Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 5:9-19

2 Wafalme 5:9-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha. Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Nenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi. Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nilidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la BWANA, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma. Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira. Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi? Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi. Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani kote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee zawadi kutoka mtumwa wako. Lakini akasema, Kama BWANA aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa. Naamani akasema; Kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa BWANA. Jambo hili BWANA amwachilie mtumwa wako; bwana wangu akiingia nyumbani mwa Rimoni ili aabudu humo, naye akitegemea mkononi mwangu, nami nikijiinama nyumbani mwa Rimoni, hapo ninapojiinama nyumbani mwa Rimoni, BWANA amwachilie mtumwa wako jambo hili. Elisha akamwambia, Nenda kwa amani.

2 Wafalme 5:9-19 Biblia Habari Njema (BHN)

Naamani akaenda na farasi wake na gari lake mpaka mlangoni mwa Elisha. Elisha akamtuma mtumishi wake amwambie, “Nenda ukaoge mara saba mtoni Yordani, nawe utapona kabisa.” Lakini Naamani alikasirika sana, akaenda zake akisema, “Nilidhani kwamba hakika atanijia na kumwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, apitishe mikono yake juu ya mahali ninapougua na kuniponya! Isitoshe, je, mito Abana na Farpari ya huko Damasko si bora kuliko mito yote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga humo na kupona?” Akaondoka na kurudi nyumbani, huku amekasirika sana. Watumishi wake wakamwendea na kumwambia, “Baba yetu kama nabii angekuambia ufanye jambo fulani gumu, je, hungelifanya? Sasa, aliyokuambia tu ni: ‘Jioshe, ili upone!’” Basi, Naamani akateremka mtoni Yordani akajitumbukiza humo mara saba, kama alivyoagizwa na Elisha mtu wa Mungu, naye akapona kabisa. Ngozi yake ikawa imara na yenye afya kama ya mtoto mdogo. Ndipo akarudi kwa mtu wa Mungu pamoja na watu wake, akasema, “Sasa najua kwamba hakuna Mungu yeyote ila tu Mungu wa Israeli; kwa hiyo, tafadhali sasa upokee zawadi za mtumishi wako.” Elisha akajibu, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai ambaye ninamtumikia, kwamba sitapokea zawadi yoyote.” Naamani akamsihi, lakini Elisha akakataa kabisa. Naamani akasema, “Ikiwa hutapokea zawadi zangu, basi tafadhali umpatie mtumishi wako udongo unaoweza kubebwa na nyumbu wawili, kwani toka leo mimi mtumishi wako sitatoa sadaka za kuteketezwa wala tambiko kwa miungu mingine ila tu kwa Mwenyezi-Mungu. Naye Mwenyezi-Mungu na anisamehe ninapofuatana na mfalme wangu kwenda kuabudu katika hekalu la Rimoni mungu wa Aramu. Naomba Mwenyezi-Mungu anisamehe!” Elisha akamwambia, “Nenda kwa amani.” Naamani akaenda zake. Alipokuwa bado hajaenda mbali

2 Wafalme 5:9-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha. Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi. Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la BWANA, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma. Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira. Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi? Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi. Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako. Lakini akasema, Kama BWANA aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa. Naamani akasema; Kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa BWANA. Jambo hili BWANA amwachilie mtumwa wako; bwana wangu akiingia nyumbani mwa Rimoni ili aabudu humo, naye akitegemea mkononi mwangu, nami nikijiinama nyumbani mwa Rimoni, hapo ninapojiinama nyumbani mwa Rimoni, BWANA amwachilie mtumwa wako jambo hili. Akamwambia, Enenda kwa amani

2 Wafalme 5:9-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kwa hiyo Naamani akaenda, akiwa na farasi zake na magari yake, na kusimama mlangoni mwa nyumba ya Elisha. Elisha akamtuma mjumbe kumwambia, “Nenda uoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itapona, nawe utatakasika.” Lakini Naamani akaondoka akiwa amekasirika, akasema, “Hakika nilidhani kwamba angetoka nje, asimame na kuliitia jina la BWANA Mungu wake, na kuweka mkono wake juu ya mahali pagonjwa, aniponye ukoma wangu. Je, Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora zaidi kuliko mito yoyote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga ndani ya hiyo mito na kutakasika?” Basi akageuka na kuondoka kwa hasira kuu. Watumishi wa Naamani wakamwendea na kumwambia, “Baba yangu, kama huyo nabii angekuambia kufanya jambo lililo kubwa, je, usingelifanya? Je, si zaidi sana basi, anapokuambia, ‘Oga na utakasike!’ ” Hivyo akashuka na kujizamisha ndani ya Yordani mara saba, kama vile huyo mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia, nayo nyama ya mwili wake ikapona na kutakasika kama ya mwili wa mvulana mdogo. Kisha Naamani na wahudumu wake wote wakarudi kwa yule mtu wa Mungu. Akasimama mbele yake na kusema, “Sasa najua kwamba hakuna Mungu katika ulimwengu wote isipokuwa katika Israeli. Tafadhali sasa upokee zawadi kutoka kwa mtumishi wako.” Nabii akajibu, “Hakika kama BWANA aishivyo, ambaye ninamtumikia, sitapokea kitu hata kimoja.” Ingawa Naamani alimsihi sana, yeye alikataa. Naamani akasema, “Ikiwa hutapokea, tafadhali mtumishi wako na apewe udongo kiasi cha mzigo wa kuweza kubebwa na punda wawili, kwa sababu mtumishi wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa na dhabihu kwa mungu mwingine isipokuwa BWANA. Lakini BWANA na amsamehe mtumishi wake kwa kitu hiki kimoja: Wakati bwana wangu atakapoingia kwenye hekalu la Rimoni ili kusujudu, naye akiwa anauegemea mkono wangu, nami nikasujudu huko pia, wakati nitakaposujudu ndani ya hekalu la Rimoni, BWANA na amsamehe mtumishi wako kwa ajili ya jambo hili.” Elisha akamwambia, “Nenda kwa amani.” Baada ya Naamani kusafiri umbali fulani

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha