2 Wakorintho 7:10-13
2 Wakorintho 7:10-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa maana huzuni ya kimungu huleta toba iletayo wokovu na wala haina majuto. Lakini huzuni ya kidunia husababisha mauti. Tazameni jinsi huzuni hii ya kimungu ilivyoleta faida ndani yenu: bidii mliyo nayo, juhudi mliyofanya kujitetea, uchungu wenu, hofu yenu, upendo wenu, shauku yenu na jinsi mlivyokuwa tayari kutoa adhabu inayostahili. Kwa kila njia mmejithibitisha kuwa safi katika jambo hilo. Hivyo ingawa niliwaandikia, haikuwa kwa sababu ya huyo aliyekosa au huyo aliyekosewa. Lakini nilitaka ninyi wenyewe mwone, mbele za Mungu, jinsi mlivyojitoa kwa ajili yetu. Kwa ajili ya haya tumefarijika. Zaidi ya kule sisi kutiwa moyo, tulifurahi sana kumwona Tito alivyo na furaha, kwa sababu roho yake imeburudishwa na ninyi nyote.
2 Wakorintho 7:10-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Kuwa na huzuni jinsi atakavyo Mungu husababisha badiliko la moyo, badiliko lenye kuleta wokovu; hivyo hakuna sababu ya kujuta. Lakini huzuni ya kidunia huleta kifo. Sasa mnaweza kuona matokeo ya kuona huzuni jinsi Mungu atakavyo: Nyinyi mmepata kuwa sasa watu wenye jitihada, wenye hoja, mnashtuka na kuogopa, mna bidii na mko tayari kuona kwamba haki yatekelezwa. Nyinyi mmethibitisha kwa kila njia kwamba hamna hatia kuhusu jambo hili. Hivyo, ingawa niliandika ile barua, haikuwa kwa ajili ya yule aliyekosa, au kwa ajili ya yule aliyekosewa. Niliandika kusudi ionekane wazi mbele ya Mungu jinsi mlivyo na bidii kwa ajili yetu. Ndiyo maana sisi tulifarijika sana. Siyo kwamba tulifarijika tu, ila pia Tito alitufurahisha kwa furaha aliyokuwa nayo kutokana na jinsi mlivyomchangamsha moyo.
2 Wakorintho 7:10-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba iletayo wokovu isiyo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti. Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii gani ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo. Basi, ijapokuwa niliwaandikia, sikuandika kwa ajili yake yeye aliyedhulumu, wala si kwa ajili yake yeye aliyedhulumiwa, bali ili bidii yenu kwa ajili yetu ipate kudhihirishwa kwenu mbele za Mungu. Kwa hiyo tulifarijiwa. Tena katika kufarijiwa kwetu tulifurahi sana kupita kiasi kwa sababu ya furaha ya Tito; maana roho yake imeburudishwa na ninyi nyote.
2 Wakorintho 7:10-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti. Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii kama nini ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionyesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo. Basi, ijapokuwa naliwaandikia, sikuandika kwa ajili yake yeye aliyedhulumu, wala si kwa ajili yake yeye aliyedhulumiwa, bali bidii yenu kwa ajili yetu ipate kudhihirishwa kwenu mbele za Mungu. Kwa hiyo tulifarijiwa. Tena katika kufarijiwa kwetu tulifurahi sana kupita kiasi kwa sababu ya furaha ya Tito; maana roho yake imeburudishwa na ninyi nyote.