2 Petro 3:1-10
2 Petro 3:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Wapenzi wangu, hii ni barua ya pili ninayowaandikia. Katika barua hizo mbili nimejaribu kufufua fikira safi akilini mwenu kwa kuwakumbusheni mambo haya. Napenda mkumbuke maneno yaliyosemwa na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi mliyopewa na mitume wenu. Awali ya yote jueni kwamba siku za mwisho watakuja watu ambao mienendo yao inatawaliwa na tamaa zao mbaya. Watawadhihaki nyinyi na kusema: “Aliahidi kwamba atakuja! Je, sasa yuko wapi? Mambo ni yaleyale tangu babu zetu walipokufa; hali ya vitu ni ileile kama ilivyokuwa mwanzo wa ulimwengu!” Watu hao, kwa makusudi, husahau kwamba zamani Mungu alinena, nazo mbingu na dunia zikaumbwa. Dunia iliumbwa kutoka katika maji na kwa maji; na kwa maji hayo, yaani yale maji ya gharika kuu, dunia ya wakati ule iliangamizwa. Lakini mbingu na dunia ya sasa zahifadhiwa kwa neno la Mungu kwa ajili ya kuharibiwa kwa moto. Zimewekwa kwa ajili ya siku ile ambapo watu wasiomcha Mungu watahukumiwa na kuangamizwa. Lakini, wapenzi wangu, msisahau kitu kimoja! Mbele ya Bwana, hakuna tofauti kati ya siku moja na miaka elfu; kwake yote ni mamoja. Bwana hakawii kutimiza yale aliyoahidi kama watu wengine wanavyofikiri kuwa atakawia. Yeye ana saburi kwa ajili yenu, maana hapendi hata mmoja wenu apotee, bali huwavuta wote wapate kutubu. Siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Siku hiyo, mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; vitu vyake vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia itatoweka pamoja na kila kitu kilichomo ndani yake.
2 Petro 3:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wapenzi, waraka huu ndio wa pili niwaandikiao ninyi; katika zote mbili naziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha, mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu. Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe, na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa. Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu; kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia. Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu. Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyodhani anakawia, bali huwavumilia, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikie toba. Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.
2 Petro 3:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wapenzi, waraka huu ndio wa pili niwaandikiao ninyi; katika zote mbili naziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha, mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu. Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe, na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa. Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu; kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia. Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu. Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba. Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.
2 Petro 3:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wapenzi, huu ndio waraka wangu wa pili ninaowaandikia. Katika nyaraka hizi mbili ninajaribu kuziamsha nia zenu safi kwa mawazo makamilifu. Nataka ninyi mkumbuke maneno yaliyosemwa zamani na manabii watakatifu na ile amri ya Bwana na Mwokozi mliyopewa kupitia kwa mitume wenu. Kwanza kabisa, ni lazima mfahamu ya kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka, wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbaya. Watasema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipofariki, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.” Lakini wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, ya kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwepo tangu zamani, nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa maji. Ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa kwa hayo maji na kuangamizwa. Lakini kwa neno lilo hilo, mbingu za sasa na dunia zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu. Lakini wapenzi, msisahau neno hili: kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba. Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilichomo ndani yake kitaunguzwa.