2 Petro 3:14-18
2 Petro 3:14-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake. Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa; vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe. Basi, wapenzi mkitangulia kujua hayo, jilindeni nafsi zenu, msije mkachukuliwa na kosa la hao wahalifu mkaanguka na kuuacha uthibitifu wenu. Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele.
2 Petro 3:14-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa hiyo wapenzi wangu, mkiwa mnaingojea siku ile, fanyeni bidii kuwa safi kabisa bila hatia mbele ya Mungu, na kuwa na amani naye. Mnapaswa kuuona uvumilivu wa Bwana kuwa ni nafasi anayowapeni mpate kuokolewa, kama Paulo ndugu yetu mpenzi alivyowaandikia akitumia hekima aliyopewa na Mungu. Hayo ndiyo asemayo katika barua zake zote anapozungumzia suala hilo. Yapo mambo kadhaa katika barua zake yaliyo magumu kuyaelewa, mambo ambayo watu wajinga, wasio na msimamo, huyapotosha kama wanavyopotosha sehemu nyingine za Maandiko Matakatifu. Hivyo wanasababisha maangamizi yao wenyewe. Lakini nyinyi, wapenzi wangu, mmekwisha jua jambo hili. Basi, muwe na tahadhari msije mkapotoshwa na makosa ya waasi, mkaanguka kutoka katika msimamo wenu imara. Lakini endeleeni kukua katika neema na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu uwe kwake, sasa na hata milele! Amina.
2 Petro 3:14-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa hiyo, wapenzi, mnapoyangojea mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane mkiwa na amani, bila doa wala dosari mbele yake. Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa; akisema juu ya mambo haya kama afanyavyo katika barua zake zote pia, katika barua hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuyaelewa na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wapotoavyo Maandiko mengine, na kujiletea maangamizi wao wenyewe. Basi, wapenzi kwa kuwa mmejua hayo, jihadharini msije mkapotoshwa na kosa la hao wahalifu mkaanguka na kuuacha uthabiti wenu. Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele.
2 Petro 3:14-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa sababu hii, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo haya, fanyeni bidii ili awakute katika amani, bila mawaa wala dosari. Hesabuni uvumilivu wa Bwana kuwa ni wokovu, kama vile ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima ile aliyopewa na Mungu. Huandika vivyo hivyo katika nyaraka zake zote, akizungumzia ndani yake mambo haya. Katika nyaraka zake kuna mambo mengine ambayo ni vigumu kuyaelewa, ambayo watu wajinga na wasio thabiti huyapotosha kwa maangamizi yao wenyewe, kama wapotoshavyo pia Maandiko mengine. Basi, ninyi wapenzi, kwa kuwa mmekwisha kujua mambo haya, jilindeni msije mkachukuliwa na kosa la watu hao waasi na kuanguka kutoka kwenye uthabiti wenu. Bali kueni katika neema na katika kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na milele! Amen.