2 Petro 2:4-11
2 Petro 2:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Malaika walipotenda dhambi, Mungu hakuwahurumia, bali aliwatupa katika moto wa Jehanamu ambako wamefungwa wakingojea siku ile ya hukumu. Mungu hakuihurumia dunia ya hapo kale, bali alileta gharika kuu juu ya nchi ile ya watu wasiomcha Mungu; lakini Noa ambaye alihubiri uadilifu, Mungu alimwokoa pamoja na watu wengine saba. Mungu aliiadhibu miji ya Sodoma na Gomora, akaiteketeza kwa moto, akaifanya iwe mfano wa mambo yatakayowapata watu wasiomcha Mungu. Alimwokoa Loti, mtu mwema, ambaye alisikitishwa sana na mwenendo mbaya wa watu hao waasi. Loti aliishi miongoni mwa watu hao, na kwa siku nyingi moyo wake ulikuwa katika wasiwasi mkuu aliposikia matendo yao maovu. Kwa hiyo, basi, Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa katika majaribu watu wanaomcha Mungu, na jinsi ya kuwaweka waovu katika adhabu hadi siku ile ya hukumu, hasa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kupuuza mamlaka. Watu hao ni wakaidi na wenye majivuno, huvitukana na hawaviheshimu viumbe vitukufu vya juu. Lakini malaika ambao wana uwezo na nguvu kuliko hao waalimu wa uongo, hawawashtaki na kuwatukana hao mbele ya Bwana.
2 Petro 2:4-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu; wala hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu; tena akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya; akamwokoa Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu; maana mtu huyu mwenye haki akikaa kati yao, kwa kuona na kusikia, alijitesa roho yake yenye haki, siku baada ya siku, kwa matendo yao yasiyo na sheria; basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu; na hasa wale waufuatao mwili katika tamaa ya mambo machafu, na kudharau mamlaka. Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matukufu; ijapokuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti mashitaka mabaya juu yao mbele za Bwana.
2 Petro 2:4-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu; wala hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu; tena akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya; akamwokoa Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu; maana mtu huyu mwenye haki akikaa kati yao, kwa kuona na kusikia, alijitesa roho yake yenye haki, siku baada ya siku, kwa matendo yao yasiyo na sheria; basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu; na hasa wale waufuatao mwili katika tamaa ya mambo machafu. na kudharau mamlaka. Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matukufu; ijapokuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti mashitaka mabaya juu yao mbele za Bwana.
2 Petro 2:4-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa maana, kama Mungu hakuwasamehe malaika walipotenda dhambi, bali aliwatupa kuzimu katika vifungo vya giza wakae humo mpaka ije hukumu; kama hakuusamehe ulimwengu wa kale alipoleta gharika juu ya watu wale wasiomcha Mungu, bali akamhifadhi Noa, mhubiri wa haki, pamoja na watu wengine saba; kama aliihukumu miji ya Sodoma na Gomora kwa kuiteketeza kwa moto ikawa majivu, na kuifanya kuwa kielelezo kwa yale yatakayowapata wale wasiomcha Mungu; na kama alimwokoa Loti, mtu mwenye haki, ambaye alihuzunishwa na maisha machafu ya watu wapotovu (kwa sababu yale matendo mapotovu aliyoyaona na kuyasikia huyo mtu mwenye haki alipoishi miongoni mwao yalimhuzunisha siku baada ya siku): ikiwa hivyo ndivyo, basi Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa wamchao Mungu kutoka majaribu, na kuwaweka waasi katika adhabu hadi siku ya hukumu. Hii ni hakika hasa kwa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kudharau mamlaka. Kwa ushupavu na kwa kiburi, watu hawa hawaogopi kunena mabaya dhidi ya viumbe vya mbinguni. Lakini hata malaika, ingawa wana nguvu na uwezo zaidi, hawaleti mashtaka mabaya dhidi ya viumbe kama hao mbele za Bwana.