2 Wafalme 4:38-44
2 Wafalme 4:38-44 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Elisha akafika Gilgali tena; na kulikuwa na njaa katika nchi; na hao wana wa manabii walikuwa wakikaa mbele yake. Akamwambia mtumishi wake, Teleka sufuria kubwa, uwapikie wana wa manabii. Na mmoja wao akaenda nje kondeni ili kuchuma mboga, akaona mtangomwitu, akayachuma matangomwitu, hata nguo yake ikawa imejaa, akaja akayapasuapasua sufuriani; kwa maana hawakuyajua. Basi wakawapakulia hao watu ili wale. Ikawa, walipokuwa katika kula chakula, wakapiga kelele, wakasema, Mauti imo sufuriani, Ee mtu wa Mungu. Wala hawakuweza kula. Lakini yeye akasema, Leteni unga. Naye akautupa ndani ya sufuria; akasema, Wapakulie watu, ili wale. Wala hakikuwamo kitu kibaya sufuriani. Tena, akaja mtu kutoka Baal-shalisha, akamletea mtu wa Mungu chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano guniani. Akasema, Uwape watu, ili wale. Na mtumishi wake akasema, Je! Niwaandalie hiki watu mia moja? Lakini akasema, Uwape watu, ili wale; kwa kuwa BWANA asema hivi, Watakula na kusaza. Basi akawaandalia, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la BWANA.
2 Wafalme 4:38-44 Biblia Habari Njema (BHN)
Elisha akarudi Gilgali wakati nchini kulikuwa na njaa. Siku moja, alipokuwa akifundisha wanafunzi wa manabii alimwambia mtumishi wake, “Weka chungu kikubwa motoni, uwapikie manabii.” Mmoja wao akaenda shambani na kuchuma mboga. Huko akaona mtango-mwitu, akachuma matango mengi kadiri alivyoweza kuchukua. Akaja nayo, akayakatakata na kuyatia chunguni bila kuyajua. Chakula kikapakuliwa. Lakini walipokionja wakamlilia Elisha wakisema, “Ee mtu wa Mungu, chakula hiki kitatuua!” Nao hawakuweza kukila. Elisha akaagiza aletewe unga. Akaletewa unga, naye akautia ndani ya chungu na kusema, “Sasa wape chakula wale.” Wakakila, na hapo hakikuwadhuru. Mtu Mmoja akatoka Baal-shalisha, akamletea Elisha mikate ishirini iliyotengenezwa kwa shayiri ya malimbuko ya mavuno ya mwaka huo na masuke mabichi ya ngano guniani. Elisha akamwagiza Gehazi awape watu wale. Mtumishi wake akasema, “Sitawapa kwa sababu hakitawatosha watu 100”. Elisha akasema, “Wape wale, kwa sababu Mwenyezi-Mungu amesema kwamba watakula washibe na kingine kitabaki.” Mtumishi wake akawaandalia chakula, wakala wote wakashiba, na kingine kikabaki, kama Mwenyezi-Mungu alivyosema.
2 Wafalme 4:38-44 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Elisha akafika Gilgali tena; na kulikuwa na njaa katika nchi; na hao wana wa manabii walikuwa wakikaa mbele yake. Akamwambia mtumishi wake, Teleka sufuria kubwa, uwapikie wana wa manabii. Na mmoja wao akaenda nje kondeni ili kuchuma mboga, akaona mtango-mwitu, akayachuma matango-mwitu, hata nguo yake ikawa imejaa, akaja akayapasua-pasua sufuriani; kwa maana hawakuyajua. Basi wakawapakulia hao watu ili wale. Ikawa, walipokuwa katika kula chakula, wakapiga kelele, wakasema, Mauti imo sufuriani, Ee mtu wa Mungu. Wala hawakuweza kula. Lakini yeye akasema, Leteni unga. Naye akautupa ndani ya sufuria; akasema, Wapakulie watu, ili wale. Wala hakikuwamo kitu kibaya sufuriani. Tena, akaja mtu kutoka Baal-shalisha, akamletea mtu wa Mungu chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano guniani. Akasema, Uwape watu, ili wale. Na mtumishi wake akasema, Je! Niwaandikie hiki watu mia? Lakini akasema, Uwape watu, ili wale; kwa kuwa BWANA asema hivi, Watakula na kusaza. Basi akawaandikia, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la BWANA.
2 Wafalme 4:38-44 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Elisha akarudi Gilgali, nako huko kulikuwa na njaa katika eneo lile. Wakati wana wa kundi la manabii walipokuwa wanakutana naye, akamwambia mtumishi wake, “Teleka chungu kikubwa jikoni uwapikie manabii.” Mmoja wao akatoka kwenda mashambani kuchuma mboga na akapata mtango mwitu. Akachuma matango na kujaza nguo yake aliyoikunja ili kubebea. Aliporudi, akayakatakata na kuyatumbukiza ndani ya chungu, ingawa hakuna aliyejua ni nini. Mchuzi ukagawiwa watu, lakini walipoanza kula, wakalia, “Ee mtu wa Mungu, kuna mauti ndani ya chungu.” Nao hawakuweza kula. Elisha akasema, “Leteni unga.” Akauweka ndani ya chungu na kusema, “Wagawie watu ili wale.” Wala hapakuwa na kitu chochote chenye madhara ndani ya chungu. Akaja mtu kutoka Baal-Shalisha, akimletea mtu wa Mungu mikate ishirini ya shayiri iliyookwa kutokana na nafaka ya kwanza, pamoja na masuke ya nafaka mpya. Elisha akasema, “Wape watu ili wale.” Mtumishi wake akamuuliza, “Nitawezaje kuandaa hii mbele ya watu mia?” Lakini Elisha akajibu, “Wape watu ili wale. Kwa maana hivi ndivyo asemavyo BWANA: ‘Watakula na kusaza.’ ” Basi akaiandaa mbele yao ile mikate, wakala na baadhi yake wakasaza, sawasawa na neno la BWANA.