pia katika urithi wa Mungu. Ndipo mimi mjakazi wako nikasema, Neno la bwana wangu mfalme na liwe la kustarehesha; kwa kuwa kama malaika wa Mungu ndivyo alivyo bwana wangu mfalme, kuyapambanua yaliyo mema na yaliyo mabaya; naye BWANA, Mungu wako na awe pamoja nawe. Ndipo mfalme akajibu, akamwambia yule mwanamke, usinifiche, nakusihi, neno lo lote nitakalokuuliza. Na mwanamke akasema, Na anene sasa bwana wangu mfalme. Mfalme akasema, Je! Si mkono wa Yoabu ulio pamoja nawe katika haya yote? Mwanamke akajibu, akasema, Kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mfalme, hapana mtu awezaye kugeuka kwa kuume, au kwa kushoto, kukana neno lo lote alilolisema bwana wangu mfalme; kwani mtumwa wako Yoabu ndiye aliyeniamuru, na kuyaweka maneno haya yote kinywani mwa mjakazi wako; mtumwa wako Yoabu ameyatenda haya ili kubadili uso wa jambo hili; na bwana wangu anayo akili, kama akili ya malaika wa Mungu, hata ajue mambo yote ya duniani. Basi mfalme akamwambia Yoabu, Angalia sasa, nimekata shauri hili; nenda, ukamrudishe tena yule kijana Absalomu. Naye Yoabu akaanguka kifulifuli hata nchi, akasujudu, akambariki mfalme, Yoabu akasema, Leo mimi mtumwa wako najua ya kwamba nimepata neema machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa kuwa mfalme amemfanyia mtumwa wake haja yake. Basi Yoabu akaondoka, akaenda Geshuri, akamleta Absalomu Yerusalemu. Naye mfalme akasema, Ageukie nyumbani kwake, asinione uso wangu. Basi Absalomu akarejea nyumbani kwake, asimwone uso mfalme. Basi katika Israeli wote hapakuwa na mtu hata mmoja mwenye kusifiwa kwa uzuri wake kama huyo Absalomu; tangu nyayo za miguu yake hata utosi wa kichwa chake hapakuwa na ila kwake. Naye aliponyoa kichwa, (basi mwisho wa kila mwaka hunyoa; na kwa sababu nywele zilikuwa nzito kwake, kwa hiyo akanyoa;) hupima nywele za kichwa chake shekeli mia mbili kwa uzani wa mfalme. Kisha wakazaliwa kwake Absalomu wana watatu na binti mmoja, ambaye jina lake aliitwa Tamari; naye alikuwa mwanamke mzuri wa uso. Absalomu akakaa miaka miwili mizima katika Yerusalemu; asimwone uso mfalme. Ndipo Absalomu akatuma kumwita Yoabu, ampeleke kwa mfalme, lakini yeye akakataa kumjia; akatuma tena mara ya pili, lakini akakataa kuja. Kwa hiyo akawaambia watumishi wake, Tazameni, shamba la Yoabu liko karibu na shamba langu, naye ana shayiri huko; nendeni mkalitie moto. Basi watumishi wa Absalomu wakalitia moto lile shamba. Ndipo akaondoka Yoabu, akamwendea Absalomu nyumbani kwake, akamwambia, Kwa nini watumishi wako wamelitia moto shamba langu? Absalomu akamjibu Yoabu, Angalia, nilituma kwako, kusema, Njoo kwangu, ili nikupeleke kwa mfalme kunena, Mbona nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa heri kwangu kama ningekuwako huko hata sasa; basi sasa na nimtazame uso mfalme; na ukiwapo uovu kwangu, na aniue. Basi Yoabu akamwendea mfalme, akamwambia hayo, naye alipomwita Absalomu, yeye akaja kwa mfalme, akainama kifulifuli hata nchi mbele ya mfalme; naye mfalme akambusu Absalomu.
2 Samueli 14:1-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Yoabu mwana wa Seruya, alitambua kwamba maelekeo ya moyo wa Daudi yalikuwa kwa Absalomu tu. Hivyo alituma watu huko Tekoa ili wamtafutie mwanamke mwenye hekima. Walipomleta, akamwambia, “Jisingizie unafanya matanga. Vaa nguo za kuomboleza, usijipake mafuta, ila ujifanye kama mwanamke ambaye amekuwa katika maombolezo ya wafu kwa muda mrefu. Halafu nenda kwa mfalme ukamwambie yale ninayokuambia.” Kisha Yoabu akamwambia maneno ya kumwambia mfalme. Huyo mwanamke kutoka Tekoa akaenda kwa mfalme, akaanguka kifudifudi, mbele ya mfalme, akasujudu, akamwambia, “Ee mfalme, nisaidie.” Mfalme akamwambia, “Una shida gani?” Yule mwanamke akajibu, “Nasikitika, mimi ni mjane, mume wangu amekufa. Nilikuwa na watoto wa kiume wawili. Siku moja, walipokuwa mbugani, walianza kugombana. Kwa vile hapakuwa na mtu yeyote wa kuwaamua, mmoja akampiga mwenzake, akamuua. Sasa ndugu zangu wote wamenigeuka mimi mtumishi wako; wanataka nimtoe kwao mtoto aliyemuua mwenzake ili wamuue kwa kuyaangamiza maisha ya ndugu yake. Hivyo, watamuua huyu ambaye sasa ndiye mrithi. Wakifanya hivyo, watazima kabisa tumaini langu lililobakia, na mume wangu hataachiwa jina wala mzawa duniani.” Mfalme akamwambia yule mwanamke, “Rudi nyumbani nitaamuru jambo lako liangaliwe.” Yule mwanamke kutoka Tekoa akasema, “Bwana wangu mfalme, hatia yote na iwe juu yangu na juu ya jamaa ya baba yangu. Hivyo, wewe na ufalme wako msiwe na hatia.” Mfalme akamwambia, “Mtu yeyote akikutishia mlete kwangu na hatakuja kukugusa tena.” Yule mwanamke akamwambia, “Tafadhali, mfalme, niombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ili yule ndugu yangu ambaye angelipiza kisasi cha mauaji ya mwanangu asifanye hatia nyingine kubwa ya kumwua yule mtoto wangu mwingine.” Mfalme Daudi akamwambia, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, hakuna hata unywele mmoja wa mwanao utakaoanguka chini.” Yule mwanamke akamwambia, “Nakuomba, mimi mtumishi wako, uniruhusu niseme neno moja kwako mfalme.” Mfalme akamwambia, “Sema”. Yule mwanamke akamwambia, “Kwa nini basi, umepanga uovu huu dhidi ya watu wa Mungu? Kulingana na uamuzi wako juu ya jambo hilo wewe mwenyewe umejihukumu kuwa na hatia kwa sababu humruhusu mwanao arudi nyumbani kutoka alikokimbilia. Sisi sote lazima tutakufa. Sisi ni kama maji yaliyomwagika chini ambayo hayazoleki. Hata Mungu hafanyi tofauti kwa mtu huyu na tofauti kwa mwingine; yeye hutafuta njia ili waliopigwa marufuku, wakakimbia, wapate kurudi. Mimi nimekuja kuzungumza nawe, bwana wangu mfalme, kwani wamenitisha. Basi, mimi mtumishi wako, niliwaza kuwa, ‘Afadhali nikazungumze na mfalme, huenda akanitimizia mahitaji yangu mimi mtumishi wake. Maana mfalme atanisikiliza na kuniokoa mikononi mwa mtu ambaye anataka kuniangamiza mimi pamoja na mwanangu kutoka urithi wa Mungu’. Nami mjakazi wako nilifikiri kuwa, ‘Neno lake bwana wangu mfalme litanipa amani moyoni, kwani wewe bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kupambanua mema na mabaya.’ Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, awe pamoja nawe.” Ndipo mfalme alipomjibu yule mwanamke, “Usinifiche jambo lolote nitakalokuuliza.” Yule mwanamke akasema, “Sema bwana wangu mfalme.” Mfalme akamwuliza, “Je, Yoabu anahusika katika jambo hili?” Yule mwanamke akasema, “Kama uishivyo, bwana wangu mfalme, mtu hawezi kukwepa kulia au kushoto kuhusu jambo ulilosema bwana wangu mfalme. Yoabu yule mtumishi wako ndiye aliyenituma. Ni yeye aliyeniambia maneno yote haya niliyokuambia mimi mtumishi wako. Yoabu alifanya hivyo ili kubadilisha mambo. Lakini, wewe bwana wangu, una hekima kama ya malaika wa Mungu hata unaweza kujua mambo yote