Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Petro 2:1-22

2 Petro 2:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Lakini kulitokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia. Na wengi watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa. Na kwa tamaa yao watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; wao ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala maangamizi yao hayasinzii. Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu; wala hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu; tena akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya; akamwokoa Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu; maana mtu huyu mwenye haki akikaa kati yao, kwa kuona na kusikia, alijitesa roho yake yenye haki, siku baada ya siku, kwa matendo yao yasiyo na sheria; basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu; na hasa wale waufuatao mwili katika tamaa ya mambo machafu, na kudharau mamlaka. Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matukufu; ijapokuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti mashitaka mabaya juu yao mbele za Bwana. Lakini hao kama wanyama wasio na akili, ambao walizaliwa kama wanyama tu wa kukamatwa na kupotezwa, wakikufuru katika mambo wasiyoyajua, wataangamizwa katika maangamizo yao; Wakipatikana na madhara, ambayo ni ujira wa udhalimu wao, wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa; wamekuwa ni mawaa na aibu wakifuata anasa zisizo kiasi katika karamu zao za upendo, wafanyapo karamu pamoja nanyi; wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana; wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu; lakini alikaripiwa kwa uhalifu wake mwenyewe; punda, asiyeweza kusema, akinena kwa sauti ya kibinadamu, aliuzuia wazimu wa nabii yule. Hawa ni visima visivyo na maji, na mawingu yachukuliwayo na tufani, ambao weusi wa giza ni akiba waliyowekewa. Maana wakinena maneno makuu mno ya kiburi, kwa tamaa za mwili na kwa ufisadi huwahadaa watu walioanza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu; wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu, maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule. Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa. Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaagaa matopeni.

Shirikisha
Soma 2 Petro 2

2 Petro 2:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Palitokea manabii wa uongo kati ya watu, na vivyo hivyo waalimu wa uongo watatokea kati yenu. Watu hao wataingiza mafundisho maharibifu na kumkana Bwana aliyewakomboa, na kwa njia hiyo watasababisha ghafla maangamizi yao wenyewe. Tena watu wengi watazifuata hizo njia zao mbaya, na kwa sababu yao wengine wataipuuza njia ya ukweli. Kwa tamaa yao mbaya watajipatia faida kwa kuwaambieni hadithi za uongo. Lakini kwa muda mrefu sasa Hakimu wao yuko tayari, na Mwangamizi wao yuko macho! Malaika walipotenda dhambi, Mungu hakuwahurumia, bali aliwatupa katika moto wa Jehanamu ambako wamefungwa wakingojea siku ile ya hukumu. Mungu hakuihurumia dunia ya hapo kale, bali alileta gharika kuu juu ya nchi ile ya watu wasiomcha Mungu; lakini Noa ambaye alihubiri uadilifu, Mungu alimwokoa pamoja na watu wengine saba. Mungu aliiadhibu miji ya Sodoma na Gomora, akaiteketeza kwa moto, akaifanya iwe mfano wa mambo yatakayowapata watu wasiomcha Mungu. Alimwokoa Loti, mtu mwema, ambaye alisikitishwa sana na mwenendo mbaya wa watu hao waasi. Loti aliishi miongoni mwa watu hao, na kwa siku nyingi moyo wake ulikuwa katika wasiwasi mkuu aliposikia matendo yao maovu. Kwa hiyo, basi, Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa katika majaribu watu wanaomcha Mungu, na jinsi ya kuwaweka waovu katika adhabu hadi siku ile ya hukumu, hasa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kupuuza mamlaka. Watu hao ni wakaidi na wenye majivuno, huvitukana na hawaviheshimu viumbe vitukufu vya juu. Lakini malaika ambao wana uwezo na nguvu kuliko hao waalimu wa uongo, hawawashtaki na kuwatukana hao mbele ya Bwana. Watu hao ambao hutukana chochote kile wasichoelewa, ni sawa na wanyama wasio na akili ambao huzaliwa na baadaye hukamatwa na kuchinjwa! Wataangamizwa kutokana na uharibifu wao wenyewe, na watalipwa mateso kwa mateso ambayo wameyasababisha. Furaha yao ni kufanya, tena mchana kabisa, chochote kinachotosheleza anasa zao za mwili. Hao ni fedheha na aibu tupu kwa jumuiya yenu wakati wanapojiunga nanyi katika karamu zenu, hali wakifurahia njia zao za udanganyifu. Macho yao yamejaa uzinzi na uwezo wao wa kutenda dhambi hauna kikomo. Huwaongoza watu walio dhaifu mpaka mitegoni. Mioyo yao imezoea kuwa na tamaa ya mali. Wapo chini ya laana ya Mungu! Wameiacha njia iliyonyoka, wakapotoka na kuifuata njia aliyofuata Balaamu, mwana wa Beori ambaye alipendelea kupata faida kwa kufanya udanganyifu, akakaripiwa kwa ajili ya uovu wake. Punda ambaye hasemi, alinena kwa sauti ya binadamu, akaukomesha wazimu wa huyo nabii. Watu hao ni kama chemchemi zilizokauka, kama mawingu yanayopeperushwa na tufani; makao yao waliyowekewa ni mahali pa giza kuu. Husema maneno ya majivuno na yasiyo na maana, na kutumia tamaa zao mbaya za kimwili kuwatega wale ambao wamejitenga hivi karibuni na watu waishio katika udanganyifu. Huwaahidi watu wengine eti watakuwa huru, kumbe wao wenyewe ni watumwa wa upotovu – maana mtu ni mtumwa wa chochote kile kinachomtawala. Watu waliokwisha ponyoka katika upotovu wa ulimwengu kwa kupata kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, kisha wakakubali kunaswa na kutawaliwa tena na upotovu huo, hali yao itakuwa mbaya zaidi kuliko awali. Ingalikuwa afadhali kwao kama wasingalijua kamwe njia hiyo ya uadilifu kuliko kuijua na kisha kuiacha na kupoteza amri takatifu waliyopokea. Ipo methali isemayo: “Mbwa huyarudia matapishi yake mwenyewe,” na nyingine isemayo: “Nguruwe aliyekwisha oshwa hugaagaa tena katika matope!” Ndivyo ilivyo kwao sasa.

Shirikisha
Soma 2 Petro 2

2 Petro 2:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia. Na wengi watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa. Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii. Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu; wala hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu; tena akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya; akamwokoa Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu; maana mtu huyu mwenye haki akikaa kati yao, kwa kuona na kusikia, alijitesa roho yake yenye haki, siku baada ya siku, kwa matendo yao yasiyo na sheria; basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu; na hasa wale waufuatao mwili katika tamaa ya mambo machafu. na kudharau mamlaka. Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matukufu; ijapokuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti mashitaka mabaya juu yao mbele za Bwana. Lakini hao kama wanyama wasio na akili, ambao walizaliwa kama wanyama tu wa kukamatwa na kupotezwa, wakikufuru katika mambo wasiyoyajua, wataangamizwa katika maangamizo yao; Wakipatikana na madhara, ambayo ni ujira wa udhalimu wao, wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa; wamekuwa ni mawaa na aibu wakifuata anasa zisizo kiasi katika karamu zao za upendo, wafanyapo karamu pamoja nanyi; wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana; wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu; lakini alikaripiwa kwa uhalifu wake mwenyewe; punda, asiyeweza kusema, akinena kwa sauti ya kibinadamu, aliuzuia wazimu wa nabii yule. Hawa ni visima visivyo na maji, na mawingu yachukuliwayo na tufani, ambao weusi wa giza ni akiba waliyowekewa. Maana wakinena maneno makuu mno ya kiburi, kwa tamaa za mwili na kwa ufisadi huwahadaa watu walioanza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu; wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu, maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule. Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa. Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni.

