Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mambo ya Nyakati 6:1-42

2 Mambo ya Nyakati 6:1-42 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo Sulemani akanena, BWANA alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Lakini nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele. Mfalme akageukia mkutano wote wa Israeli akawabariki, mkutano wote wa Israeli ukiwa umesimama. Akasema, BWANA, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenena kwa kinywa chake na baba yangu Daudi, akalitimiza kwa mikono yake, akasema, Tangu siku ile nilipowatoa watu wangu katika nchi ya Misri, sikuchagua mji wowote wa kabila zote za Israeli ili kujenga nyumba, jina langu liwe humo; wala sikumchagua mtu yeyote awe mkuu juu ya watu wangu Israeli; lakini nimeuchagua Yerusalemu, jina langu liwe humo; na Daudi nimemchagua awe juu ya watu wangu Israeli. Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako; lakini si wewe utakayeijenga nyumba hiyo; ila mwanao atakayetoka katika uzao wako, yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu. Basi BWANA amelitimiza neno lile alilolinena; nami nimesimama mahali pa Daudi baba yangu, na kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, kama BWANA alivyoahidi, nami nimeijenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Ndimo nilimoliweka hilo sanduku, ambalo ndani yake mna agano la BWANA, alilolifanya na wana wa Israeli. Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akainyosha mikono; (maana Sulemani alikuwa amefanya mimbari ya shaba, urefu wake dhiraa tano, na upana wake dhiraa tano, na kwenda juu kwake dhiraa tatu, na kuisimamisha katikati ya ua; akasimama juu yake, akapiga magoti mbele ya mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake kuelekea mbinguni); akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni, wala duniani; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa moyo wao wote; uliyemtimizia mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidi; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo. Sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, umtimizie mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu machoni pangu, wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli; wakiwa tu watoto wako wataiangalia njia yao, ili kuiendea torati yangu, kama wewe ulivyokwenda mbele zangu. Basi sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako Daudi. Lakini Mungu je! Yamkini atakaa na watu duniani? Tazama, mbingu na mbingu za mbingu za mbingu hazikutoshi; seuze nyumba hii niliyoijenga! Walakini umwangalie mtumishi wako anayoyaomba, na kusihi, Ee BWANA, Mungu wangu, usikie kilio na maombi anayoyaomba mtumishi wako mbele zako; ili macho yako yafumbuke kwa nyumba hii mchana na usiku, mahali uliponena, ndipo utakapoliweka jina lako; usikie maombi atakayoomba mtumishi wako, akikabili mahali hapa. Uyasikie atakayosihi mtumishi wako, na watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, usikie toka makaoni mwako, toka mbinguni, nawe usikiapo, samehe. Ikiwa mtu amemkosea mwenzake, akitiwa kiapo, aapishwe, naye akija na kuapa hapa mbele ya madhabahu yako nyumbani humu; basi, usikie mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumishi wako; ukimlipiza mwovu, kumpatilizia njia yake kichwani; ukamfanyie haki mwenye haki, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake. Ikiwa watu wako Israeli wamepigwa mbele ya adui zao, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakirejea kwako, na kulikiri jina lako, wakikuomba na kukusihi nyumbani humu; basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watu wako Israeli, na kuwarejeza tena katika nchi uliyowapa wao na baba zao. Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, uwatesapo; basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumishi wako, na ya watu wako Israeli; uwafundishapo njia njema iwapasayo waiendee; ukainyeshee mvua nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi. Ikiwa nchi imeingia njaa, au tauni, au ukame, au ukungu, au nzige, au panzi; ikiwa adui wamewahusuru katika nchi ya miji yao, au ukiwapo msiba wowote, au ugonjwa wowote; yoyote atakayoyaomba na kusihi mtu awaye yote, au watu wako Israeli wote pamoja, watakaojua kila mtu pigo lake mwenyewe, na msiba wake mwenyewe, akiinyoshea mikono nyumba hii; basi usikie huko mbinguni, ukaapo, ukasamehe, ukampatilize kila mtu kwa kadiri ya njia zake zote; wewe umjuaye moyo; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu); ili wakuche wewe, waziendee njia zako, siku zote watakazoishi katika nchi uliyowapa baba zetu. Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako kuu, na mkono wako ulio hodari, na mkono wako ulionyoshwa; hao watakapokuja na kuomba wakiielekea nyumba hii; basi usikie huko mbinguni, toka makaoni mwako, ukatende yote atakayokuomba huyo mgeni; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe, kama watu wako Israeli, tena wajue ya kuwa nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa jina lako. Ikiwa watu wako wametoka kupigana na adui zao, utakakowatuma kokote, wakikuomba kuuelekea mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako; basi uyasikie huko mbinguni wayaombayo, na kusihi, ukaitetee haki yao. Wakikukosa, (maana hakuna mtu asiyekosa), hata uwakasirikie, na kuwatia mikononi mwa adui zao, wawahamishe, na kuwachukua mateka mpaka nchi iliyo mbali au iliyo karibu; basi wakikumbuka katika nchi walikohamishwa, na kutubu, na kukusihi katika nchi ya uhamisho wao, wakisema, Tumekosa, tumetenda kwa ukaidi, tumefanya maovu; wakurudiapo kwa mioyo yao yote, na kwa nia zao zote, katika nchi ya uhamisho wao, adui walikowahamisha, wakiomba na kuielekea nchi uliyowapa baba zao, na mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako; basi uyasikie toka mbinguni, toka makaoni mwako, wayaombayo, na kusihi, ukaitetee haki yao; ukawasamehe watu wako, waliokosa juu yako. Na sasa, Ee Mungu wangu, macho yako yafumbuke, nakusihi, masikio yako yakasikilize maombi yaombwayo mahali hapa. Sasa, Ee BWANA, Mungu, uondoke, uende kwenye raha yako, wewe na sanduku la nguvu zako; makuhani wako, Ee BWANA, Mungu, wavikwe wokovu, watakatifu wako na washangilie mema. Ee BWANA, Mungu, usimpe kisogo masihi wako; uzikumbuke fadhili za Daudi mtumishi wako.

2 Mambo ya Nyakati 6:1-42 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo Sulemani akanena, BWANA alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Lakini nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele. Mfalme akageuza uso wake, akawabarikia mkutano wote wa Israeli; na mkutano wote wa Israeli wakasimama. Akasema, BWANA, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenena kwa kinywa chake na baba yangu Daudi, akalitimiza kwa mikono yake, akasema, Tangu siku ile nilipowatoa watu wangu katika nchi ya Misri, sikuchagua mji wo wote wa kabila zote za Israeli ili kujenga nyumba, jina langu liwe humo; wala sikumchagua mtu ye yote awe mkuu juu ya watu wangu Israeli; lakini nimeuchagua Yerusalemu, jina langu liwe humo; na Daudi nimemchagua awe juu ya watu wangu Israeli. Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako; lakini si wewe utakayeijenga nyumba hiyo; ila mwanao atakayetoka katika viuno vyako, yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu. Basi BWANA amelitimiza neno lile alilolinena; nami nimesimama mahali pa Daudi baba yangu, na kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, kama BWANA alivyoahidi, nami nimeijenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Ndimo nilimoliweka hilo sanduku, ambalo ndani yake mna agano la BWANA, alilolifanya na wana wa Israeli. Akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akainyosha mikono; (maana Sulemani alikuwa amefanya mimbari ya shaba, urefu wake mikono mitano, na upana wake mikono mitano, na kwenda juu kwake mikono mitatu, na kuisimamisha katikati ya ua; akasimama juu yake, akapiga magoti mbele ya mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake kuelekea mbinguni); akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni, wala duniani; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa moyo wao wote; uliyemtimizia mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidi; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo. Sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu machoni pangu, wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli; wakiwa tu watoto wako wataiangalia njia yao, ili kuiendea torati yangu, kama wewe ulivyokwenda mbele zangu. Basi sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako Daudi. Lakini Mungu je! Yamkini atakaa na watu duniani? Tazama, mbingu na mbingu za mbingu za mbingu hazikutoshi; siuze nyumba hii niliyoijenga! Walakini umwangalie mtumwa wako anayoyaomba, na kusihi, Ee BWANA, Mungu wangu, usikie kilio na maombi anayoyaomba mtumwa wako mbele zako; ili macho yako yafumbuke kwa nyumba hii mchana na usiku, mahali uliponena, ndipo utakapoliweka jina lako; usikie maombi atakayoomba mtumwa wako, akikabili mahali hapa. Uyasikie atakayosihi mtumwa wako, na watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, usikie toka makaoni mwako, toka mbinguni, nawe usikiapo, samehe. Ikiwa mtu amemkosea mwenzake, akitiwa kiapo, aapishwe, naye akija na kuapa hapa mbele ya madhabahu yako nyumbani humu; basi, usikie mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimlipiza mwovu, kumpatilizia njia yake kichwani; ukamfanyie haki mwenye haki, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake. Ikiwa watu wako Israeli wamepigwa mbele ya adui zao, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakirejea kwako, na kulikiri jina lako, wakikuomba na kukusihi nyumbani humu; basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watu wako Israeli, na kuwarejeza tena katika nchi uliyowapa wao na baba zao. Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, uwatesapo; basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumwa wako, na ya watu wako Israeli; uwafundishapo njia njema iwapasayo waiendee; ukainyeshee mvua nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi. Ikiwa nchi imeingia njaa, au tauni, au ukosefu wa mvua, au ukungu, au nzige, au panzi; ikiwa adui wamewahusuru katika nchi ya miji yao, au ukiwapo msiba wo wote, au uele wo wote; yo yote atakayoyaomba na kusihi mtu awaye yote, au watu wako Israeli wote pamoja, watakaojua kila mtu pigo lake mwenyewe, na msiba wake mwenyewe, akiinyoshea mikono nyumba hii; basi usikie huko mbinguni, ukaapo, ukasamehe, ukampatilize kila mtu kwa kadiri ya njia zake zote; wewe umjuaye moyo; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu); ili wakuche wewe, waziendee njia zako, siku zote watakazoishi katika nchi uliyowapa baba zetu. Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako kuu, na mkono wako ulio hodari, na mkono wako ulionyoshwa; hao watakapokuja na kuomba wakiielekea nyumba hii; basi usikie huko mbinguni, toka makaoni mwako, ukatende yote atakayokuomba huyo mgeni; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe, kama watu wako Israeli, tena wajue ya kuwa nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa jina lako. Ikiwa watu wako wametoka kupigana na adui zao, utakakowatuma ko kote, wakikuomba kuuelekea mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako; basi uyasikie huko mbinguni wayaombayo, na kusihi, ukaitetee haki yao. Wakikukosa, (maana hakuna mtu asiyekosa), hata uwakasirikie, na kuwatia mikononi mwa adui zao, wawahamishe, na kuwachukua mateka mpaka nchi iliyo mbali au iliyo karibu; basi wakikumbuka katika nchi walikohamishwa, na kutubu, na kukusihi katika nchi ya uhamisho wao, wakisema, Tumekosa, tumetenda kwa ukaidi, tumefanya maovu; wakurudiapo kwa mioyo yao yote, na kwa nia zao zote, katika nchi ya uhamisho wao, adui walikowahamisha, wakiomba na kuielekea nchi uliyowapa baba zao, na mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako; basi uyasikie toka mbinguni, toka makaoni mwako, wayaombayo, na kusihi, ukaitetee haki yao; ukawasamehe watu wako, waliokosa juu yako. Na sasa, Ee Mungu wangu, macho yako yafumbuke, nakusihi, masikio yako yakasikilize maombi yaombwayo mahali hapa. Sasa, Ee BWANA, Mungu, uondoke, uende kwenye raha yako, wewe na sanduku la nguvu zako; makuhani wako, Ee BWANA, Mungu, wavikwe wokovu, watakatifu wako na washangilie mema. Ee BWANA, Mungu, usiurudishe nyuma uso wa masihi wako; uzikumbuke fadhili za Daudi mtumishi wako.

2 Mambo ya Nyakati 6:1-42 Biblia Habari Njema (BHN)

Ndipo Solomoni akasema, “Mwenyezi-Mungu alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Hakika nimekujengea nyumba tukufu, mahali pa makao yako ya milele.” Kisha Solomoni akaigeukia jumuiya yote ya watu wa Israeli wakiwa wamesimama, akawabariki. Akasema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwani kwa nguvu yake ameitimiza ahadi yake aliyoitoa kwa baba yangu Daudi akisema, ‘Tangu niwaondoe watu wangu kutoka nchi ya Misri, sikuchagua mji wowote katika makabila ya Israeli ili nijengewe nyumba nitakamoabudiwa; na sikumchagua mtu yeyote awe mkuu wa watu wangu Israeli. Nimeuchagua mji wa Yerusalemu uwe mji ambamo nitaabudiwa, na nimemchagua Daudi awatawale watu wangu Israeli.’ “Kwa hiyo, baba yangu Daudi alikusudia kujenga nyumba atakamoabudiwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia baba yangu Daudi, ‘Ni vyema kwamba ulikusudia moyoni mwako kunijengea nyumba. Hata hivyo, si wewe utakayejenga hiyo nyumba, ila mwanao utakayemzaa ndiye atakayenijengea hiyo nyumba.’” “Na sasa Mwenyezi-Mungu ametimiza ahadi yake, kwani nimekuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, na kukikalia kiti cha enzi cha Israeli kama Mwenyezi-Mungu alivyoahidi; pia nimejenga nyumba ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Katika nyumba hiyo nimeliweka sanduku la agano, ambalo ndani yake mna agano la Mwenyezi-Mungu alilofanya na watu wa Israeli.” Kisha, Solomoni alisimama mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu halafu mbele ya jumuiya yote ya watu wa Israeli, aliinua mikono yake juu. Solomoni alikuwa ametengeneza jukwaa la shaba ambalo aliliweka katikati ya ua. Urefu na upana wake ulikuwa mita mbili na robo, na kimo chake mita moja na robo. Alipanda jukwaani na kupiga magoti mbele ya jumuiya yote ya Israeli, akainua mikono yake kuelekea mbinguni. Aliomba akisema, “Ee, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu mwingine kama wewe, mbinguni ama duniani. Wewe ni mwaminifu, kwani umetimiza agano lako na kuwaonesha fadhili zako watumishi wako wanaoishi wakikutii kwa moyo wao wote. Umetimiza ahadi uliyotoa kwa mtumishi wako baba yangu Daudi; naam, yale uliyonena umeyatimiza leo kwa uwezo wako mwenyewe. “Kwa hiyo sasa, Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ninakuomba pia utimize ile ahadi uliyomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu, ukisema, ‘Siku zote utakuwa na mzawa wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, iwapo wazawa wako watafuata kwa uangalifu sheria yangu kama wewe ulivyofanya mbele yangu.’ Sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nakusihi utimize yote uliyomwahidi mtumishi wako Daudi. “Lakini, ee Mungu kweli utakaa humu duniani na binadamu? Hata mbingu zenyewe, wala mbingu za mbingu za juu sana hazikutoshi, itakutoshaje nyumba hii ambayo nimeijenga? Hata hivyo, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mimi mtumishi wako, nakuomba unisikilize na kunitimizia ombi langu ninalokuomba leo. Ichunge nyumba hii mchana na usiku, mahali ambapo umechagua watu wako waliabudu jina lako. Unisikie mimi mtumishi wako ninapokuja mahali hapa kuomba. Sikia maombi yangu mimi mtumishi wako na ya watu wako Israeli wanapoomba wakielekea mahali hapa. Usikie maombi kutoka huko mbinguni na ukisha sikia, utusamehe. “Mtu akimkosea mwenzake, naye akaletwa apate kuapa mbele ya madhabahu yako katika nyumba hii, na akiapa tafadhali wewe usikie kutoka huko mbinguni, uchukue hatua na kuwahukumu watumishi wako. Aliye na hatia umwadhibu kadiri ya makosa yake; asiye na hatia umwachilie na kumpatia tuzo kadiri ya uadilifu wake. “Wakati watu wako Israeli watakaposhindwa na maadui zao, kwa sababu ya dhambi walizotenda dhidi yako, nao wakitubu kwako na kukiri jina lako, wakiomba msamaha wako kwa unyenyekevu katika nyumba hii, basi, usikie kutoka huko mbinguni. Usamehe dhambi zao na uwarudishe katika nchi uliyowapa wao na babu zao. “Mvua isiponyesha kwa sababu wametenda dhambi dhidi yako, wakiomba wakielekea mahali hapa na kulikiri jina lako, pia wakiziacha dhambi zao, tafadhali uwasikie kutoka huko mbinguni, na usamehe dhambi zao watumishi wako watu wako Waisraeli, huku ukiwafundisha kufuata njia nyofu, ukanyeshe mvua katika nchi yako hii ambayo uliwapa watu wako iwe mali yao. “Iwapo kuna njaa nchini au tauni, ukame, ugonjwa wa mimea, nzige au viwavi, au ikiwa watu wako wamezingirwa na maadui zao katika mji wao wowote ule; ikiwa kuna pigo lolote au ugonjwa wowote, tafadhali usikie maombi yoyote yatakayoombwa na mtu yeyote au watu wako wote wa Israeli, kila mtu akijua taabu yake na huzuni yake akikuomba huku akinyosha mikono yake kuelekea nyumba hii. Basi usikie kutoka kwako mbinguni, utoe msamaha, pia umtendee kila mtu kadiri anavyostahili, kwani ni wewe tu ujuaye mawazo ya mioyo ya wanadamu wote. Hivyo watakutii na kuenenda katika njia zako wakati wote wanapoishi katika nchi uliyowapa babu zetu. “Vivyo hivyo wakati mgeni asiye mmoja wa watu wako Israeli atakuja kutoka nchi ya mbali kwa ajili ya jina lako kuu, na kwa sababu ya nguvu na ulinzi wako, kuomba katika nyumba hii, nakusihi umsikie toka huko kwako mbinguni, na umjalie huyo mgeni yote atakayokuomba kusudi watu wote ulimwenguni wapate kujua jina lako na kukutii kama wafanyavyo watu wako Israeli na wapate kufahamu kwamba nyumba hii ambayo nimeijenga inajulikana kwa jina lako. “Watu wako wakienda vitani kupigana na maadui zao kokote kule utakakowapeleka, nao wakikuomba wakielekea mji huu uliouchagua na nyumba ambayo nimeijenga kwa ajili ya jina lako, nakusihi usikie sala yao na maombi yao ukiwa huko mbinguni na uwapatie ushindi vitani. “Ikiwa watatenda dhambi dhidi yako, maana hakuna mtu asiyetenda dhambi, na ukiwakasirikia na kuwaacha washindwe na adui, hata wapelekwe mateka mpaka nchi ya mbali au ya karibu; kama watakapokuwa huko uhamishoni watajirudi kwa roho yao yote na kwa moyo wao wote na kutubu na kukuomba msamaha, wakisema, ‘Tumetenda dhambi; tumepotoka na kufanya maovu’; pia kama watatubu kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote wakati watakapokuwa katika nchi ya uhamisho, na kama watakuomba wakielekea nchi yao ambayo uliwapatia babu zao, mji huu ambao uliuchagua na nyumba hii ambayo nimeijenga kwa ajili ya jina lako; basi, nakusihi usikie huko mbinguni uliko sala yao na maombi yao na uwapatie haki zao, uwasamehe watu wako ambao wametenda dhambi dhidi yako. “Sasa ee Mungu wangu, tuangalie na upokee maombi tutakayoomba mahali hapa. Sasa inuka ee Bwana Mungu, uingie mahali pako pa kupumzika wewe pamoja na sanduku la agano la nguvu zako. Makuhani wako ee Bwana Mungu, wapate wokovu, na watakatifu wako wafurahie wema wako. Ee Bwana Mungu, usimpige kisogo masiha wako. Kumbuka fadhili zako kwa mtumishi wako Daudi.”

2 Mambo ya Nyakati 6:1-42 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo Solomoni akasema, “BWANA alisema kwamba ataishi katika giza nene. Nimejenga Hekalu zuri kwa ajili yako, mahali pako pa kukaa milele.” Kusanyiko lote la Israeli lilipokuwa limesimama hapo, mfalme akageuka na kuwabariki. Kisha akasema: “Ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye kwa mikono yake mwenyewe ametimiza lile alilomwahidi Daudi baba yangu kwa kinywa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisema, ‘Tangu siku niliyowatoa watu wangu kutoka Misri, sikuchagua mji katika kabila lolote la Israeli ili Hekalu lijengwe humo ili Jina langu lipate kuwamo humo, wala sikumchagua mtu yeyote kuwa kiongozi wa watu wangu Israeli. Lakini sasa nimeuchagua Yerusalemu ili Jina langu lipate kuwamo humo, na nimemchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.’ “Ilikuwa moyoni mwa Daudi baba yangu kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, ‘Kwa sababu ilikuwa moyoni mwako kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu, ulifanya vyema kuwa na jambo hili moyoni mwako. Hata hivyo, sio wewe utakayenijengea Hekalu, bali mwanao, ambaye ni nyama yako na damu yako mwenyewe, yeye ndiye atakayejenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’ “BWANA ametimiza ahadi aliyoiweka: Nimeingia mahali pa Daudi baba yangu na sasa ninakikalia kiti cha ufalme cha Israeli, kama vile BWANA alivyoahidi, nami nimejenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Nimeliweka humo Sanduku la Agano, ambamo ndani yake kuna lile Agano la BWANA alilofanya na watu wa Israeli.” Kisha Solomoni akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA machoni pa kusanyiko lote la Israeli, naye akakunjua mikono yake. Basi Solomoni alikuwa ametengeneza jukwaa la shaba, urefu wake dhiraa tano, na upana wake dhiraa tano na kimo chake dhiraa tatu, naye akaliweka katikati ya ukumbi wa nje. Akapanda juu ya hilo jukwaa kisha akapiga magoti mbele ya kusanyiko lote la Israeli, akanyoosha mikono yake kwelekea mbinguni. Akasema: “Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe juu mbinguni wala chini duniani, wewe unayetunza Agano lako la upendo na watumishi wanaodumu katika njia yako kwa moyo wote. Umetimiza ahadi yako kwa mtumishi wako Daudi baba yangu, kwa kinywa chako uliahidi na kwa mkono wako umetimiza, kama ilivyo leo. “Sasa BWANA, Mungu wa Israeli, mtimizie mtumishi wako Daudi baba yangu ahadi zako ulizomwahidi uliposema, ‘Kamwe hutakosa kuwa na mtu atakayeketi mbele zangu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli, kama wanao wakiangalia yote wayafanyayo kuenenda mbele zangu kama vile ulivyofanya.’ Sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, acha neno lako lile ulilomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu litimie. “Lakini kweli, je, Mungu atafanya makao duniani na wanadamu? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga! Hata hivyo sikiliza dua ya mtumishi wako na maombi yake kwa huruma, Ee BWANA Mungu wangu. Sikia kilio na dua ambayo mtumishi wako anaomba mbele zako siku hii ya leo. Macho yako na yafumbuke kuelekea Hekalu hili usiku na mchana, mahali hapa ambapo ulisema, ‘Jina langu litakuwako humo,’ ili kwamba upate kusikia maombi ambayo mtumishi wako ataomba kuelekea mahali hapa. Usikie maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli wakati wanapoomba kuelekea mahali hapa. Sikia kutoka mbinguni, mahali pa makao yako na usikiapo, samehe. “Mtu anapomkosea jirani yake na akatakiwa kuapa, akija na kuapa mbele ya madhabahu yako ndani ya Hekalu hili, basi, sikia kutoka mbinguni na ukatende. Hukumu kati ya watumishi wako, ukimwadhibu yule mwenye hatia kwa kuleta juu ya kichwa chake yale aliyoyatenda. Umtangazie mwenye haki kwamba hana hatia, hivyo ukathibitishe kuwa haki kwake. “Wakati watu wako Israeli watakapokuwa wameshindwa na adui kwa sababu ya dhambi walizofanya dhidi yako, watakapokugeukia na kulikiri jina lako, wakiomba na kufanya dua kwako katika Hekalu hili, basi usikie kutoka mbinguni, ukasamehe dhambi ya watu wako Israeli na kuwarudisha katika nchi uliyowapa baba zao. “Wakati mbingu zitakapokuwa zimefungwa kusiwe na mvua kwa sababu watu wako wametenda dhambi dhidi yako, watakapoomba kuelekea mahali hapa na kulikiri jina lako nao wakageuka kutoka dhambi zao kwa sababu umewaadhibu, basi usikie kutoka mbinguni na usamehe dhambi ya watumishi wako, watu wako Israeli. Wafundishe njia sahihi ya kuishi na ukanyeshe mvua juu ya nchi uliyowapa watu wako kuwa urithi. “Wakati njaa au tauni vikija juu ya nchi, au koga au kawa, nzige au panzi, au wakati adui atakapowazingira katika mji wao wowote, maafa ya namna yoyote au ugonjwa wowote unaoweza kuwajia, wakati dua au maombi yatakapofanywa na mmojawapo wa watu wako Israeli, kila mmoja akitambua taabu zake na uchungu wake, naye akainyoosha mikono yake kuelekea Hekalu hili, basi usikie kutoka mbinguni, katika makao yako. Usamehe na utende, umpe kila mtu kulingana na matendo yake, kwa kuwa unaujua moyo wake (kwa kuwa ni wewe peke yako ujuaye mioyo ya watu wote), ili wakuogope kwa wakati wote watakaoishi katika nchi uliyowapa baba zetu. “Kwa habari ya mgeni ambaye si miongoni mwa watu wako Israeli, lakini amekuja kutoka nchi ya mbali kwa sababu ya jina lako kuu na mkono wako wenye nguvu ulionyooshwa, atakapokuja kuomba kuelekea Hekalu hili, basi na usikie kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, ukafanye lolote ambalo mgeni huyo anakuomba, ili mataifa yote ya dunia wapate kujua jina lako na wakuogope kama wafanyavyo watu wako Israeli nao wapate pia kujua kwamba nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa Jina lako. “Wakati watu wako watakapokwenda vitani dhidi ya adui zao, popote utakapowapeleka, wakati watakapoomba kwa BWANA kuelekea mji ambao umeuchagua, na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako, basi usikie dua na maombi yao kutoka mbinguni, ukawatetee haki yao. “Watakapotenda dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna mtu yeyote ambaye hatendi dhambi, nawe ukachukizwa nao na kuwakabidhi kwa adui, ambaye atawachukua utumwani katika nchi iliyo mbali au karibu na kama watabadilika mioyo yao katika nchi wanakoshikiliwa mateka, nao wakatubu na kukulilia katika nchi ya utumwa na kusema, ‘Tumetenda dhambi, tumefanya makosa na tumetenda uovu’; kama wakikugeukia kwa moyo wao wote na nafsi zao katika nchi ya adui zao ambao waliwachukua mateka, wakakuomba kuelekea nchi uliyowapa baba zao, kuelekea mji uliouchagua na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako, basi kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, usikie dua yao na maombi yao na kuitetea haki yao. Uwasamehe watu wako, waliotenda dhambi dhidi yako. “Sasa, Mungu wangu, macho yako na yafumbuke na masikio yako yasikie maombi yaombwayo mahali hapa. “Sasa inuka, Ee BWANA Mungu, na uje mahali pako pa kupumzikia, wewe na Sanduku la nguvu zako. Makuhani wako, Ee BWANA Mungu, na wavikwe wokovu, watakatifu wako na wafurahi katika wema wako. Ee BWANA Mungu, usimkatae mpakwa mafuta wako. Kumbuka upendo mkuu uliomwahidia Daudi mtumishi wako.”