yaliyoko duniani.” Kisha, mfalme akamwambia Yoabu, “Sasa sikiliza, natoa kibali changu ili umrudishe nyumbani yule kijana Absalomu.” Yoabu alianguka chini kifudifudi, akasujudu na kumtakia mfalme baraka, akasema, “Leo, mimi mtumishi wako, bwana wangu mfalme, ninajua kuwa nimepata kibali mbele yako, kwa kulikubali ombi langu.” Hivyo, Yoabu aliondoka, akaenda Geshuri kumleta Absalomu mjini Yerusalemu. Lakini mfalme akasema, “Absalomu aishi mbali nami; aishi nyumbani kwake. Asije hapa kuniona.” Hivyo, Absalomu akawa anaishi mbali, nyumbani kwake na hakumwona mfalme Daudi. Katika Israeli yote, hakuna yeyote aliyesifiwa kwa uzuri kama Absalomu. Tangu nyayo zake hadi utosini mwake, Absalomu hakuwa na kasoro yoyote. Kila alipokata nywele zake, (na kila mwishoni mwa mwaka alikata nywele zake kwani zilikuwa nzito), alipozipima, zilikuwa na uzito wa kilo mbili kulingana na vipimo vya kifalme. Absalomu alizaa watoto watatu wa kiume pamoja na binti mmoja jina lake Tamari. Tamari alikuwa mwanamke mzuri. Basi, Absalomu aliishi mjini Yerusalemu kwa muda wa miaka miwili mizima bila kumwona mfalme Daudi. Kisha, Absalomu alimtumia ujumbe Yoabu, ili aende kwa mfalme kwa niaba yake, lakini Yoabu akakataa. Absalomu akatuma ujumbe mara ya pili lakini Yoabu akakataa. Basi, Absalomu akawaambia watumishi wake, “Angalieni Yoabu ana shamba la shayiri karibu na langu. Nendeni mkalichome moto.” Kwa hiyo watumishi wa Absalomu wakalichoma moto shamba la Yoabu. Yoabu akaenda nyumbani kwa Absalomu akamwuliza, “Kwa nini watumishi wako wamechoma moto shamba langu?” Absalomu akamjibu, “Tazama, nilikupelekea ujumbe, uje huku ili nikutume kwa mfalme, ukamwulize: ‘Kwa nini niliondoka Geshuri? Ingekuwa bora kwangu kubaki huko’. Sasa nisaidie nipate kumwona mfalme. Kama nina hatia basi, na aniue!” Kwa hiyo Yoabu akaenda na kumweleza mfalme maneno hayo yote, naye akamwita Absalomu, naye akaingia kwa mfalme, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme. Na mfalme akambusu Absalomu.
2 Samueli 14:1-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Yoabu, mwana wa Seruya, akatambua ya kuwa moyo wa mfalme unamwelekea Absalomu. Yoabu akatuma watu waende Tekoa, akaleta kutoka huko mwanamke mwenye akili, akamwambia, Nakusihi, ujifanye kama unaomboleza, ukavae nguo za kufiwa, nakusihi, wala usijitie mafuta, ila ukafanane na mwanamke aliyeomboleza siku nyingi kwa ajili yake aliyefariki; kisha uingie kwa mfalme ukamwambie maneno haya. Hivyo Yoabu akamtia maneno kinywani. Naye yule mwanamke wa Tekoa aliponena na mfalme, akaanguka kifudifudi chini, akamsujudia, akasema, Nisaidie, Ee mfalme. Mfalme akamwuliza, Una nini? Naye akajibu, Hakika ni mjane mimi, niliyefiwa na mume wangu. Nami mjakazi wako nilikuwa na wana wawili, na hao wawili wakashindana uwandani, wala hapakuwa na mtu wa kuwaamua, lakini mmoja akampiga mwenzake, akamwua. Na tazama, jamaa yote wameniinukia mimi mjakazi wako, wakasema, Mtoe yule aliyempiga nduguye, ili tupate kumwua yeye kwa maisha ya nduguye aliyemwua, hata na kumwua mrithi pia; ndivyo watakavyolizima kaa langu lililobaki, wasimwachie mume wangu jina wala mabaki usoni pa nchi. Mfalme akamwambia huyo mwanamke, Nenda nyumbani kwako, nami nitakufanyia agizo. Ndipo huyo mwanamke wa Tekoa akamwambia mfalme, Na uwe juu yangu, Ee bwana wangu mfalme, na juu ya nyumba ya baba yangu uovu huu; wala kwa mfalme na kwa kiti chake cha enzi pasiwepo hatia. Mfalme akasema, Yeyote atakaye kuambia neno, mlete kwangu, naye hatakugusa tena. Ndipo akajibu, Nakusihi, mfalme na amkumbuke BWANA, Mungu wako, ili mlipiza kisasi cha damu asizidi kuharibu, wasije kumharibu mwanangu. Naye akasema, Aishivyo BWANA, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa mwanao. Mwanamke akasema, Mwache mjakazi wako, nakusihi, niseme neno moja kwa bwana wangu mfalme. Akasema, Haya nena. Mwanamke akasema, Kwa nini basi wewe umewafikiria mambo kama hayo watu wa Mungu? Maana kwa kunena neno hili mfalme ni kama mwenye hatia, kwa kuwa hamrudishi kwao tena yule mfukuzwa wake. Kwa kuwa hatuna budi kufa, nasi tu kama maji yaliyomwagika chini, yasiyoweza kuzoleka tena; wala Mungu haondoi maisha ila hufikiri shauri, kwamba yeye aliyefukuzwa asiwe mkimbizi kwake. Hata sasa nilivyokuja mimi kunena neno hili na bwana wangu mfalme, ni kwa sababu watu wamenitisha; nami, mjakazi wako, nikasema, Mimi nitanena sasa kwa mfalme; labda itakuwa mfalme atanifanyia haja yangu mimi mtumishi wake. Kwa kuwa mfalme atasikia, ili amwokoe mtumishi wake mkononi mwa yule mtu atakaye kuniharibu mimi na mwanangu pia katika urithi wa Mungu. Ndipo mimi mjakazi wako nikasema, Neno la bwana wangu mfalme na liwe la kustarehesha; kwa kuwa kama malaika wa Mungu ndivyo alivyo bwana wangu mfalme, kuyapambanua yaliyo mema na yaliyo mabaya; naye BWANA, Mungu wako na awe pamoja nawe. Ndipo mfalme akajibu, akamwambia yule mwanamke, usinifiche, nakusihi, neno lolote nitakalokuuliza. Na mwanamke akasema, Na anene sasa bwana wangu mfalme. Mfalme akasema, Je! Si mkono wa Yoabu ulio pamoja nawe katika haya yote? Mwanamke akajibu, akasema, Kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mfalme, hapana mtu awezaye kugeuka kwa kulia, au kwa kushoto, kukana neno lolote alilolisema bwana wangu mfalme; kwani mtumishi wako Yoabu ndiye aliyeniamuru, na kuyaweka maneno haya yote kinywani mwa mjakazi wako; mtumishi wako Yoabu ameyatenda haya ili kubadili uso wa jambo hili; na bwana wangu anayo akili, kama akili ya malaika wa Mungu, hata ajue mambo yote ya duniani. Basi mfalme akamwambia Yoabu, Angalia sasa, nimekata shauri hili; nenda, ukamrudishe tena yule kijana Absalomu. Naye Yoabu akaanguka kifudifudi hadi chini, akasujudu, akambariki mfalme, Yoabu akasema, Leo mimi mtumwa wako ninajua ya kwamba nimepata neema machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa kuwa mfalme amemfanyia mtumishi wake haja yake. Basi Yoabu akaondoka, akaenda Geshuri, akamleta Absalomu Yerusalemu. Naye mfalme akasema, Ageukie nyumbani kwake, asinione uso wangu. Basi Absalomu akarejea nyumbani kwake, asimwone uso mfalme. Basi katika Israeli wote hapakuwa na mtu hata mmoja mwenye kusifiwa kwa uzuri wake kama huyo Absalomu; tangu nyayo za miguu yake hadi utosi wa kichwa chake hapakuwa na ila kwake. Naye aliponyoa kichwa, (basi mwisho wa kila mwaka hunyoa; na kwa sababu nywele zilikuwa nzito kwake, kwa hiyo akanyoa;) hupima nywele za kichwa chake shekeli mia mbili kwa uzani wa mfalme. Kisha wakazaliwa kwake Absalomu wana watatu na binti mmoja, ambaye jina lake aliitwa Tamari; naye alikuwa mwanamke mzuri wa uso. Absalomu akakaa miaka miwili mizima katika Yerusalemu; asimwone uso mfalme. Ndipo Absalomu akatuma Yoabu aitwe, amtume kwa mfalme, lakini yeye akakataa kumjia; akatuma tena mara ya pili, lakini akakataa kuja. Kwa hiyo akawaambia watumishi wake, Tazameni, shamba la Yoabu liko karibu na shamba langu, naye ana shayiri huko; nendeni mkalitie moto. Basi watumishi wa Absalomu wakalitia moto lile shamba. Ndipo akaondoka Yoabu, akamwendea Absalomu nyumbani kwake, akamwambia, Kwa nini watumishi wako wamelitia moto shamba langu? Absalomu akamjibu Yoabu, Angalia, nilituma kwako, nikisema, Njoo kwangu, ili nikutume kwa mfalme kunena, Mbona nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa heri kwangu kama ningekuwako huko hata sasa; basi sasa na nimtazame uso mfalme; na ukiwapo uovu kwangu, na aniue. Basi Yoabu akamwendea mfalme, akamwambia hayo, naye alipomwita Absalomu, yeye akaja kwa mfalme, akainama kifudifudi hadi chini mbele ya mfalme; naye mfalme akambusu Absalomu.
2 Samueli 14:1-33 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yoabu mwana wa Seruya akafahamu kuwa moyo wa mfalme ulikuwa na shauku ya kumwona Absalomu. Kwa hiyo Yoabu akamtuma mtu fulani kwenda Tekoa na kumleta mwanamke mwenye hekima kutoka huko. Akamwambia huyo mwanamke, “Jifanye uko katika maombolezo. Vaa nguo za kuomboleza, nawe usitumie mafuta yoyote ya uzuri, jifanye kama mwanamke ambaye amekuwa na huzuni kwa siku nyingi kwa ajili ya kufiwa. Kisha nenda kwa mfalme ukazungumze maneno haya.” Naye Yoabu akaweka maneno kinywani mwa yule mwanamke. Huyo huyo mwanamke kutoka Tekoa alipofika kwa mfalme, akaanguka kifudifudi kumpa mfalme heshima, akasema, “Ee mfalme, nisaidie!” Mfalme akamuuliza, “Una shida gani?” Akamwambia, “Mimi ni mjane hasa, mume wangu amekufa. Mimi mtumishi wako nilikuwa na wana wawili. Wakapigana wao kwa wao huko shambani wala huko hapakuwa na mtu hata mmoja wa kuwaamua. Mmoja akampiga mwenzake na kumuua. Sasa ukoo wote umeinuka dhidi ya mtumishi wako, wakisema, ‘Utukabidhi huyo aliyemuua ndugu yake, ili tumuue kwa ajili ya uhai wa ndugu yake ambaye alimuua, nasi hapo tutakuwa tumekatilia mbali na mrithi pia.’ Wakifanya hivyo, watakuwa wamezima tumaini langu lililobaki, mume wangu hataachiwa jina wala mzao katika uso wa dunia.” Mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Nenda nyumbani, nami nitatoa agizo kwa ajili yako.” Lakini huyo mwanamke kutoka Tekoa akamwambia, “Mfalme bwana wangu, lawama na iwe juu yangu na juu ya nyumba ya baba yangu, naye mfalme na kiti chake cha enzi na asiwe na hatia.” Mfalme akajibu, “Ikiwa mtu yeyote atakusemesha lolote, mlete kwangu, naye hatakusumbua tena.” Huyo mwanamke akasema, “Basi mfalme na amwombe BWANA Mungu wake ili kuzuia mlipiza kisasi cha damu kuongeza juu ya uharibifu, ili kwamba mwanangu asije akaangamizwa.” Mfalme akasema, “Hakika kama aishivyo BWANA, hakuna unywele mmoja wa kichwa cha mwanao utakaoanguka chini.” Ndipo huyo mwanamke akasema, “Mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa mfalme bwana wangu.” Mfalme akajibu, “Sema.” Huyo mwanamke akasema, “Mbona basi wewe umewaza jambo kama hili dhidi ya watu wa Mungu? Je, mfalme asemapo hili, hajitii hatiani mwenyewe, kwa maana mfalme hajamrudisha mwanawe aliyefukuziwa mbali? Kama vile maji yaliyomwagika ardhini, yasivyoweza kuzoleka tena, hivyo sisi kufa ni lazima. Lakini Mungu haondoi uhai, badala yake, yeye hufanya njia ili kwamba aliyefukuzwa asibaki akiwa amefarikishwa naye. “Nami sasa nimekuja kusema hili kwa bwana wangu mfalme kwa sababu watu wameniogopesha. Mtumishi wako alifikiri, ‘Nitanena na mfalme, labda mfalme atamfanyia mtumishi wake kile anachoomba. Labda mfalme atakubali kumwokoa mtumishi wake kutoka mkononi mwa mtu anayejaribu kunikatilia mbali, mimi na mwanangu, kutoka kwenye urithi Mungu aliotupatia.’ “Basi sasa mtumishi wako anasema, ‘Neno la bwana wangu mfalme na linipatie pumziko, kwa maana bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kutambua jema na baya. BWANA Mungu wako na awe pamoja nawe.’ ” Basi mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Usinifiche jibu kuhusu hilo nitakalokuuliza.” Huyo mwanamke akasema, “Mfalme bwana wangu na aseme.” Mfalme akauliza, “Je, mkono wa Yoabu haupo pamoja nawe katika jambo hilo lote?” Huyo mwanamke akajibu, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu mfalme, hakuna yeyote anayeweza kugeuka kulia wala kushoto kutokana na chochote anachosema bwana wangu mfalme. Naam, ni mtumishi wako Yoabu ndiye alinifundisha kufanya hivi, naye ndiye aliweka maneno haya yote kinywani mwa mtumishi wako. Mtumishi wako Yoabu amefanya hivi ili kubadili hali iliyopo. Bwana wangu ana hekima kama ile ya malaika wa Mungu, hufahamu kila kitu kinachotokea katika nchi.” Mfalme akamwambia Yoabu, “Vyema sana, nitalifanya jambo hili. Nenda, ukamlete kijana Absalomu.” Yoabu akaanguka kifudifudi mpaka ardhini kumpa mfalme heshima, naye akambariki mfalme. Yoabu akasema, “Leo mtumishi wako anajua kuwa amepata kibali machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa sababu mfalme amemjalia mtumishi wake ombi lake.” Ndipo Yoabu akaenda hadi Geshuri akamrudisha Absalomu Yerusalemu. Lakini mfalme akasema, “Lazima Absalomu aende kwenye nyumba yake mwenyewe; kamwe asiuone uso wangu.” Kwa hiyo Absalomu akaenda kwenye nyumba yake na hakuuona uso wa mfalme. Katika Israeli yote hakuna mtu yeyote aliyesifiwa kwa uzuri wa sura kama Absalomu. Kuanzia utosi wa kichwa chake hadi wayo wa mguu wake hapakuwa na kasoro. Kila mara aliponyoa nywele za kichwa chake, kwa kuwa alikuwa akinyoa mara kwa mara zilipokuwa zinamwia nzito, alizipima uzito wake ulikuwa shekeli mia mbili kwa kipimo cha kifalme. Walizaliwa wana watatu na binti mmoja kwa Absalomu. Jina la binti yake aliitwa Tamari, naye akawa mwanamke mzuri wa sura. Absalomu akaishi miaka miwili huko Yerusalemu pasipo kuuona uso wa mfalme. Basi Absalomu akamwita Yoabu kwa kusudi la kumtuma kwa mfalme, lakini Yoabu akakataa kuja kwa Absalomu. Ndipo akamwita tena mara ya pili, lakini pia akakataa kuja. Ndipo akawaambia watumishi wake, “Tazama, shamba la Yoabu liko jirani na langu, naye ana shayiri humo. Nendeni mkalitie moto.” Kisha watumishi wa Absalomu wakalitia moto shamba hilo. Basi Yoabu akaenda nyumbani kwa Absalomu, akamwambia, “Kwa nini watumishi wako wametia moto shamba langu?” Absalomu akamwambia Yoabu, “Tazama, nilikutumia ujumbe na kusema, ‘Njoo ili niweze kukutuma kwa mfalme kuuliza, “Kwa nini nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa bora zaidi kwangu kama ningebaki huko!” ’ Sasa basi, nataka kuuona uso wa mfalme, na ikiwa nina hatia ya jambo lolote, basi na aniue.” Basi Yoabu akaenda kwa mfalme na kumwambia jambo hili. Kisha mfalme akamwita Absalomu, naye akaingia ndani akasujudu uso wake mpaka ardhini mbele ya mfalme. Naye mfalme akambusu Absalomu.