2 Wafalme 7:1-20
2 Wafalme 7:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Elisha akasema, Lisikieni neno la BWANA; BWANA asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria. Basi yule afisa, ambaye mfalme alikuwa akitegemea mkono wake, akamjibu yule mtu wa Mungu, akasema, Tazama, kama BWANA angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akamwambia, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula. Basi walikuwapo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe? Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vile vile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu. Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kambi ya Washami, kumbe! Hapakuwa na mtu. Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi. Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi wao, na punda zao, na kambi yao vile vile kama ilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao. Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha. Ndipo wakaambiana, Mambo haya tufanyayo si mema; leo ni siku ya habari njema, na sisi tunanyamaza; mkingoja hata kutakapopambazuka, madhara yatatupata; basi twende tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme. Basi wakaenda, wakawaita mabawabu wa mji; wakawaambia, Tulifika kituo cha Washami, na tazama, hapana mtu yeyote huko, wala sauti ya mtu, ila farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na hema zao kama walivyoziacha. Na mabawabu wakaita wakawaambia watu wa nyumba ya mfalme. Mfalme akaondoka usiku, akawaambia watumishi wake, Sasa nitawaonesha ninyi walivyotutendea Washami. Wanajua ya kuwa tuna njaa; basi wametoka kituoni, ili kujificha shambani, wakisema Watakapotoka mjini, tutawakamata hai; tena tutapata kuingia mjini. Na mmojawapo wa watumishi wake akajibu, akasema, Kunradhi; baadhi ya watu na watwae farasi watano katika hao waliosalia, waliobaki ndani ya mji (tazama wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli waliobaki ndani yake; tazama, wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli walioangamia), tukawapeleke tukaone. Basi wakatwaa magari mawili na farasi wake; mfalme akawatuma kuwafuata Washami, akasema, Nendeni, mkaangalie. Wakawafuata mpaka Yordani; na kumbe! Njia yote ilikuwa imejaa mavazi na vyombo, walivyovitupa Washami, wapate kukimbia upesi. Watu wale waliotumwa wakarudi, wakamwambia mfalme. Basi watu wakatoka, wakaziteka nyara hema za Washami. Ikawa kipimo cha unga mzuri kikauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, sawasawa na neno la BWANA. Naye mfalme akamweka yule ofisa mlinzi, ambaye alitegemea mkono wake, awasimamie watu langoni; na watu wakamkanyaga langoni, akafa; kama alivyosema yule mtu wa Mungu, aliyenena hapo mfalme alipomshukia. Ikatukia kama vile yule mtu wa Mungu alivyomwambia mfalme, Vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, na kipimo cha unga mzuri kwa shekeli, ndivyo vitakavyokuwa kesho, panapo saa hii, katika lango la Samaria; na yule kiongozi akamjibu mtu wa Mungu, akasema, Sasa tazama, kama BWANA angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akasema, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula. Ikampata vivyo hivyo, kwa kuwa watu wakamkanyaga langoni, akafa.
