Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 6:8-23

2 Wafalme 6:8-23 Biblia Habari Njema (BHN)

Wakati mmoja kulikuwa na hali ya vita kati ya Aramu na Israeli. Basi, mfalme wa Aramu akashauriana na maofisa wake kuhusu mahali watakaposhambulia. Lakini Elisha akampelekea habari mfalme wa Israeli ajihadhari na mahali hapo, kwa kuwa Waaramu walikuwa tayari kupashambulia. Basi, mfalme wa Israeli akapeleka askari wake karibu na mahali alipoambiwa. Elisha aliendelea kumwonya mfalme naye mfalme alijiweka katika hali ya tahadhari. Jambo hilo lilifanyika mara nyingi. Mfalme wa Aramu akafadhaishwa sana na hali hiyo; akawaita maofisa wake, akawauliza, “Niambieni nani kati yenu anayetusaliti kwa mfalme wa Israeli?” Mmoja wao akajibu, “Hakuna anayetusaliti, ee mfalme. Anayehusika ni Elisha, nabii aliyeko huko Israeli. Yeye humwambia mfalme wa Israeli chochote unachosema hata ukiwa katika chumba chako cha kulala.” Mfalme akawaambia, “Nendeni mkapeleleze mjue mahali alipo nami nitawatuma watu wamkamate.” Basi, wakamwarifu kwamba Elisha alikuwa huko Dothani. Kwa hiyo mfalme akapeleka huko jeshi kubwa pamoja na farasi na magari ya kukokotwa. Jeshi hilo likafika huko wakati wa usiku na kuuzingira mji. Mtumishi wa Elisha alipoamka mapema kesho yake na kutoka nje, akaona jeshi pamoja na farasi na magari ya kukokotwa limeuzingira mji. Akarudi ndani akasema, “Ole wetu, ee, Bwana wangu! Sasa tutafanya nini?” Elisha akamjibu, “Usiogope kwa sababu walio pamoja nasi ni wengi kuliko walio pamoja nao.” Kisha Elisha akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, umfumbue macho ili apate kuona!” Basi, Mwenyezi-Mungu akamfumbua macho huyo kijana, akaona farasi na magari ya moto yakiwa kila mahali katika mlima wote, kumzunguka Elisha. Waaramu waliposhambulia, Elisha alimwomba Mwenyezi-Mungu akisema, “Nakuomba uwafanye watu hawa wawe vipofu!” Mwenyezi-Mungu akasikiliza ombi lake na kuwafanya vipofu. Ndipo Elisha akawaendea na kuwaambia, “Mmepotea njia. Huu siyo mji ambao mnautafuta. Nifuateni nami nitawapeleka kwa yule mnayemtafuta.” Naye akawaongoza mpaka Samaria. Mara walipoingia mjini, Elisha akaomba, akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, wafumbue macho ili waone.” Mwenyezi-Mungu akasikia ombi lake, akawafumbua macho. Nao wakajikuta wako katikati ya mji wa Samaria. Mfalme wa Israeli alipowaona Waaramu, alimwuliza Elisha, “Je, baba, niwaue?” Elisha akajibu, “La, usiwaue. Kwani hawa unaotaka kuwaua uliwateka kwa upanga wako na mshale wako? Wape chakula na maji, wale na kunywa kisha uwaache warudi kwa bwana wao.” Mfalme wa Israeli akawafanyia karamu kubwa; walipomaliza kula na kunywa, akawarudisha kwa bwana wao. Toka wakati huo, Waaramu hawakuishambulia tena nchi ya Israeli.

2 Wafalme 6:8-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi, mfalme wa Shamu alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo changu kitakuwapo mahali fulani. Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami. Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili. Basi mfalme wa Shamu moyo wake ukamfadhaika sana kwa ajili ya jambo hili; akawaita watumishi wake, akawaambia, Je! Hamtanionesha, ni mtu yupi miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli? Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika chumba chako cha kulala. Akasema, Nendeni, mkamwangalie aliko, nipate kupeleka watu kwenda kumchukua. Akaambiwa ya kwamba, Tazama, yuko Dothani. Kwa hiyo akapeleka huko farasi, na magari, na jeshi kubwa; wakafika usiku, wakauzingira mji ule pande zote. Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje? Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao. Elisha akaomba, akasema, Ee BWANA, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. BWANA akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote. Na walipomteremkia Elisha akamwomba BWANA, akasema, Uwapige, nakusihi, watu hawa kwa upofu. Akawapiga kwa upofu sawasawa na neno la Elisha. Elisha akawaambia, Njia hii siyo, na mji huu sio, nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa mtu yule mnayemtafuta. Akawapeleka Samaria. Hata walipokwisha kuingia Samaria, Elisha akasema, BWANA wafumbue macho watu hawa, wapate kuona. BWANA akawafumbua macho wakaona; kumbe! Walikuwa katikati ya Samaria. Naye mfalme wa Israeli alipowaona, akamwambia Elisha, Ee baba yangu, niwapige? Niwapige? Akamjibu, Usiwapige; je! Ungetaka kuwapiga watu ambao umewatwaa mateka kwa upanga wako na uta wako? Weka chakula na maji mbele yao, wapate kula na kunywa, na kwenda kwa bwana wao. Basi akawaandalia chakula tele; nao walipokwisha kula na kunywa, akawaacha, wakaenda zao kwa bwana wao. Na vikosi vya Shamu havikuja tena katika nchi ya Israeli.

2 Wafalme 6:8-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi, mfalme wa Shamu alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo changu kitakuwapo mahali fulani. Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami. Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili. Basi mfalme wa Shamu moyo wake ukamfadhaika sana kwa ajili ya jambo hili; akawaita watumishi wake, akawaambia, Je! Hamtanionyesha, ni mtu yupi miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli? Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika chumba chako cha kulala. Akasema, Enendeni, mkamwangalie aliko, nipate kupeleka watu kwenda kumchukua. Akaambiwa ya kwamba, Tazama, yuko Dothani. Kwa hiyo akapeleka huko farasi, na magari, na jeshi kubwa; wakafika usiku, wakauzingira mji ule pande zote. Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje? Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao. Elisha akaomba, akasema, Ee BWANA, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. BWANA akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote. Na walipomtelemkia Elisha akamwomba BWANA, akasema, Uwapige, nakusihi, watu hawa kwa upofu. Akawapiga kwa upofu sawasawa na neno la Elisha. Elisha akawaambia, Njia hii siyo, na mji huu sio, nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa mtu yule mnayemtafuta. Akawapeleka Samaria. Hata walipokwisha kuingia Samaria, Elisha akasema, BWANA wafumbue macho watu hawa, wapate kuona. BWANA akawafumbua macho wakaona; kumbe! Walikuwa katikati ya Samaria. Naye mfalme wa Israeli alipowaona, akamwambia Elisha, Ee baba yangu, niwapige? Niwapige? Akamjibu, Usiwapige; je! Ungetaka kuwapiga watu ambao umewatwaa mateka kwa upanga wako na uta wako? Weka chakula na maji mbele yao, wapate kula na kunywa, na kwenda kwa bwana wao. Basi akawaandalia chakula tele; nao walipokwisha kula na kunywa, akawaacha, wakaenda zao kwa bwana wao. Na vikosi vya Shamu havikuja tena katika nchi ya Israeli.

2 Wafalme 6:8-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wakati huo mfalme wa Aramu alikuwa akipigana vita na Israeli. Baada ya kukubaliana na maafisa wake, akasema, “Nitapiga kambi yangu mahali fulani na fulani.” Mtu wa Mungu akatuma ujumbe kwa mfalme wa Israeli: “Jihadhari usije ukapita mahali pale, kwa sababu Waaramu wanashuka huko.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akatuma neno la tahadhari mahali pale alikokuwa ameelekezwa na mtu wa Mungu. Mara kwa mara Elisha alimwonya mfalme kwamba watu wawe macho kwenye maeneo kama hayo. Hili lilimfadhaisha sana mfalme wa Aramu. Akawaita maafisa wake, akawauliza, “Je, hamtaniambia ni nani miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli?” Mmoja wa maafisa wake akasema, “Mfalme bwana wangu, hakuna hata mmoja wetu. Lakini Elisha, yule nabii aliye Israeli, humwambia mfalme wa Israeli hata yale maneno unayozungumza katika chumba chako cha kulala.” Mfalme akaagiza akisema, “Nendeni, mkatafute aliko, ili niweze kutuma watu kumkamata.” Taarifa ikarudi kwamba, “Yuko Dothani.” Ndipo akatuma farasi na magari ya vita na jeshi lenye nguvu huko. Walikwenda usiku na kuuzunguka mji. Kesho yake asubuhi na mapema, mtumishi wa mtu wa Mungu alipoamka na kutoka nje, jeshi, pamoja na farasi na magari ya vita, likawa limeuzunguka mji. Mtumishi wake akasema, “Ole wetu, bwana wangu! Tutafanya nini?” Nabii akajibu, “Usiogope. Wale walio pamoja nasi ni wengi zaidi kuliko wale walio pamoja nao.” Kisha Elisha akaomba, “Ee BWANA, mfumbue macho huyu mtumishi ili apate kuona.” Ndipo BWANA akayafumbua macho ya yule mtumishi, naye akatazama na kuona vilima vimejaa farasi na magari ya moto, yamemzunguka Elisha pande zote. Wakati adui waliposhuka kumwelekea, Elisha akamwomba BWANA: “Wapige watu hawa kwa upofu.” Basi Mungu akawapiga kwa upofu, kama Elisha alivyoomba. Elisha akawaambia, “Hii sio njia yenyewe, na huu sio huo mji. Nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa huyo mtu mnayemtafuta.” Naye akawapeleka Samaria. Baada ya kuingia mjini, Elisha akasema, “BWANA, yafungue macho ya watu hawa ili wapate kuona.” Ndipo BWANA akayafungua macho yao, na walipotazama, kumbe hapo ndipo walipojikuta, ndani ya Samaria. Wakati mfalme wa Israeli alipowaona, akamuuliza Elisha, “Je, baba yangu, niwaue?” Naye akajibu, “Usiwaue. Je, utawaua watu uliowateka kwa upanga wako mwenyewe na upinde wako? Wape chakula na maji ili wapate kula na kunywa, na kisha wamrudie bwana wao.” Basi akawaandalia karamu kubwa, na baada ya kula na kunywa, akawaaga nao wakarudi kwa bwana wao. Hivyo, vikosi kutoka Aramu vikakoma kuvamia nchi ya Israeli.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha