2 Wakorintho 11:1-6
2 Wakorintho 11:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Laiti mngenivumilia kidogo, hata kama mimi ni mjinga kiasi! Naam, nivumilieni kidogo. Ninawaoneeni wivu lakini ni wivu wa Mungu; maana nyinyi ni kama bikira safi niliyemposa kwa mwanamume mmoja tu ambaye ndiye Kristo. Lakini naogopa kwamba, kama vile yule nyoka kwa hila zake za uongo alimdanganya Hawa, fikira zenu zaweza kupotoshwa, mkauacha uaminifu wenu wa kweli kwa Kristo. Maana mtu yeyote ajaye na kumhubiri Yesu aliye tofauti na yule tuliyemhubiri, nyinyi mwampokea kwa mikono miwili; au mnakubali roho au Injili tofauti kabisa na ile mliyopokea kutoka kwetu! Sidhani kwamba mimi ni mdogo kuliko hao “mitume wakuu.” Labda sina ufasaha wa lugha, lakini elimu ninayo; jambo hili tumelionesha wazi kwenu, kila mahali na kila wakati.
2 Wakorintho 11:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Laiti mngechukuliana nami katika upumbavu wangu kidogo! Naam, mchukuliane nami. Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa niliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi. Lakini nahofu; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo. Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au Injili nyingine msiyoikubali, mnavumiliana naye punde! Maana nadhani ya kuwa mimi sikupungukiwa na kitu walicho nacho mitume walio wakuu. Lakini nijapokuwa mimi ni mtu asiyejua kunena, hii si hali yangu katika elimu; ila katika kila neno tumedhihirishwa kwenu.
2 Wakorintho 11:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Laiti mngechukuliana nami katika upumbavu wangu kidogo! Naam, mchukuliane nami. Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi. Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo. Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye! Maana nadhani ya kuwa mimi sikupungukiwa na kitu walicho nacho mitume walio wakuu. Lakini nijapokuwa mimi ni mtu asiyejua kunena, hii si hali yangu katika elimu; ila katika kila neno tumedhihirishwa kwenu.
2 Wakorintho 11:1-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Laiti mngenivumilia kidogo katika upumbavu wangu! Naam, nivumilieni kidogo. Ninawaonea wivu, wivu wa Kimungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Kristo kama mabikira safi. Lakini nina hofu kuwa, kama vile Eva alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo. Kwa sababu kama mtu akija na kuwahubiria Yesu mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au kama mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au Injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi. Lakini sidhani ya kuwa mimi ni dhalili sana kuliko hao “mitume wakuu.” Inawezekana mimi nikawa si mnenaji hodari, lakini ni hodari katika elimu. Jambo hili tumelifanya liwe dhahiri kwenu kwa njia zote.