2 Wafalme 14:1-7
2 Wafalme 14:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika mwaka wa pili wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. Naye alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na kenda katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, ila si kama babaye Daudi; akafanya kama yote aliyoyafanya baba yake Yoashi. Walakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu. Ikawa, mara ufalme ulipokuwa imara mkononi mwake, aliwaua watumishi wale waliomwua mfalme baba yake; ila hakuwaua watoto wa hao wauaji; kama ilivyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, kama alivyoamuru BWANA, akisema, Mababa wasife kwa makosa ya wana, wala wana wasife kwa makosa ya mababa; lakini kila mtu atakufa kwa kosa lake mwenyewe. Akawaua Waedomi katika Bonde la Chumvi watu elfu kumi; akautwaa Sela vitani, akauita jina lake Yoktheeli hata leo.
2 Wafalme 14:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Katika mwaka wa pili wa enzi ya Yehoashi mwana wa Yehoahazi huko Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alipoanza kutawala alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano, naye alitawala katika Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu. Alitenda yaliyo mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwa kama babu yake Daudi. Bali alifanya mambo yote kama Yoashi baba yake; isipokuwa mahali pa ibada milimani hapakuharibiwa na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani mahali hapo. Mara tu Amazia alipojiimarisha mamlakani, aliwaua watumishi waliomuua mfalme, baba yake. Lakini hakuwaua watoto wa wauaji; kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria za Mose, Mwenyezi-Mungu anapotoa amri akisema, “Wazazi hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya wazazi wao; bali kila mtu atauawa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.” Amazia aliwaua Waedomu 10,000 katika Bonde la Chumvi; aliutwaa kwa nguvu mji wa Sela na kuuita Yoktheeli, na hivi ndivyo unavyoitwa mpaka sasa.
2 Wafalme 14:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika mwaka wa pili wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. Naye alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na tisa katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, ila si kama babaye Daudi; akafanya kama yote aliyoyafanya baba yake Yoashi. Walakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu. Ikawa, mara ufalme ulipokuwa imara mkononi mwake, aliwaua watumishi wale waliomwua mfalme baba yake; ila hakuwaua watoto wa hao wauaji; kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Torati ya Musa, kama alivyoamuru BWANA, akisema, Mababa wasife kwa makosa ya wana, wala wana wasife kwa makosa ya mababa; lakini kila mtu atakufa kwa kosa lake mwenyewe. Akawaua Waedomi katika Bonde la Chumvi watu elfu kumi; akautwaa Sela vitani, akauita jina lake Yoktheeli hata leo.
2 Wafalme 14:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika mwaka wa pili wa utawala wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani, kutoka Yerusalemu. Akatenda yaliyo mema machoni pa BWANA, lakini sio kama Daudi baba yake alivyokuwa amefanya. Katika kila kitu alifuata mfano wa Yoashi baba yake. Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko. Baada ya ufalme kuimarika mikononi mwake, aliwaua maafisa waliomuua mfalme baba yake. Hata hivyo, hakuwaua wana wa wale wauaji, sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria ya Mose ambako BWANA aliamuru, “Baba hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto kwa ajili ya baba zao. Kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.” Ndiye aliwashinda Waedomu elfu kumi katika Bonde la Chumvi, na akauteka Sela katika vita, naye akauita Yoktheeli, jina ambalo mji huo unalo hadi leo.