2 Petro 1:3-8
2 Petro 1:3-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe. Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na kuishiriki hali yake ya kimungu. Kwa sababu hiyo, fanyeni bidii ya kuongeza imani yenu kwa fadhila, fadhila yenu kwa elimu, elimu yenu kwa kuwa na kiasi, kuwa na kiasi kwa uvumilivu, uvumilivu wenu kwa uchaji wa Mungu, uchaji wenu kwa urafiki wa kindugu, na urafiki wenu wa kindugu kwa mapendo. Mkiwa na sifa hizo zote kwa wingi, zitawawezesheni kuwa watendaji na kupata faida katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
2 Petro 1:3-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa kutoka kwa uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa. Naam, na kwa sababu iyo hiyo jitahidini sana ili katika imani yenu mtie na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu subira, na katika subira yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
2 Petro 1:3-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa. Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
2 Petro 1:3-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Uweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Kwa sababu hiyo, ametukirimia ahadi zake kuu na za thamani kupitia mambo haya, ili kupitia hayo mpate kuwa washiriki wa asili ya uungu, na kuokoka kutoka upotovu ulioko duniani unaosababishwa na tamaa mbaya. Kwa sababu hii hasa, jitahidini sana katika imani yenu kuongeza wema; na katika wema, maarifa; katika maarifa, kiasi; katika kiasi, saburi; katika saburi, utauwa; katika utauwa, upendano wa ndugu; na katika upendano wa ndugu, upendo. Kwa maana haya yakiwa ndani yenu kwa wingi na kuzidi kuongezeka, yanawasaidia msikose bidii wala kutozaa matunda katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.