2 Wafalme 7:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Elisha akasema, Lisikieni neno la BWANA; BWANA asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria. Basi yule akida, ambaye mfalme alikuwa akitegemea mkono wake, akamjibu yule mtu wa Mungu, akasema, Tazama, kama BWANA angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akamwambia, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula. Basi walikuwapo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe? Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vile vile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu. Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hapana mtu. Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi. Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vile vile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao. Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha. Ndipo wakaambiana, Mambo haya tufanyayo si mema; leo ni siku ya habari njema, na sisi tunanyamaza; mkingoja hata kutakapopambazuka, madhara yatatupata; basi twende tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme. Basi wakaenda, wakawaita mabawabu wa mji; wakawaambia, Tulifika kituo cha Washami, na tazama, hapana mtu ye yote huko, wala sauti ya mtu, ila farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na hema zao kama walivyoziacha. Na mabawabu wakaita wakawaambia watu wa nyumba ya mfalme. Mfalme akaondoka usiku, akawaambia watumishi wake, Sasa nitawaonyesha ninyi walivyotutendea Washami. Wanajua ya kuwa tuna njaa; basi wametoka kituoni, ili kujificha kondeni, wakisema Watakapotoka mjini, tutawakamata hai; tena tutapata kuingia mjini. Na mmojawapo wa watumishi wake akajibu, akasema, Kunradhi; baadhi ya watu na watwae farasi watano katika hao waliosalia, waliobaki ndani ya mji (tazama wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli waliobaki ndani yake; tazama, wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli walioangamia), tukawapeleke tukaone. Basi wakatwaa magari mawili na farasi zake; mfalme akawatuma kuwafuata Washami, akasema, Enendeni, mkaangalie. Wakawafuata mpaka Yordani; na kumbe! Njia yote ilikuwa imejaa mavazi na vyombo, walivyovitupa Washami, wapate kukimbia upesi. Watu wale waliotumwa wakarudi, wakamwambia mfalme. Basi watu wakatoka, wakaziteka nyara hema za Washami. Ikawa kipimo cha unga mzuri kikauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, sawasawa na neno la BWANA. Naye mfalme akamweka yule akida, ambaye alitegemea mkono wake, awasimamie watu langoni; na watu wakamkanyaga langoni, akafa; kama alivyosema yule mtu wa Mungu, aliyenena hapo mfalme alipomshukia. Ikatukia kama vile yule mtu wa Mungu alivyomwambia mfalme, Vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, na kipimo cha unga mzuri kwa shekeli, ndivyo vitakavyokuwa kesho, panapo saa hii, katika lango la Samaria; na yule akida akamjibu mtu wa Mungu, akasema, Sasa tazama, kama BWANA angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akasema, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula. Ikampata vivyo hivyo, kwa kuwa watu wakamkanyaga langoni, akafa.
2 Wafalme 7:1-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Elisha akasema, “Sikiliza neno la BWANA. Hivi ndivyo asemavyo BWANA: Wakati kama huu kesho, kipimo kimoja cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli moja ya fedha, na vibaba viwili vya shayiri kwa shekeli moja ya fedha katika lango la Samaria.” Yule afisa ambaye mfalme alikuwa anauegemea mkono wake akamwambia yule mtu wa Mungu, “Tazama, hata kama BWANA atafungua madirisha ya mbinguni, je, jambo hili litawezekana?” Elisha akajibu, “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini wewe hutakula