2 Wafalme 18:9-12
2 Wafalme 18:9-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Katika mwaka wa nne wa enzi ya Hezekia, ambao pia ulikuwa mwaka wa saba wa enzi ya Hoshea mwana wa Ela mfalme wa Israeli, Shalmanesa mfalme wa Ashuru alishambulia mji wa Samaria na kuuzingira. Mwishoni mwa mwaka wa tatu Waashuru waliuteka Samaria. Ilikuwa katika mwaka wa sita wa enzi ya Hezekia na pia mwaka wa tisa wa enzi ya Hoshea mfalme wa Israeli, Samaria ulipotekwa. Mfalme wa Ashuru aliwachukua watu wa Israeli mateka mpaka Ashuru na kuwaweka wengine wao katika mji wa Hala, na karibu ya Habori, mji wa Gozani, pia na wengine katika miji ya Media, kwa sababu Waisraeli hawakutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, bali walivunja agano lake, hata hawakusikia wala kutii yote Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliyowaamuru.
2 Wafalme 18:9-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata katika mwaka wa nne wa Hezekia, ndio mwaka wa saba wa Hoshea, mwana wa Ela, mfalme wa Israeli, Shalmanesa, mfalme wa Ashuru, akakwea ili kupigana na Samaria, akauhusuru. Wakautwaa baada ya miaka mitatu; yaani, katika mwaka wa sita wa Hezekia, ndio mwaka wa tisa wa Hoshea, mfalme wa Israeli, ndipo Samaria ulipotwaliwa. Mfalme wa Ashuru akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala, na katika Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi; kwa sababu hawakuitii sauti ya BWANA, Mungu wao, bali waliyavunja maagano yake, mambo yote ambayo Musa mtumishi wa BWANA aliwaamuru, wasikubali kuyasikiliza, wala kuyatenda.
2 Wafalme 18:9-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata katika mwaka wa nne wa Hezekia, ndio mwaka wa saba wa Hoshea, mwana wa Ela, mfalme wa Israeli, Shalmanesa, mfalme wa Ashuru, akakwea ili kupigana na Samaria, akauhusuru. Wakautwaa baada ya miaka mitatu; yaani, katika mwaka wa sita wa Hezekia, ndio mwaka wa kenda wa Hoshea, mfalme wa Israeli, ndipo Samaria ulipotwaliwa. Mfalme wa Ashuru akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala, na katika Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi; kwa sababu hawakuitii sauti ya BWANA, Mungu wao, bali waliyahalifu maagano yake, mambo yote ambayo Musa mtumishi wa BWANA aliwaamuru, wasikubali kuyasikiliza, wala kuyatenda.
2 Wafalme 18:9-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mwaka wa nne wa Mfalme Hezekia, ambao ulikuwa mwaka wa saba wa Hoshea mwana wa Ela kutawala Israeli, Shalmanesa mfalme wa Ashuru alikwenda kuishambulia Samaria na kuuzunguka kwa majeshi. Baada ya miaka mitatu Waashuru wakautwaa. Kwa hiyo Samaria ulitekwa katika mwaka wa sita wa utawala wa Mfalme Hezekia, ambao ulikuwa mwaka wa tisa wa utawala wa Hoshea mfalme wa Israeli. Mfalme wa Ashuru akawahamishia Waisraeli huko Ashuru na akawaweka Hala, na Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi. Hili lilitokea kwa sababu hawakumtii BWANA Mungu wao, lakini walikuwa wamevunja agano lake, yale yote ambayo Mose mtumishi wa BWANA aliwaamuru. Hawakuzisikiliza amri wala kuzitimiza.