Shirikisha
Soma 2 Petro 2

2 Petro 2:1-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama vile watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu. Wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli kwa siri, hata kumkana Bwana wa pekee aliyewanunua, na hivyo kujiletea wenyewe maangamizi ya haraka. Hata hivyo, wengi watafuata njia zao za ufisadi, na kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa. Nao katika tamaa zao mbaya, walimu hawa watajipatia faida kwenu kwa hadithi walizotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, wala uangamivu wao haujalala usingizi. Kwa maana, kama Mungu hakuwasamehe malaika walipotenda dhambi, bali aliwatupa kuzimu katika vifungo vya giza wakae humo mpaka ije hukumu; kama hakuusamehe ulimwengu wa kale alipoleta gharika juu ya watu wale wasiomcha Mungu, bali akamhifadhi Noa, mhubiri wa haki, pamoja na watu wengine saba; kama aliihukumu miji ya Sodoma na Gomora kwa kuiteketeza kwa moto ikawa majivu, na kuifanya kuwa kielelezo kwa yale yatakayowapata wale wasiomcha Mungu; na kama alimwokoa Loti, mtu mwenye haki, ambaye alihuzunishwa na maisha machafu ya watu wapotovu (kwa sababu yale matendo mapotovu aliyoyaona na kuyasikia huyo mtu mwenye haki alipoishi miongoni mwao yalimhuzunisha siku baada ya siku): ikiwa hivyo ndivyo, basi Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa wamchao Mungu kutoka majaribu, na kuwaweka waasi katika adhabu hadi siku ya hukumu. Hii ni hakika hasa kwa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kudharau mamlaka. Kwa ushupavu na kwa kiburi, watu hawa hawaogopi kunena mabaya dhidi ya viumbe vya mbinguni. Lakini hata malaika, ingawa wana nguvu na uwezo zaidi, hawaleti mashtaka mabaya dhidi ya viumbe kama hao mbele za Bwana. Lakini watu hawa hukufuru katika mambo wasiyoyafahamu. Wao ni kama wanyama wasio na akili, viumbe wanaotawaliwa na hisia za mwili, waliozaliwa ili wakamatwe na kuchinjwa. Hawa nao kama wanyama wataangamizwa pia. Watalipwa madhara kwa ajili ya madhara waliyowatendea wengine. Huhesabu kuwa ni fahari kufanya karamu za ulevi na ulafi mchana peupe. Wao ni mawaa na dosari, wakijifurahisha katika anasa zao wanaposhiriki katika karamu zenu. Wakiwa na macho yaliyojaa uzinzi, kamwe hawaachi kutenda dhambi. Huwashawishi wale wasio imara. Wao ni hodari kwa kutamani; ni wana wa laana! Wameiacha njia iliyonyooka, wakapotoka na kuifuata njia ya Balaamu mwana wa Beori aliyependa mshahara wa uovu. Lakini kwa ajili ya uovu wake, alikemewa na punda, mnyama asiyejua kusema, akaongea akitumia sauti ya mwanadamu na kuzuia wazimu wa huyo nabii. Watu hawa ni chemchemi zisizo na maji, na ukungu upeperushwao na tufani. Giza nene limewekwa tayari kwa ajili yao. Kwa maana wao hunena maneno makuu mno ya kiburi cha bure, na kwa kuvutia tamaa mbaya za asili ya mwili, huwashawishi watu ambao ndipo tu wamejiondoa miongoni mwa wale wanaoishi katika ufisadi. Huwaahidi uhuru hao waliowanasa, wakati wao wenyewe ni watumwa wa ufisadi: kwa maana mtu ni mtumwa wa kitu chochote kinachomtawala. Kama wameukimbia upotovu wa dunia kwa kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo, kisha wakanaswa tena humo na kushindwa, hali yao ya mwisho ni mbaya zaidi kuliko ile ya kwanza. Ingelikuwa afadhali kwao kama wasingeliijua kamwe njia ya haki, kuliko kuijua kisha wakaiacha ile amri takatifu waliyokabidhiwa. Imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli isemayo: “Mbwa huyarudia matapiko yake mwenyewe,” tena, “Nguruwe aliyeoshwa hurudi kugaagaa matopeni.”

Shirikisha
Soma 2 Petro 2

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha