2 Wakorintho 9:1-15
2 Wakorintho 9:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Si lazima kuandika zaidi kuhusu huduma yenu hiyo kwa ajili ya watu wa Mungu. Ninajua jinsi mlivyo na moyo wa kusaidia, na nilijivuna juu yenu kuhusu jambo hilo mbele ya watu wa Makedonia. Niliwaambia: “Ndugu zetu wa Akaya wako tayari tangu mwaka jana.” Hivyo, moto wenu umekwisha wahimiza watu wengi zaidi. Basi, nimewatuma ndugu zetu hao, ili fahari yetu juu yenu ionekane kwamba si maneno matupu, na kwamba mko tayari kabisa na msaada wenu kama nilivyosema. Isije ikawa kwamba watu wa Makedonia watakapokuja pamoja nami tukawakuta hamko tayari, hapo sisi tutaaibika – bila kutaja aibu mtakayopata nyinyi wenyewe – kwa sababu tutakuwa tumewatumainia kupita kiasi. Kwa hiyo, nimeona ni lazima kuwaomba hawa ndugu watutangulie kuja kwenu, wapate kuweka tayari zawadi yenu kubwa mliyoahidi; nayo ioneshe kweli kwamba ni zawadi iliyotolewa kwa hiari na si kwa kulazimishwa. Kumbukeni: “Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye kwa wingi huvuna kwa wingi.” Kila mmoja, basi, na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha. Mungu anaweza kuwapeni nyinyi zaidi ya yale mnayoyahitaji, mpate daima kuwa na kila kitu mnachohitaji, na hivyo mzidi kusaidia katika kila kazi njema. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Yeye hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini; wema wake wadumu milele.” Na Mungu ampaye mkulima mbegu na mkate kwa chakula, atawapa nyinyi pia mbegu mnazohitaji, na atazifanya ziote, zikue na kuwapa mavuno mengi ya ukarimu wenu. Yeye atawatajirisha nyinyi daima kwa kila kitu, ili watu wapate kumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi zenu wanazozipokea kwa mikono yetu. Maana huduma hii takatifu mnayoifanya si kwamba itasaidia mahitaji ya watu wa Mungu tu, bali pia itasababisha watu wengi wamshukuru Mungu. Kutokana na uthibitisho unaooneshwa kwa huduma hii yetu, watu watamtukuza Mungu kwa sababu ya uaminifu wenu kwa Habari Njema ya Kristo mnayoiungama, na pia kwa sababu ya ukarimu mnaowapa wao na watu wote. Kwa hiyo watawaombea nyinyi kwa moyo kwa sababu ya neema ya pekee aliyowajalieni Mungu. Tumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi yake isiyo na kifani!
2 Wakorintho 9:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kuhusu kuwahudumia watakatifu sina haja ya kuwaandikia. Maana najua utayari wenu, ninaojisifia kwa ajili yenu kwa Wamakedonia, kwamba Akaya ilikuwa tayari tangu mwaka mzima; na bidii yenu imewatia moyo wengi wao. Lakini niliwatuma hao ndugu, ili kujisifu kwetu kwa ajili yenu kusibatilike katika jambo hili; mpate kuwa tayari, kama nilivyosema; kusudi, wakija Wamakedonia pamoja nami, na kuwakuta hamjawa tayari, tusije tukatahayarika sisi, (tusiseme ninyi), katika hali hiyo ya kutumaini. Basi niliona ya kuwa ni lazima niwaonye ndugu hawa watangulie kufika kwenu, na kutengeneza mapema karama yenu mliyoahidi tangu zamani, ili iwe tayari, na hivi iwe kama kipawa, wala si kama kitu kitolewacho kwa nguvu. Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, Haki yake yakaa milele. Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu; mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu. Maana utumishi wa huduma hii hauwatimizii watakatifu riziki walizopungukiwa tu, bali huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu; kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo, wanamtukuza Mungu kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili ya Kristo, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote. Nao wenyewe, wakiomba dua kwa ajili yenu, wawaonea shauku kwa sababu ya neema ya Mungu iliyozidi sana ndani yenu. Mungu ashukuriwe kwa sababu ya kipawa chake, tusichoweza kukisifu kama ipasavyo.
2 Wakorintho 9:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa habari za kuwahudumia watakatifu sina haja ya kuwaandikia. Maana najua utayari wenu, ninaojisifia kwa ajili yenu kwa Wamakedonia, kwamba Akaya ilikuwa tayari tangu mwaka mzima; na bidii yenu imewatia moyo wengi wao. Lakini naliwatuma hao ndugu, ili kujisifu kwetu kwa ajili yenu kusibatilike katika jambo hili; mpate kuwa tayari, kama nilivyosema; kusudi, wakija Wamakedonia pamoja nami, na kuwakuta hamjawa tayari, tusije tukatahayarika sisi, (tusiseme ninyi), katika hali hiyo ya kutumaini. Basi naliona ya kuwa ni lazima niwaonye ndugu hawa watangulie kufika kwenu, na kutengeneza mapema karama yenu mliyoahidi tangu zamani, ili iwe tayari, na hivi iwe kama kipawa, wala si kama kitu kitolewacho kwa unyimivu. Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, Haki yake yakaa milele. Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu; mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu. Maana utumishi wa huduma hii hauwatimizii watakatifu riziki walizopungukiwa tu, bali huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu; kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo, wanamtukuza Mungu kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili ya Kristo, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote. Nao wenyewe, wakiomba dua kwa ajili yenu, wawaonea shauku kwa sababu ya neema ya Mungu iliyozidi sana ndani yenu. Mungu ashukuriwe kwa sababu ya kipawa chake, tusichoweza kukisifu kama ipasavyo.
2 Wakorintho 9:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hakuna haja yangu kuwaandikia kuhusu huduma hii itolewayo kwa ajili ya watakatifu. Kwa kuwa ninajua mlivyo na shauku ya kusaidia, nami nimekuwa nikijivuna kwa ajili ya jambo hilo kwa watu wa Makedonia, nikiwaambia kuwa ninyi wa Akaya mmekuwa tayari kutoa tangu mwaka jana na shauku yenu imewachochea wengi wao katika kutoa. Lakini sasa nawatuma hawa ndugu ili kujivuna kwetu kuhusu mchango wenu kusiwe maneno matupu, bali mpate kuwa tayari kama nilivyosema mngekuwa tayari. Kwa maana kama nikija na Mmakedonia yeyote na kuwakuta hamjawa tayari, tutaona aibu kusema chochote juu yenu katika matoleo. Kwa hivyo niliona ni muhimu niwahimize hawa ndugu watangulie kuja huko kwenu kabla yangu, wafanye mipango ya hayo matoleo ya ukarimu mliyokuwa mmeahidi, ili yawe tayari kama matoleo ya hiari wala si kama ya kutozwa kwa nguvu. Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema. Kama ilivyoandikwa: “Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini; haki yake hudumu milele.” Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu. Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu, ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani. Huduma hii mnayofanya si tu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watakatifu, bali huzidi sana kwa shukrani nyingi apewazo Mungu. Kwa sababu ya huduma ambayo mmejithibitisha wenyewe, watu watamtukuza Mungu kwa ajili ya utiifu ufuatanao na ukiri wenu wa Injili ya Kristo, na kwa ukarimu wenu wa kushiriki pamoja nao na pia wengine wote. Nao katika maombi yao kwenu mioyo yao itawaonea shauku kwa sababu ya neema ipitayo kiasi mliyopewa na Mungu. Ashukuriwe Mungu kwa karama yake isiyoelezeka.