2 Wafalme 19:14-37
2 Wafalme 19:14-37 Biblia Habari Njema (BHN)
Mfalme Hezekia alipokea barua kutoka kwa wajumbe na kuisoma. Kisha akaenda na kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, naye akaiweka mbele yake Mwenyezi-Mungu. Halafu akamwomba Mwenyezi-Mungu akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, unayekaa katika kiti cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa, ni wewe tu uliye Mungu, unayetawala falme zote za ulimwengu. Wewe uliumba nchi na mbingu. Ee Mwenyezi-Mungu, fumbua macho uone, tega sikio lako, uyasikie matusi yote ambayo Senakeribu amepeleka kukutukana wewe Mungu uliye hai. Ee Mwenyezi-Mungu, ni kweli kwamba wafalme wa Ashuru wameangamiza mataifa na nchi zao. Walitupa miungu yao motoni kwa sababu haikuwa miungu ya kweli, bali sanamu za miti na mawe zilizochongwa na mikono ya watu. Sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, nakusihi utuokoe makuchani mwa Senakeribu, falme zote za dunia zijue kwamba ni wewe peke yako, ee Mwenyezi-Mungu, uliye Mungu.” Kisha Isaya, mwana wa Amozi akatuma ujumbe kwa Hezekia, akisema, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ‘Nimesikia ombi lako kwangu kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru:’ Hili ndilo neno la Mwenyezi-Mungu alilosema kumhusu Senakeribu: Anakudharau, anakubeza binti Siyoni, anatikisa kichwa chake nyuma yako binti Yerusalemu. Je, uliyekuwa unamkashifu na kumdhihaki ni nani? Nani umemwinulia sauti na kumkodolea macho kwa kiburi? Juu ya Mtakatifu wa Israeli!” Kwa kuwatuma wajumbe wako umemkashifu Bwana, wewe umesema, “Kwa magari yangu mengi ya vita, nimekwea vilele vya milima mpaka kilele cha Lebanoni. Nimekata mierezi yake mirefu, na misonobari mizurimizuri; nimeingia mpaka ndani yake na ndani ya misitu yake mikubwa. Nimechimba visima na kunywa maji mageni nilikausha mito yote ya Misri kwa nyayo za miguu yangu. ‘Je, hujasikia, kwamba nilipanga jambo hili tangu awali? Ninachotekeleza sasa nilikipanga zamani.’ Nilikuweka uijenge miji yenye ngome kwa rundo la magofu. Wakazi wake wakiwa wameishiwa nguvu, wametishika na kufadhaika, wamekuwa kama mimea ya shambani, kama majani yasiyo na nguvu. Kama majani yaotayo juu ya paa; yakaukavyo kabla ya kukua. Najua kuketi kwako, na kuamka kwako nako kuingia kwako; nayo mipango yako dhidi yangu. Kwa vile umefanya mipango dhidi yangu na nimeusikia ufidhuli wako, nitatia ndoana yangu puani mwako, na lijamu yangu kinywani mwako. Nitakurudisha njia ileile uliyojia.” Kisha Isaya akamwambia mfalme Hezekia, “Na hii ndio itakuwa ishara kwako Hezekia: Mwaka huu na mwaka ujao mtakula kinachomea chenyewe bila kupandwa. Lakini katika mwaka wa tatu mtapanda na kuvuna mavuno; mtapanda mizabibu na kula matunda yake. Wale watakaobaki katika ukoo wa Yuda wataongezeka na kuwa wengi kama vile mti unavyotoa mizizi yake udongoni na kuzaa matunda juu. Maana kutakuwako watu watakaosalia huko Yerusalemu; naam, huko mlimani Siyoni kutakuwako watu wachache watakaosalimika; maana Mwenyezi-Mungu amedhamiria kukamilisha hayo. “Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya mfalme wa Waashuru: ‘Hataingia katika mji huu wala kuupiga mshale wala kuujia kwa ngao wala kuuzingira. Atarudi kwa njia ileile aliyoijia na wala hataingia katika mji huu,’ ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu. ‘Naam, kwa ajili ya heshima yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi nitaulinda na kuokoa mji huu.’” Basi, usiku huo malaika wa Mwenyezi-Mungu aliingia kambini mwa Waashuru na kuwaua watu laki moja. Kulipopambazuka watu wakaamka, hao wote walionekana wakiwa maiti. Kisha Senakeribu mfalme wa Ashuru aliondoka akaenda zake na kukaa Ninewi. Siku moja wakati Senakeribu alipokuwa akiabudu katika nyumba ya Nisroki mungu wake, wanawe wawili, Adrameleki na Sharezeri walimuua kwa upanga, halafu wakakimbilia nchini Ararati. Naye Esar-hadoni, mwanawe akatawala badala yake.
2 Wafalme 19:14-37 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya BWANA, akaukunjua mbele za BWANA. Naye Hezekia akaomba mbele za BWANA, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, Ee BWANA, usikie; fumbua macho yako, Ee BWANA, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu aje nayo ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, BWANA, wafalme wa Ashuru wamewaharibu mataifa na nchi zao, na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana haikuwa miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu, ndiyo sababu wakaiharibu. Basi sasa, Ee BWANA, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe BWANA Mungu, wewe peke yako. Ndipo Isaya, mwana wa Amozi, akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akisema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa umeniomba juu ya Senakeribu, mfalme wa Ashuru, mimi nimekusikia. Tamko alilolitamka BWANA katika habari zake ndilo hili, Bikira, binti Sayuni, amekudharau, na kukudhihaki sana; binti Yerusalemu ametikisa kichwa chake juu yako. Ni nani uliyemshutumu na kumtukana? Umeinua sauti yako juu ya nani, na kuinua macho yako juu? Juu ya Mtakatifu wa Israeli. Kwa vinywa vya wajumbe wako umemshutumu Bwana, ukasema, Kwa wingi wa magari yangu nimepanda juu ya vilele vya milima, mpaka mahali pa ndani pa Lebanoni. Nami nitaikata mierezi yake mirefu, na misonobari yake mizuri; nami nitaingia ndani ya makazi yake yaliyo mbali sana, na msitu wa shamba lake lizaalo sana. Nimechimba na kunywa maji mageni, na kwa nyayo za miguu yangu nitaikausha mito yote ya Misri. Je! Hukusikia wewe ya kuwa mimi ndimi niliyeyatenda hayo tokea zamani, na kuyafanya tokea siku za kale? Sasa mimi nimelitimiza jambo hili, iwe kazi yako kuangamiza miji yenye boma, hata ikawe chungu na magofu. Ndiyo sababu wenyeji wao walikuwa na nguvu chache, wakafadhaika, na kuhangaika; wakawa kama majani ya mashamba, kama miche mibichi, kama majani juu ya dari, na kama ngano iliyokaushwa kabla haijaiva. Lakini nakujua, kuketi kwako, na kutoka kwako, na kuingia kwako; na ghadhabu yako unayonighadhibikia. Kwa sababu ya kunighadhibikia kwako, na kwa sababu kutakabari kwako kumefika masikioni mwangu; kwa sababu hiyo nitatia kulabu yangu puani mwako, na hatamu yangu midomoni mwako, nami nitakurudisha nyuma kwa njia ile ile uliyoijia. Na kwako wewe hii ndiyo dalili; mwaka huu mtakula vitu viotavyo vyenyewe; na mwaka wa pili mtakula mazao ya vitu hivyo; na mwaka wa tatu pandeni mbegu, kavuneni; mkapande mashamba ya mizabibu, mkale matunda yake. Na mabaki yaliyookoka ya nyumba ya Yuda yatatia mizizi chini, na kuzaa matunda juu. Maana mabaki yatatoka katika Yerusalemu, na wao watakaookoka katika mlima wa Sayuni wivu wa BWANA utatimiza jambo hilo. Basi BWANA asema hivi katika habari za mfalme wa Ashuru, Yeye hatauingia mji huu, wala hatapiga mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake. Njia ile ile aliyojia, kwa njia iyo hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya mji huu, asema BWANA. Maana nitaulinda mji huu, niuokoe, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu. Ikawa usiku uo huo malaika wa BWANA alitoka, akakiingia kituo cha Waashuri, akawapiga watu mia moja themanini na tano elfu. Na watu walipoamka asubuhi na mapema, kumbe! Hao walikuwa maiti wote pia. Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka, akaenda zake, akarudi akakaa Ninawi. Ikawa, alipokuwa akiabudu nyumbani mwa Nisroki, mungu wake, Adrameleki na Shareza wakampiga kwa upanga; wakaikimbilia nchi ya Ararati. Na Esar-hadoni mwanawe akatawala mahali pake.
2 Wafalme 19:14-37 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya BWANA, akaukunjua mbele za BWANA. Naye Hezekia akaomba mbele za BWANA, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, Ee BWANA, usikie; fumbua macho yako, Ee BWANA, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu aje nayo ili kumtukana Mungu aliye hai. Ni kweli, BWANA, wafalme wa Ashuru wamewaharibu mataifa na nchi zao, na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana haikuwa miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu, ndiyo sababu wakaiharibu. Basi sasa, Ee BWANA, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe BWANA Mungu, wewe peke yako. Ndipo Isaya, mwana wa Amozi, akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akisema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa umeniomba juu ya Senakeribu, mfalme wa Ashuru, mimi nimekusikia. Tamko alilolitamka BWANA katika habari zake ndilo hili, Bikira, binti Sayuni, amekudharau, na kukudhihaki sana; binti Yerusalemu ametikisa kichwa chake juu yako. Ni nani uliyemshutumu na kumtukana? Umeinua sauti yako juu ya nani, na kuinua macho yako juu? Juu ya Mtakatifu wa Israeli. Kwa vinywa vya wajumbe wako umemshutumu Bwana, ukasema, Kwa wingi wa magari yangu nimepanda juu ya vilele vya milima, mpaka mahali pa ndani pa Lebanoni. Nami nitaikata mierezi yake mirefu, na misunobari yake mizuri; nami nitaingia ndani ya makazi yake yaliyo mbali sana, na msitu wa shamba lake lizaalo sana. Nimechimba na kunywa maji mageni, na kwa nyayo za miguu yangu nitaikausha mito yote ya Misri. Je! Hukusikia wewe ya kuwa mimi ndimi niliyeyatenda hayo tokea zamani, na kuyafanya tokea siku za kale? Sasa mimi nimelitimiza jambo hili, iwe kazi yako kuangamiza miji yenye boma, hata ikawe chungu na magofu. Ndiyo sababu wenyeji wao walikuwa na nguvu chache, wakafadhaika, na kuhangaika; wakawa kama majani ya mashamba, kama miche mibichi, kama majani juu ya dari, na kama ngano iliyokaushwa kabla haijaiva. Lakini nakujua, kuketi kwako, na kutoka kwako, na kuingia kwako; na ghadhabu yako unayonighadhibikia. Kwa sababu ya kunighadhibikia kwako, na kwa sababu kutakabari kwako kumefika masikioni mwangu; kwa sababu hiyo nitatia kulabu yangu puani mwako, na hatamu yangu midomoni mwako, nami nitakurudisha nyuma kwa njia ile ile uliyoijia. Na kwako wewe hii ndiyo dalili; mwaka huu mtakula vitu viotavyo vyenyewe; na mwaka wa pili mtakula mazao ya vitu hivyo; na mwaka wa tatu pandeni mbegu, kavuneni; mkapande mashamba ya mizabibu, mkale matunda yake. Na mabaki yaliyookoka ya nyumba ya Yuda yatatia mizizi chini, na kuzaa matunda juu. Maana mabaki yatatoka katika Yerusalemu, na wao watakaookoka katika mlima wa Sayuni wivu wa BWANA utatimiza jambo hilo. Basi BWANA asema hivi katika habari za mfalme wa Ashuru, Yeye hatauingia mji huu, wala hatapiga mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake. Njia ile ile aliyojia, kwa njia iyo hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya mji huu, asema BWANA. Maana nitaulinda mji huu, niuokoe, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu. Ikawa usiku uo huo malaika wa BWANA alitoka, akakiingia kituo cha Waashuri, akawapiga watu mia na themanini na tano elfu. Na watu walipoondoka asubuhi na mapema, kumbe! Hao walikuwa maiti wote pia. Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka, akaenda zake, akarudi akakaa Ninawi. Ikawa, alipokuwa akiabudu nyumbani mwa Nisroki, mungu wake, Adrameleki na Shareza wakampiga kwa upanga; wakaikimbilia nchi ya Ararati. Na Esar-hadoni mwanawe akatawala mahali pake.
2 Wafalme 19:14-37 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hezekia akapokea barua kutoka kwa wale wajumbe, naye akaisoma. Kisha akapanda katika Hekalu la BWANA, akaikunjua mbele za BWANA. Naye Hezekia akamwomba BWANA akisema: “Ee BWANA, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe umeumba mbingu na nchi. Tega sikio, Ee BWANA, usikie; fungua macho yako, Ee BWANA, uone; sikiliza maneno ambayo Senakeribu ametuma kumtukana Mungu aliye hai. “Ni kweli, Ee BWANA, kwamba wafalme wa Ashuru wameyaangamiza mataifa haya na nchi zao. Wameitupa miungu yao kwenye moto na kuiangamiza, kwa kuwa haikuwa miungu, bali miti na mawe tu iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. Sasa basi, Ee BWANA Mungu wetu, tuokoe kutoka mkononi mwake, ili falme zote duniani zipate kujua kwamba wewe peke yako, Ee BWANA, ndiwe Mungu.” Kisha Isaya mwana wa Amozi akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akasema: “Hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Israeli: Nimesikia maombi yako kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru. Hili ndilo neno ambalo BWANA amelisema dhidi yake: “ ‘Bikira Binti Sayuni anakudharau na kukudhihaki. Binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake unapokimbia. Ni nani uliyemtukana na kumkufuru? Ni nani uliyeinua sauti yako dhidi yake, na kumwinulia macho yako kwa kiburi? Ni dhidi ya yule Aliye Mtakatifu wa Israeli! Kupitia kwa wajumbe wako umelundika matukano juu ya Bwana. Nawe umesema, “Kwa magari yangu mengi ya vita, nimepanda juu ya vilele vya milima, vilele vya juu sana katika Lebanoni. Nami nimeiangusha mierezi yake mirefu, misunobari yake iliyo bora sana. Nimefikia sehemu zake zilizo mbali sana, misitu yake iliyo mizuri sana. Nimechimba visima katika nchi za kigeni na kunywa maji yake. Kwa nyayo za miguu yangu nimekausha vijito vyote vya Misri.” “ ‘Je, hujasikia? Zamani sana niliamuru hili. Siku za kale nilipanga hili; sasa nimelifanya litokee, kwamba umegeuza miji yenye ngome kuwa malundo ya mawe. Watu wa miji hiyo wameishiwa nguvu, wanavunjika mioyo na kuaibishwa. Wao ni kama mimea katika shamba, kama machipukizi mororo ya kijani, kama majani yachipuayo juu ya paa la nyumba, ambayo hukauka kabla ya kukua. “ ‘Lakini ninajua mahali ukaapo, kutoka kwako na kuingia kwako, na jinsi unavyoghadhibika dhidi yangu. Kwa sababu unaghadhibika dhidi yangu, na ufidhuli wako umefika masikioni mwangu, nitaweka ndoana yangu puani mwako na hatamu yangu kinywani mwako, nami nitakufanya urudi kwa njia ile uliyoijia.’ “Hii ndiyo itakuwa ishara kwako, ee Hezekia: “Mwaka huu utakula kile kiotacho chenyewe, na mwaka wa pili utakula kutoka machipukizi yake. Lakini katika mwaka wa tatu, panda na uvune, panda mashamba ya mizabibu na ule matunda yake. Mara nyingine tena mabaki ya nyumba ya Yuda wataeneza mizizi chini na kuzaa matunda juu. Kwa kuwa kutoka Yerusalemu watakuja mabaki, na kutoka Mlima Sayuni kundi la walionusurika. Wivu wa BWANA Mwenye Nguvu Zote ndio utatimiza jambo hili. “Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA kuhusu mfalme wa Ashuru: “Hataingia katika mji huu wala hatapiga mshale hapa. Hatakuja mbele yake akiwa na ngao, wala kupanga majeshi kuuzingira. Kwa njia ile aliyoijia, ndiyo atakayorudi; hataingia katika mji huu, asema BWANA. Nitaulinda mji huu na kuuokoa, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu.” Usiku ule, malaika wa BWANA akaenda, akawaua wanajeshi 185,000 katika kambi ya Waashuru. Wenzao walipoamka asubuhi yake, walikuta maiti kila mahali! Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akavunja kambi na kuondoka. Akarudi Ninawi na kukaa huko. Siku moja, alipokuwa akiabudu katika hekalu la mungu wake Nisroki, wanawe Adrameleki na Shareza wakamuua kwa upanga, nao wakakimbilia nchi ya Ararati. Naye Esar-Hadoni mwanawe akawa mfalme badala yake.