2 Wafalme 4:1-7
2 Wafalme 4:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wanafunzi wa manabii akamwendea Elisha, akamwambia, “Mtumishi wako, mume wangu amefariki, na kama ujuavyo, alikuwa mcha Mungu, lakini aliyemwia fedha amekuja kuwatwaa wanangu wawili wawe watumwa wake.” Elisha akamwuliza, “Sasa nikusaidieje? Niambie kile ulicho nacho nyumbani.” Mama huyo mjane akamjibu, “Mimi mtumishi wako sina kitu chochote ila chupa ndogo ya mafuta.” Elisha akamwambia, “Nenda kwa jirani zako uazime vyombo vitupu vingi kadiri utakavyopata. Kisha uende, wewe pamoja na wanao, mjifungie ndani ya nyumba, na muanze kujaza mafuta. Kila chombo mnachojaza, kiwekeni kando.” Akaenda na kujifungia ndani ya nyumba na wanawe na kuanza kumimina mafuta ndani ya vyombo. Vilipojaa vyote, akamwambia mwanawe mmojawapo, “Niletee chombo kingine.” Mwanae akamjibu, “Vyote vimejaa!” Hapo mafuta yakakoma kutiririka. Akarudi kwa mtu wa Mungu na kumweleza habari hizo. Naye mtu wa Mungu akamwambia, “Nenda ukauze hayo mafuta na kulipa madeni yako, ndipo wewe na wanao mtaishi kwa kutumia hayo yatakayobaki.”
2 Wafalme 4:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha BWANA; na aliyemdai amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa. Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta. Akasema, Nenda, ukaazime vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usiazime vichache. Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina. Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma. Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema, Nenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako.
2 Wafalme 4:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha BWANA; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa. Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta. Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache. Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina. Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma. Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako.
2 Wafalme 4:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mke wa mmoja wa wana wa manabii akamlilia Elisha, akamwambia, “Mtumishi wako, mume wangu, amekufa, nawe unajua alikuwa anamcha BWANA. Lakini sasa yule anayemdai anakuja kuchukua wanangu wawili kama watumwa wake.” Elisha akamjibu, “Nitawezaje kukusaidia? Niambie, una nini ndani ya nyumba yako?” Akasema, “Mtumishi wako hana kitu chochote kabisa, isipokuwa mafuta kidogo.” Elisha akasema, “Zunguka kwa majirani zako wote ukaombe vyombo vitupu. Usiombe vichache. Kisha ingia ndani na ujifungie mlango, wewe na wanao. Mimina mafuta kwenye vyombo vyote, na kila kimoja kinapojaa, kiweke kando.” Yule mjane akaondoka na kujifungia ndani, yeye na wanawe. Wao wakamletea vyombo, naye akaendelea kumimina mafuta. Vyombo vyote vilipojaa, akamwambia mwanawe, “Niletee chombo kingine.” Lakini mwanawe akajibu, “Hakuna chombo kingine kilichobaki.” Basi mafuta yakakoma kutiririka. Yule mwanamke akaenda akamwambia yule mtu wa Mungu, naye mtu wa Mungu akasema, “Nenda ukayauze hayo mafuta ulipe madeni yako. Wewe na wanao mnaweza kuishi kwa kile kinachosalia.”