2 Wakorintho 8:1-5
2 Wakorintho 8:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu, tunapenda kuwapa habari juu ya neema ambazo Mungu ameyajalia makanisa ya Makedonia. Waumini wa huko walijaribiwa sana kwa taabu; lakini furaha yao ilikuwa kubwa hivi hata wakawa wakarimu kupita kiasi, ingawaje walikuwa maskini sana. Naweza kushuhudia kwamba walikuwa wakarimu kadiri ya nguvu zao na hata zaidi. Kwa hiari yao wenyewe, walitusihi sana wapewe nafasi ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watu wa Mungu. Hilo lilikuwa jambo ambalo hatukulitazamia kabisa! Kwanza walijitolea wao wenyewe kwa Bwana, kisha wakajitolea wenyewe kwetu pia, kufuatana na mapenzi ya Mungu.
2 Wakorintho 8:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia; maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao. Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana pamoja na kutusihi kuhusu neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu. Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu.
2 Wakorintho 8:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia; maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao. Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu. Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu.
2 Wakorintho 8:1-5 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi sasa ndugu, nataka ninyi mjue kuhusu ile neema ambayo Mungu amewapa makanisa ya Makedonia. Pamoja na majaribu makali na taabu walizopata, furaha waliyokuwa nayo ilikuwa kubwa, ingawa walikuwa maskini kupindukia, kwa upande wao walifurika kwa wingi wa ukarimu. Kwa maana nashuhudia kwamba wao walitoa kwa kadiri wawezavyo, hata na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe, wakitusihi kwa bidii wapewe fursa ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watakatifu. Wala hawakufanya tulivyotazamia, bali walijitoa wao wenyewe kwa Bwana kwanza na ndipo wakajitoa kwa ajili yetu, kufuatana na mapenzi ya Mungu.