chochote kati ya hivyo!” Basi kulikuwepo na watu wanne wenye ukoma katika ingilio la lango la mji. Wakaambiana, “Kwa nini tukae hapa mpaka tufe? Kama tukisema, ‘Tutaingia mjini,’ mjini kuna njaa, nasi tutakufa humo. Kama tukikaa hapa, tutakufa. Kwa hiyo twende kwenye kambi ya Waaramu na tujisalimishe. Kama wakituacha hai, tutaishi; kama wakituua, basi na tufe.” Wakati wa giza la jioni, wakaondoka na kwenda kwenye kambi ya Waaramu. Walipofika mwanzo wa kambi, hapakuwa na mtu, kwa kuwa Bwana alilifanya jeshi la Waaramu lisikie sauti kama ya magari ya vita, farasi na jeshi kubwa, kiasi kwamba waliambiana, “Tazama, mfalme wa Israeli ameajiri mfalme wa Wahiti na mfalme wa Wamisri kuja kutushambulia sisi!” Kwa hiyo wakaondoka na kukimbia wakati wa giza la jioni na kuacha mahema yao, farasi wao na punda wao. Wakakimbia kuokoa maisha yao na kuacha kila kitu ndani ya kambi kama kilivyokuwa. Wale watu wenye ukoma walipofika mwanzoni mwa kambi, wakaingia kwenye mojawapo ya mahema. Wakala na kunywa, na kuchukua fedha, dhahabu na nguo, wakaenda kuvificha. Wakarudi na kuingia katika hema jingine, na kuchukua baadhi ya vitu kutoka ndani yake na kuvificha pia. Kisha wakaambiana, “Hili tunalolifanya sio jema. Hii ni siku ya habari njema, nasi tunakaa kimya. Kama tukisubiri mpaka mapambazuko, maafa yatatupata. Twendeni mara moja tukatoe habari hizi katika jumba la mfalme.” Hivyo wakaenda mjini na kuwaita walinzi wa langoni, wakawaambia, “Tulikwenda katika kambi ya Waaramu lakini hapakuwepo na mtu huko, hata sauti ya mtu yeyote, ila farasi na punda waliofungwa na mahema yaliyoachwa kama yalivyokuwa.” Walinzi wa langoni wakatangaza habari ile kwa sauti kuu, na taarifa hii ikatolewa ndani ya jumba la mfalme. Mfalme akaamka usiku na kuwaambia maafisa wake, “Nitawaambia kile Waaramu walichotufanyia. Wanajua kwamba tuna njaa, hivyo wameacha kambi yao ili kujificha mashambani, wakifikiri, ‘Kwa hakika watatoka nje ya mji, nasi tutawakamata wakiwa hai na kuingia ndani ya mji.’ ” Mmoja wa maafisa wake akajibu, “Waamuru watu wachache wakawachukue farasi watano kati ya wale waliobaki katika mji. Hatima yao itakuwa kama ya Waisraeli wote walio hapa. Watakuwa tu kama Waisraeli hawa ambao wanangoja kifo. Hivyo tuwatumeni wajue kumetendeka nini.” Ndipo wakachagua magari mawili ya vita pamoja na farasi wake, naye mfalme akawatuma wafuatilie jeshi la Waaramu. Akawaamuru waendeshaji akisema, “Nendeni mkaone ni nini kilichotokea.” Wakawafuatia hadi Yordani, nao wakakuta barabara yote ikiwa imetapakaa nguo na vyombo vya Waaramu walivyokuwa wamevitupa walipokuwa wanatoroka. Basi wale wajumbe wakarudi na kutoa taarifa kwa mfalme. Kisha watu wakatoka na kuteka nyara kambi ya Waaramu. Kwa hiyo kipimo cha unga mzuri kikauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, kama vile BWANA alivyokuwa amesema. Basi mfalme alikuwa amemweka yule afisa ambaye mfalme alikuwa anauegemea mkono wake awe msimamizi wa lango. Nao watu wakamkanyaga walipoingia langoni, naye akafa, kama vile mtu wa Mungu alivyokuwa ametangulia kusema wakati mfalme alipofika nyumbani kwake. Ikatokea kama vile mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia mfalme: “Wakati kama huu kesho, kipimo kimoja cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli moja ya fedha, na vibaba viwili vya shayiri kwa shekeli moja ya fedha katika lango la Samaria.” Yule afisa alikuwa amemwambia yule mtu wa Mungu, “Tazama, hata kama BWANA atafungua madirisha ya mbinguni, je, jambo hili litawezekana?” Naye yule mtu wa Mungu alikuwa amemjibu, “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini wewe hutakula chochote kati ya hivyo!” Ndivyo hasa ilivyotokea kwake, kwa kuwa watu walimkanyaga langoni, naye akafa.
2 Wafalme 7:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Elisha akamjibu, “Sikiliza neno la Mwenyezi-Mungu: Kesho wakati kama huu, humu Samaria kilo tatu za unga bora wa ngano zitagharimu fedha shekeli moja ya fedha, na kilo sita za shayiri kadhalika zitagharimu fedha shekeli moja.” Kapteni mwaminifu wa mfalme akamwambia Elisha, “Kama Mwenyezi-Mungu mwenyewe angefanya madirisha mbinguni, je, jambo hilo litawezekana!” Elisha akamjibu, “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini wewe hutakula.” Kulikuwa na watu wanne wenye ugonjwa wa ukoma waliokuwa nje ya milango ya mji wa Samaria ambao walisemezana, wao kwa wao, “Mbona tunakaa hapa tukifa njaa? Hakuna maana ya kuingia mjini kwa sababu huko tutakufa. Kwa hiyo hebu twende kwenye kambi ya Waaramu; inawezekana wakatuua, au wasituue.” Hivyo, giza lilipoanza kuingia, wakaenda kwenye kambi ya Waaramu, lakini walipofika huko, hapakuwa na mtu. Maana Mwenyezi-Mungu alilifanya jeshi la Waaramu lisikie sauti kama ya jeshi kubwa lililokuwa na magari na farasi. Waaramu wakadhani kuwa mfalme wa Israeli amekodisha majeshi ya Wahiti na Wamisri kuja kuwashambulia. Basi, katika usiku huo, Waaramu walikimbia wote ili kuyaokoa maisha yao wakiacha mahema yao, farasi na punda wao, na hata kambi yao jinsi ilivyokuwa. Wakoma wale wanne walipofika pembeni mwa kambi, waliingia ndani ya hema moja, wakala na kunywa vile walivyopata humo, wakachukua fedha, dhahabu na nguo, wakaenda kuzificha. Wakaingia katika hema nyingine na kufanya vivyo hivyo. Lakini wakaambiana, “Tunalofanya si sawa! Hii ni habari njema tuliyo nayo leo, na ikiwa tutangoja mpaka asubuhi, bila shaka tutaadhibiwa. Twende mara moja tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme!” Hivyo, wakaondoka katika kambi ya Waaramu na kuwaita mabawabu wa mji na kuwaambia: “Tulikwenda katika kambi ya Waaramu na hatukuweza kumwona wala kumsikia mtu yeyote. Farasi na punda wangali wamefungwa, na mahema yako kama walivyoyaacha.” Walinda malango wakaeneza habari hizi mpaka zikafika nyumbani kwa mfalme. Ingawa kulikuwa bado giza, mfalme aliamka na kuwaambia maofisa wake, “Mimi najua mpango wa Waaramu! Wanajua tuna njaa mjini, sasa wameacha kambi yao kwenda kujificha ili tutakapokwenda kutafuta chakula, watukamate sote hai na kuuteka mji.” Mmoja kati ya maofisa wake akasema, “Watu wengi tayari wameangamia kama vile wale ambao wamekwisha fariki. Tafadhali utume watu wachache na farasi watano wa wale waliobaki ili waende kuona kumetokea nini.” Wakachagua watu na kuwapa magari mawili. Mfalme akawatuma kuwafuata Waaramu, akisema, “Nendeni mkaone.” Watu hao wakaenda mpaka Yordani na njiani waliona nguo na vifaa vingine Waaramu walivyoacha walipokuwa wanakimbia. Wakarudi na kumpasha mfalme habari. Watu wa Samaria wakatoka na kuteka nyara kambi ya Waaramu. Kama vile Mwenyezi-Mungu alivyosema: Kilo tano za unga safi wa ngano au kilo kumi za shayiri ziliuzwa kwa kipande kimoja cha fedha. Naye mfalme alikuwa amemweka ofisa mlinzi wake kulinda lango la mji. Ofisa huyo alikanyagwa papo hapo langoni na kuuawa na watu, kama vile Elisha mtu wa Mungu alivyotabiri wakati mfalme alipokwenda kumwona. Elisha alikuwa amemwambia mfalme kwamba wakati kama huo siku iliyofuata, kilo tano za unga mzuri wa ngano au kilo kumi za shayiri zingeuzwa kwa kipande kimoja cha fedha; lakini hapo awali kapteni alikuwa amembishia Elisha, akisema, “Kama Mwenyezi-Mungu mwenyewe angefanya madirisha mbinguni, je, jambo hili lingewezekana?” Naye Elisha alikuwa amemjibu, “Utaona yakitendeka, lakini chakula chenyewe hutakila.” Na hivyo ndivyo ilivyotokea – kapteni akafa kwa kukanyagwa na watu kwenye lango la mji.