2 Wakorintho 12:2-10
2 Wakorintho 12:2-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Namjua mtu mmoja Mkristo, ambaye miaka kumi na minne iliyopita alinyakuliwa mpaka katika mbingu ya tatu. (Sijui kama alikuwa huko kwa mwili au kwa roho; Mungu ajua). Narudia: Najua kwamba mtu huyo alinyakuliwa mpaka peponi. (Lakini sijui kama alikuwa huko kwa mwili au kwa roho; Mungu ajua). Huko akasikia mambo ya siri ambayo binadamu hastahili kuyatamka. Basi, nitajivunia juu ya mtu wa namna hiyo, na si juu yangu mimi binafsi, isipokuwa tu juu ya udhaifu wangu. Kama ningetaka kujivuna singekuwa mpumbavu hata kidogo, maana ningekuwa nasema ukweli tupu. Lakini sitajivuna; sipendi mtu anifikirie zaidi ya vile anavyoona na kusikia kutoka kwangu. Lakini, kusudi mambo haya makuu niliyofunuliwa yasinifanye nilewe majivuno, nilipewa maumivu mwilini kama mwiba, mjumbe wa Shetani mwenye kunipiga, nisijivune kupita kiasi. Nilimsihi Bwana mara tatu kuhusu jambo hili ili linitoke. Lakini akaniambia: “Neema yangu inatosha kwa ajili yako; maana uwezo wangu hukamilishwa zaidi katika udhaifu.” Basi, ni radhi kabisa kujivunia udhaifu wangu ili uwezo wake Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo nakubali kwa radhi udhaifu, dharau, taabu, udhalimu na mateso, kwa ajili ya Kristo; maana ninapokuwa dhaifu, ndipo ninapokuwa na nguvu.
2 Wakorintho 12:2-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu. Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua); ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haistahili mwanadamu ayaseme. Kuhusu mtu kama huyo nitajisifu; lakini kwa ajili ya nafsi yangu sitajisifu, isipokuwa kuhusu udhaifu wangu. Maana kama ningetaka kujisifu singekuwa mpumbavu, kwa sababu nitasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu asinihesabie zaidi ya hayo ayaonayo kwangu au kuyasikia kwangu. Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nilipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nilimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na matusi, na matatizo, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.
2 Wakorintho 12:2-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu. Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua); ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene. Kwa habari za mtu kama huyo nitajisifu; lakini kwa ajili ya nafsi yangu sitajisifu, isipokuwa katika habari ya udhaifu wangu. Maana kama ningetaka kujisifu singekuwa mpumbavu, kwa sababu nitasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu asinihesabie zaidi ya hayo ayaonayo kwangu au kuyasikia kwangu. Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.
2 Wakorintho 12:2-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Namjua mtu mmoja katika Kristo ambaye miaka kumi na minne iliyopita alichukuliwa juu hadi mbingu ya tatu. Kama ni katika mwili au nje ya mwili, sijui, Mungu ajua. Nami najua ya kwamba mtu huyu, kwamba ni katika mwili au nje ya mwili mimi sijui, lakini Mungu ajua, alinyakuliwa hadi Paradiso. Huko alisikia mambo yasiyoelezeka, mambo ambayo binadamu hana ruhusa ya kuyasimulia. Nitajisifu kwa ajili ya mtu kama huyo, lakini sitajisifu kuhusu mimi mwenyewe ila mimi nitajisifia udhaifu wangu. Hata kama ningependa kujisifu, sitakuwa mjinga, kwa maana nitakuwa nasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu yeyote asije akaniona mimi kuwa bora zaidi kuliko ninavyoonekana katika yale ninayotenda na kusema. Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.