Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wakorintho 3:6-18

2 Wakorintho 3:6-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Maana yeye ndiye aliyetuwezesha kulihudumia Agano Jipya ambalo si agano la sheria iliyoandikwa, bali agano la Roho. Maana sheria iliyoandikwa huleta kifo, lakini Roho huleta uhai. Sheria iliwekwa kwa kuandikwa juu ya vipande vya mawe. Ingawaje mwisho wake umekuwa kifo, utukufu wake ulikuwa mkuu mno hata wana wa Israeli wasiweze kuutazama uso wa Mose kwa sababu ya mngao wake. Tena mngao huo ulikuwa wa muda tu. Basi, ikiwa huduma ya kile ambacho kimesababisha kifo imefanyika kwa utukufu mwingi kiasi hicho, basi, huduma ya Roho ina utukufu mkuu zaidi. Ikiwa basi, kulikuwa na utukufu katika huduma ile iliyoleta hukumu, ni wazi kwamba huduma iletayo uadilifu itakuwa na utukufu mkuu zaidi. Sasa utukufu mkuu zaidi umechukua nafasi ya ule utukufu uliokuja hapo awali, ambao fahari yake imekwisha toweka. Maana ikiwa kile kilichokuwa cha muda tu kilikuwa na utukufu wake, bila shaka kile chenye kudumu milele kitakuwa na utukufu mkuu zaidi. Kwa vile hili ndilo tumaini letu, sisi twasema kwa uhodari mkuu. Sisi hatufanyi kama Mose ambaye alilazimika kuufunika uso wake kwa kitambaa ili watu wa Israeli wasiuone ule mwisho wa mngao ule uliokuwa unafifia. Lakini akili zao zilipumbazwa. Mpaka leo hii lisomwapo Agano la Kale, kifuniko hicho bado kipo. Kifuniko hicho kitaondolewa tu mtu anapoungana na Kristo. Naam, mpaka hivi leo kila isomwapo sheria akili zao huwa zimefunikwa. Lakini, wakati mtu amgeukiapo Bwana, kifuniko hicho huondolewa. Hapa “Bwana” ni Roho; na pale alipo Roho wa Bwana ndipo ulipo uhuru. Basi, sisi sote ambao nyuso zetu hazikufunikwa, tunaona kama katika kioo, utukufu wa Bwana; tunabadilishwa tufanane zaidi na huo mfano wake kwa utukufu mwingi zaidi. Hiyo ni kazi yake Roho wa Bwana.

2 Wakorintho 3:6-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha. Basi, ikiwa huduma ya mauti, iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika; je! Huduma ya roho haitazidi kuwa katika utukufu? Kwa maana ikiwa huduma ya adhabu ina utukufu, seuze huduma ya haki ina utukufu unaozidi. Maana hata ile iliyotukuzwa haikuwa na utukufu hivi, kwa sababu ya utukufu uzidio sana. Kwa maana, ikiwa ile inayobatilika ilikuwa na utukufu, zaidi sana ile idumuyo ina utukufu. Basi, kwa kuwa mna tumaini la namna hii, twatumia ujasiri mwingi; nasi si kama Musa alivyotia utaji juu ya uso wake, ili kwamba Waisraeli wasitazame sana mwisho wa ile iliyokuwa ikibatilika; ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi, wakati lisomwapo Agano la Kale, utaji uo huo wakaa; yaani, haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo; ila hata leo, Torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao. Lakini wakati wowote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa. Basi “Bwana” ndiye Roho; lakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru. Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.

2 Wakorintho 3:6-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha. Basi, ikiwa huduma ya mauti, iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika; je! Huduma ya roho haitazidi kuwa katika utukufu? Kwa maana ikiwa huduma ya adhabu ina utukufu, siuze huduma ya haki ina utukufu unaozidi. Maana hata ile iliyotukuzwa haikuwa na utukufu hivi, kwa sababu ya utukufu uzidio sana. Kwa maana, ikiwa ile inayobatilika ilikuwa na utukufu, zaidi sana ile ikaayo ina utukufu. Basi, kwa kuwa mna taraja la namna hii, twatumia ujasiri mwingi; nasi si kama Musa alivyotia utaji juu ya uso wake, ili kwamba Waisraeli wasitazame sana mwisho wa ile iliyokuwa ikibatilika; ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi, wakati lisomwapo Agano la Kale, utaji uo huo wakaa; yaani, haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo; ila hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao. Lakini wakati wo wote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa. Basi “Bwana” ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru. Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.

2 Wakorintho 3:6-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndiye alituwezesha sisi kuwa wahudumu wa Agano Jipya: si wa andiko, bali wa Roho; kwa kuwa andiko huua bali Roho hutia uzima. Basi ikiwa ile huduma iliyoleta mauti, iliyoandikwa kwa herufi juu ya jiwe ilikuja kwa utukufu, hata Waisraeli wakawa hawawezi kuutazama uso wa Mose kwa sababu ya ule utukufu wake ingawa ulikuwa ni wa kufifia, je, huduma ya Roho haitakuwa na utukufu zaidi? Ikiwa huduma ile inayowahukumu wanadamu ina utukufu, je, ile huduma iletayo haki haitakuwa ya utukufu zaidi? Kwa maana kile kilichokuwa na utukufu sasa hakina utukufu ukilinganisha na huu utukufu unaozidi wa Agano Jipya. Ikiwa kile kilichokuwa kinafifia kilikuja kwa utukufu, je, si zaidi utukufu wa kile kinachodumu? Kwa hiyo, kwa kuwa tunalo tumaini hili, tuna ujasiri sana. Sisi si kama Mose, ambaye ilimpasa kuweka utaji ili kufunika uso wake ili Waisraeli wasiuone ule mngʼao uliokuwa juu yake hadi ulipofifia na hatimaye kutoweka. Lakini akili zao zilipumbazwa, kwa maana mpaka leo utaji ule ule hufunika wakati Agano la Kale linasomwa. Huo utaji haujaondolewa, kwa maana ni katika Kristo peke yake unaondolewa. Hata leo Sheria ya Mose inaposomwa, utaji hufunika mioyo yao. Lakini wakati wowote mtu anapomgeukia Bwana, utaji unaondolewa. Basi Bwana ndiye Roho. Mahali alipo Roho wa Bwana hapo pana uhuru. Nasi sote, tukiwa na nyuso zisizotiwa utaji tunadhihirisha utukufu wa Bwana, kama kwenye kioo. Nasi tunabadilishwa ili tufanane naye, toka utukufu hadi utukufu mkuu zaidi, utokao kwa Bwana, ambaye ndiye Roho.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha