Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 1:7-17

2 Wafalme 1:7-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfalme akauliza, “Ni mtu gani huyo aliyekutana nanyi na kuwaambieni mambo hayo?” Wao wakamjibu, “Alikuwa amevaa vazi la manyoya na mshipi wa ngozi kiunoni.” Mfalme akasema, “Huyo ni Elia kutoka Tishbe!” Hapo mfalme akamtuma kapteni mmoja na watu wake hamsini wamlete Elia. Kapteni huyo akamkuta Elia ameketi mlimani, akamwambia, “Ewe mtu wa Mungu, mfalme anakuamuru ushuke.” Elia akamjibu huyo kapteni wa watu hamsini, “Kama mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni na kukuteketeza wewe pamoja na watu wako!” Mara moto ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza pamoja na watu wake hamsini. Mfalme akamtuma kapteni mwingine na watu wake hamsini wamlete Elia. Naye akapanda juu akamwambia Elia, “Ewe mtu wa Mungu, mfalme anakuamuru ushuke mara moja!” Elia akamjibu, “Kama kweli mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe pamoja na watu wako!” Papo hapo moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza pamoja na watu wake hamsini. Kwa mara nyingine tena, mfalme akatuma kapteni mwingine na watu wake hamsini. Kapteni wa tatu akapanda mlimani, akapiga magoti mbele ya Elia na kumsihi akisema, “Ewe mtu wa Mungu, nakusihi uyathamini maisha yangu, na ya watu wako hawa, usituangamize! Maofisa wawili waliotangulia na watu wao, wameteketezwa na moto ulioshuka kutoka mbinguni; lakini sasa nakuomba uyahurumie maisha yangu.” Hapo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Elia, “Shuka pamoja naye, wala usimwogope.” Basi, Elia akainuka, akashuka pamoja naye mpaka kwa mfalme, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa sababu ulituma wajumbe kumtaka shauri Baal-zebubu, mungu wa Ekroni – kana kwamba hapakuwa na Mungu katika Israeli ambaye ungemwomba shauri – basi, hutashuka katika kitanda ulichopanda; hakika utakufa.’” Baadaye Ahazia akafariki kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia nabii wake Elia. Na, kwa kuwa Ahazia hakuwa na mtoto wa kiume, Yoramu akawa mfalme mahali pake, katika mwaka wa pili wa utawala wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati, mfalme wa Yuda.

2 Wafalme 1:7-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Akawaambia, Je! Mtu yule aliyetokea, akaonana nanyi, akawaambia maneno hayo, alikuwa mtu wa namna gani? Wakamwambia, Alikuwa amevaa vazi la manyoya, tena amejifunga shuka ya ngozi kiunoni mwake. Naye akasema, Ndiye yule Eliya Mtishbi. Ndipo mfalme akatuma kamanda wa askari hamsini pamoja na hamsini wake, wamwendee Eliya. Akamwendea, na tazama, ameketi juu ya kilima. Akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka. Eliya akajibu, akamwambia yule kamanda wa hamsini, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto ukashuka, ukamteketeza, yeye na hamsini wake. Akatuma tena kiongozi wa hamsini mwingine pamoja na hamsini wake, wamwendee. Akajibu, akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka upesi. Eliya akajibu, akamwambia, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza, yeye na hamsini wake. Tena akatuma kamanda wa hamsini wa tatu, pamoja na hamsini wake. Yule kamanda wa hamsini wa tatu akapanda, akaenda akapiga magoti mbele ya Eliya, akamsihi sana, akamwambia, Ee mtu wa Mungu, nakusihi, roho yangu, na roho za watumishi wako hawa hamsini, ziwe na thamani machoni pako. Tazama, moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawateketeza wale kamanda wa hamsini wawili wa kwanza pamoja na hamsini wao; laiti sasa roho yangu na iwe na thamani machoni pako. Malaika wa BWANA akamwambia Eliya, Shuka pamoja naye; usimwogope. Akaondoka, akashuka pamoja naye hadi kwa mfalme. Akamwambia, BWANA asema hivi, Kwa kuwa umetuma wajumbe waulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, je! Ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli, uulize neno lake? Kwa hiyo hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Basi akafa, sawasawa na neno la BWANA alilolinena Eliya. Na Yoramu alianza kutawala mahali pake katika mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda; kwa kuwa yeye hakuwa na mwana.

2 Wafalme 1:7-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Akawaambia, Je! Mtu yule aliyetokea, akaonana nanyi, akawaambia maneno hayo, alikuwa mtu wa namna gani? Wakamwambia, Alikuwa amevaa vazi la manyoya, tena amejifunga shuka ya ngozi kiunoni mwake. Naye akasema, Ndiye yule Eliya Mtishbi. Ndipo mfalme akatuma akida wa askari hamsini pamoja na hamsini wake, wamwendee Eliya. Akamwendea, na tazama, ameketi juu ya kilima. Akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka. Eliya akajibu, akamwambia yule akida wa hamsini, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto ukashuka, ukamteketeza, yeye na hamsini wake. Akatuma tena akida wa hamsini mwingine pamoja na hamsini wake, wamwendee. Akajibu, akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka upesi. Eliya akajibu, akamwambia, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza, yeye na hamsini wake. Tena akatuma akida wa hamsini wa tatu, pamoja na hamsini wake. Yule akida wa hamsini wa tatu akapanda, akaenda akapiga magoti mbele ya Eliya, akamsihi sana, akamwambia, Ee mtu wa Mungu, nakusihi, roho yangu, na roho za watumishi wako hawa hamsini, ziwe na thamani machoni pako. Tazama, moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawateketeza wale akida wa hamsini wawili wa kwanza pamoja na hamsini wao; laiti sasa roho yangu na iwe na thamani machoni pako. Malaika wa BWANA akamwambia Eliya, Shuka pamoja naye; usimwogope. Akaondoka, akashuka pamoja naye hata kwa mfalme. Akamwambia, BWANA asema hivi, Kwa kuwa umetuma wajumbe waulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, uulize neno lake? Kwa hiyo hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Basi akafa, sawasawa na neno la BWANA alilolinena Eliya. Na Yoramu alianza kutawala mahali pake katika mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda; kwa kuwa yeye hakuwa na mwana.

2 Wafalme 1:7-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mfalme akawauliza, “Alikuwa mtu wa namna gani ambaye mlikutana naye, akawaambia hili?” Wakamjibu, “Alikuwa mtu aliyekuwa na vazi la manyoya na mkanda wa ngozi kiunoni mwake.” Mfalme akasema, “Huyo alikuwa ni Eliya, Mtishbi.” Ndipo mfalme akamtuma mkuu mmoja wa kikosi pamoja na kikosi chake cha askari hamsini kwa nabii Eliya. Yule mkuu wa kikosi akamwendea Eliya, aliyekuwa ameketi juu ya kilima, na kumwambia, “Mtu wa Mungu, mfalme anasema, ‘Shuka chini!’ ” Eliya akamjibu yule mkuu wa kikosi, “Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni ukuteketeze wewe na watu wako hamsini!” Ndipo moto ukashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza yule mkuu wa kikosi pamoja na watu wake. Aliposikia hili, mfalme akatuma kwa Eliya mkuu wa kikosi mwingine na askari wake hamsini. Yule mkuu wa kikosi akamwambia Eliya, “Mtu wa Mungu, hili ndilo asemalo mfalme, ‘Shuka chini mara moja!’ ” Eliya akajibu, “Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni ukuteketeze wewe na watu wako hamsini!” Ndipo moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza yeye na watu wake hamsini. Hivyo mfalme akatuma mkuu wa kikosi wa tatu na watu wake hamsini. Huyu mkuu wa kikosi wa tatu akapanda na kupiga magoti mbele ya Eliya, akiomba, “Mtu wa Mungu, tafadhali niachie uhai wangu na uhai wa hawa watu hamsini, watumishi wako! Tazama, moto umeshuka kutoka mbinguni na kuwateketeza wale wakuu wa vikosi viwili vya kwanza pamoja na watu wao. Lakini sasa niachie uhai wangu!” Malaika wa BWANA akamwambia Eliya, “Shuka pamoja naye, usimwogope.” Hivyo Eliya akainuka na kushuka pamoja naye kwa mfalme. Akamwambia mfalme, “Hili ndilo asemalo BWANA: Je, ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli wa kumuuliza habari, ndiyo maana ukatuma wajumbe kuuliza Baal-Zebubu, mungu wa Ekroni? Kwa sababu umefanya hili, kamwe hutaondoka kwenye kitanda unachokilalia. Hakika utakufa!” Hivyo akafa, sawasawa na lile neno la BWANA ambalo Eliya alikuwa amesema. Kwa kuwa Ahazia hakuwa na mwana, Yoramu akawa mfalme baada yake katika mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda.