2 Mambo ya Nyakati 9:1-7
2 Mambo ya Nyakati 9:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Malkia wa Sheba aliposikia sifa za Solomoni, aliwasili Yerusalemu ili kumjaribu Solomoni kwa maswali magumu. Alifuatana na msafara wa watu, pamoja na ngamia waliobeba manukato, dhahabu nyingi sana na vito vya thamani. Na alipofika kwa Solomoni, alimwuliza maswali yote aliyokuwa nayo moyoni mwake. Solomoni aliyajibu maswali yote; hapakuwapo na jambo lolote aliloshindwa kumweleza. Malkia wa Sheba alipoiona hekima ya Solomoni na nyumba aliyokuwa ameijenga, tena alipotazama chakula kilichoandaliwa mezani pwake na kuona jinsi maofisa wake walivyoketi mezani na huduma ya watumishi wake na jinsi walivyovalia; pia wanyweshaji wake na jinsi walivyovalia, tambiko za kuteketeza ambazo alizitoa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, alipoona hayo yote akashangaa sana. Basi, akamwambia mfalme, “Yote niliyosikia nchini kwangu kuhusu kazi zako na hekima yako ni ya kweli! Lakini sikuweza kuamini habari zao mpaka nilipofika na kujionea mwenyewe, na kumbe niliambiwa nusu tu; hekima yako na ufanisi wako ni zaidi ya yale niliyosikia. Wana bahati wake zako! Wana bahati hawa watumishi wako ambao daima husimama mbele yako na kusikiliza hekima yako!
2 Mambo ya Nyakati 9:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani, alikuja ili amjaribu Sulemani kwa maswali ya fumbo huko Yerusalemu, mwenye wafuasi wengi, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akamwambia mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala halikuwako neno alilofichiwa Sulemani, asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima ya Sulemani, na nyumba aliyoijenga, na vyakula vya mezani mwake, na kikao cha watumishi wake, na usimamizi wao wangoje wake, na mavazi yao; na wanyweshaji wake, na mavazi yao; na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya BWANA; roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako.
2 Mambo ya Nyakati 9:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Solomoni, huyo malkia akaja Yerusalemu kumjaribu kwa maswali magumu. Alifika akiwa na msafara mkubwa sana, pamoja na ngamia waliobeba vikolezi, kiasi kikubwa cha dhahabu na vito vya thamani, alikuja kwa Solomoni na kuzungumza naye kuhusu yote ambayo alikuwa nayo moyoni mwake. Solomoni akamjibu maswali yake yote, wala hakukuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwake asiweze kumwelezea. Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Solomoni na jumba la kifalme alilokuwa amejenga, chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika Hekalu la BWANA alipatwa na mshangao. Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli. Lakini sikuamini yaliyosemwa hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana kuliko ile taarifa niliyoisikia. Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wasimamao mbele yako daima na kusikia hekima yako!
2 Mambo ya Nyakati 9:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na malkia wa Sheba aliposikia sifa za Sulemani, alikuja ili amjaribu Sulemani kwa maswali ya fumbo huko Yerusalemu, akiwa na wafuasi wengi, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikia Sulemani, akamwambia mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala halikuwako neno alilofichiwa Sulemani, asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima ya Sulemani, na nyumba aliyoijenga, na vyakula vya mezani mwake, na kikao cha maofisa wake, na huduma ya watumishi wake na mavazi yao; pia wanyweshaji wake na mavazi yao; na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya BWANA; roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Habari zile nilizozisikia katika nchi yangu zihusuzo mambo yako na hekima yako ni za kweli. Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako.